11 wa kuaminika Yanga |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC
inashuka dimbani leo, kumenyana na African Lyon katika mfululizo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huo ukiwa mchezo wa mwisho kabla
ya kumenyana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC Jumatano.
Mechi hiyo itaanza saa 11:00 jioni na kurushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini.
Yanga leo,
itakuwa na kocha mpya kwenye benchi Mholanzi, Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus
Johannes Brandts, aliyewasili juzi na kusaini mkataba wa mwaka jana.
Brandts amesema
kwamba atajitahidi kadiri ya uwezo wake, kuhakikisha anaiongoza timu hiyo
kushinda mechi ya leo na Jumatano dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC ingawa
anajua utakuwa mtihani mgumu.
Brandts
alisema hayo, baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo mbele ya
Waandishi wa Habari, katika Mkutano uliofanyika makao makuu ya klabu, makutano
ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam asubuhi hii.
Alisema
kwanza anaushukuru uongozi wa klabu hiyo kuwa kumuamini, na anaafiki kwa kiasi
kikubwa kupewa nafasi ya kurithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet, aliyetupiwa
virago wiki iliyopita, baada ya kuitumikia Yanga kwa siku 80.
“Muhimu
kwangu, nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kuipa matokeo mazuri klabu kwa
asilimia mia moja. Nilikuwa Uholanzi, nikapigiwa simu na Mwenyekiti, Yussuf
Manji, akaniambia anataka nije kufanya kazi Yanga, nilikuwa nina ofa nyingi,
ila nilivutiwa naye (Manji), aliponiambia falsafa na sera za klabu, anataka
kuindeleza klabu.
Kitu kingine
ni kuhusu timu, kama kocha, kweli tuntaka kushinda kila mechi, lakini tunataka
kucheza soka ya kuvutia. Jambo muhimu kwangu ni kufanya kila mchezaji mmoja
mmoja acheze vizuri, na timu icheze vizuri, kwa sababu hakuna bora zaidi ya
timu,”alisema.
Brandts pia
alizungumzia nihdamu, akisema; “Kuzingatia nidhamu, ni muhimu si hapa tu
Afrika, hata Asia na Ulaya kwa sababu, ukitaka kuamka saa moja kamili amka saa
moja kamili na ukitaka kujenga timu nzuri, muhimu kujituma, hata mimi
nilipokuwa nacheza ilikuwa hivyo pia, ni muhimu kujivunia timu unayochezea na
kila mchezaji anatakiwa kujivunia kuchezea Yanga,”alisema.
Kuhusu kazi,
alisema; “Kitu kingine, kuna mechi kesho na kuna mechi Jumatano, dhidi ya Simba
itakuwa ngumu sana, tutafanya kila tunachoweza kuhakikisha tunashinda, naijua
Yanga nimekuja hapa miaka miwili, ni timu nzuri. Sasa nakwenda kujaribu
kuboresha timu, najiona mwenye bahati kusaini mkataba na timu hii,”alisema.
Brandts
alikuja mwaka jana na mwaka huu kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, akiwa na APR ya Rwanda na mara zote, Yanga iliibuka bingwa,
mwaka jana ikifundishwa na Mganda Sam Timbe na mwaka huu ikifundishwa na
Mbelgiji, Saintfiet.
Mwaka jana,
APR ilitolewa mapema katika kundi lake Morogoro, lakini mwaka huu ilifika hadi
Nusu Fainali na kutolewa na Yanga.
Awali ya
hapo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba wamepata kocha
mzoefu wa soka ya Afrika ambaye amefanya kazi APR ya Rwanda.
“Tulikuwa na
makocha wengi katika mchakato, tumekuwa makini kutokana na matatizo
yaliyojitokeza awali, tumekuwa makini na aina ya mikataba tunayoingia na
makocha, ili tusije tukarudia makosa, tumezungumza naye matatizo yaliyotokea na
kocha aliyemtangulia, ameridhika, ameona tuko sahihi, naye amesema yuko tayari
kutimiza masharti ya mwajiri wake mpya,”alisema Sanga.
Beki huyo wa
zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi,
aliwasili juzi majira ya saa 3:45 usiku katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere na ndege ya KLM na kupokewa na Katibu Mkuu wa Yanga,
Lawrence Mwalusako na viongozi wengine, Abdallah Ahmad Bin Kleb, Seif Ahmad
‘Magari’ na Majjid Suleiman.
Yanga,
imetimiza malengo yake ya kuwa kocha mpya, kabla ya kucheza na wapinzani wao wa
jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kumfukuza Mbelgiji, Tom Saintfiet,
kutokana na kuwasili kwa Brandts, ambaye anaanza kazi mara moja leo.
Kikosi cha
Yanga kipo kambini, hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam na kabla ya
kucheza na Simba Jumatano, kesho kitacheza na African Lyon, Uwanja wa Taifa
pia.
Mholanzi
huyo aliyemaliza mkataba wake APR ya Rwanda baada ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Agosti mwaka huu amepewa ukocha wa Yanga,
baada ya Mbrazil Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Mtaalamu
huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV
Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea
mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza
Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika
fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa
mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali
za Kombe la Dunia.
Alianza
kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi
ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi
na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu
soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa
hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya
tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha
mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa
kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR
ya Rwanda mwaka 2010, ambako ‘riziki’ yake imeisha miezi miwili iliyopita na
sasa amepata maisha mapya Yanga.
Akiwa APR,
Brandts alifungwa mechi zote mbili na Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mbelgiji
Tom Saintfiet katika Kombe la Kagame, moja ya makundi 2-0 na nyingine ya Nusu
Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa, ikiifunga Azam FC 2-0 kwenye fainali.
Brandts
atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza
msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima anayeingia katika
msimu wa pili, ambao alifanya nao kazi APR.
Tayari Yanga
imecheza mechi tatu za Ligi Kuu, kushinda moja, sare moja na kufungwa moja-
hivyo inaachwa kwa mbali na wapinzani wake wakuu katika mbio za taji, Simba SC
yenye pointi 12 na Azam FC yenye pointi 10, baada ya mechi nne.
Ushindi leo
ni muhimu kwa Yanga, kwani utaifanya iwasogelee wapinzani wake Azam kwa tofauti
ya pointi mbili, kutoka nne hadi saba.
0 comments:
Post a Comment