Saintfiet akiwapungia mikono mashabiki wa Yanga SC wakati akiingia Uwanja wa jamhuri kwenye mechi iliyopita, kumbe alikuwa anawaaaga. |
Na Mahmoud Zubeiry
MABINGWA wa
soka Afrika Masharikia na Kati, Yanga SC leo wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam kumenyana na JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara.
Hiyo itakuwa
moja kati ya mechi nne za leo za ligi hiyo, nyingine zikiwa ni kati ya Azam FC na
Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, JKT Oljoro na Polisi Morogoro
kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha na Coastal Union na Toto
Africans kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mechi hiyo
inatarajiwa kuwa ngumu kwa sababu timu zote, zilifungwa katika michezo yao
iliyopita, Yanga ikichapwa 3-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Mtibwa Sugar
na JKT ikitundikwa 2-0 na mabingwa watetezi Simba SC.
Angalau, JKT
ilivuna pointi tatu kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting kwa
ushindi wa 2-1 Uwanja wa Chamazi, lakini Yanga hata mechi yake ya kwanza ya
ligi hiyo, ililazimishwa sare ya bila kufungana Prisons mjini Mbeya.
Katika mchezo
wa leo, Yanga inatarajiwa kuongozwa na kocha wake Msaidizi, Freddy Felix
Minziro, kufuatia kutupiwa virago kwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet jana usiku,
baada ya kutofautiana sera na uongozi.
Saintfiet
ameiongoza Yanga katika mechi 14 tu tangu ajiunge nayo Julai mwaka huu,
akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic na katika mechi hizo
amefungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na Atletico ya Burundi 2-0.
Katika mechi
hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico
ya Burundi.
Wachezaji wa
Yanga watacheza mechi ya leo kwa shinikizo, kwa sababu uongozi wa klabu hiyo
chini ya Mwenyekiti wake, Yussuf Mehboob Manji unaonekana kucharuka hivi sasa
na kuwa tayari kuchukua maamuzi magumu, baada ya timu kuanza vibaya katika mechi
mbili za awali za ligi hiyo.
Jana, uongozi
wa Yanga ya Dar es Salaam, ulitangaza kuisimamisha kazi Sekretarieti nzima ya
klabu, akiwemo Katibu Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu,
kutokana na kile ilichoeleza utendaji usioridhisha.
Makamu
Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwaambia Waandishi wa Habari, makao makuu
ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, kwamba maamuzi hayo yamefuatia kikao cha
Kamati ya Utendaji kilichofanyika tangu saa 5:30 hadi saa 9:30 jioni jana.
Wengine waliokumbwa
na panga hilo ni Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala, Philip Chifuka aliyekuwa
Mhasibu na Hafidh Saleh aliyekuwa Meneja ambaye anahamishiwa kwenye majukumu
mengine.
Baada ya
kuondolewa sekretarieti hiyo, sasa beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya
Tanzania, Taifa Stars, Lawrence Mwalusako atakaimu nafasi ya Katibu wa klabu
hiyo, wakati kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Sekilojo Johnson Chambua atakuwa
Meneja mpya wa klabu hiyo.
Nafasi
nyingine za Mhasibu mpya, iliyoachwa wazi na Philip Chifuka itakuwa chini ya
dada mmoja, aliyetajwa kwa jina moja tu, Rose aliyekuwa akifanya kazi ofisi
hiyo kwa muda mrefu, wakati Msemaji wa klabu iliyoachwa wazi na Louis Sendeu,
inaelezwa atapewa mdogo wa mke wa Ridhiwani Kikwete, aliyehesabu kura za
Abdallah Bin Kleb katika uchaguzi mdogo wa klabu, Julai 14.
Mapema kabla
ya kutupiwa virago jana, kocha Saintfiet alitaja wachezaji 18 wa kucheza mechi
ya leo, akimteka mshambuliaji Said Bahanuzi, mfungaji bora wa Kombe la Kagame,
lakini baada ya mabadiliko hayo hakuna hakika kama kikosi kitakuwa kile kile.
Wachezaji aliowateua
Mtakatifu Tom ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika.
Aliwataja viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Rashid Gumbo, Shamte Ally na Simon Msuva, wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza na ambao hawamo kwenye programu ya kesho ni kipa Said Mohamed, mabeki Nsajigwa Shadrack, Job Ibrahim, viungo Frank Domayo, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa Assega, na Issa Ngao wa Yanga B anayekomazwa kikosi cha kwanza na mshambuliaji Said Bahanuzi.
Mechi nyingine
za ligi zitapigwa kesho, Mgambo JKT wakimenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga, Simba SC na Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na African Lyon
na Prisons Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
MSIMAMO WA LIGI KUU BARA
P W D L GF GA GD P
Simba SC 2 2 - - 5 - 5 6
Mtibwa Sugar 2 1 1 - 3 - 3 4
Azam FC 2 1 1 - 2 1 1 4
Coastal 2 1 1 - 2 1 1 4
Ruvu
Shooting 2 1 - 1 3 3 - 3
JKT Ruvu 2 1 - 1 2 3 -1 3
African Lyon 2 1 - 1 1 3 -2 3
Toto African 2 - 2 1 3 2 1 2
JKT Oljoro 2 - 2 1 1 - - 2
Prisons 2 - 2 - 1 1 - 2
Polisi Moro 2 - 1 1 - 1 -1 1
Kagera Sugar 2 - 1 1 - 1 -1 1
Yanga SC 2 - 1 1 - 3 -3 1
JKT Mgambo 2 - - 2 1 3 -2 0
0 comments:
Post a Comment