Mbuyu Twite |
Na Mahmoud Zubeiry
HAIKUWA mbaya Yanga kumsajili Mbuyu Twite, kwa sababu baada
ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan, beki mwingine wa kati waliyekuwa
naye ni Ibrahim Job pekee.
Niliamini kusajiliwa kwa Twite, maana yake Yanga itakuwa na
mabeki wawili wa kati uwanjani na wawili benchi, lakini sasa si hivyo.
Ni kama Yanga imeridhika na uchezaji wa pamoja wa Yondan na
Cannavaro, lakini inalazimisha na Twite acheze.
Mwanzoni, Twite alikuwa anapangwa kama kiungo mkabaji, lakini
akashindwa kucheza kwa ubora wa Athumani Iddi ‘Chuji’, hivyo akahamishiwa beki
ya pembeni.
Morogoro dhidi ya Mtibwa alipangwa beki ya kushoto, akawa
uchochoro wa Hussein Javu na Jumamosi dhidi ya JKT Ruvu alicheza beki ya kulia-
pia sikuridhishwa na uchezaji wake, naamini Juma Abdul, Godfrey Tauta, au Nahodha
Nsajigwa Shadrack, yeyote angecheza vema zaidi yake.
Mechi na JKT Ruvu ilikuwa nyepesi kwa Yanga na timu ilishinda
na kwa desturi yetu Watanzania, timu inaposhinda watu hawaangaalii makosa ua
mapungufu ya timu.
Twite ni beki wa kati na naamini anaweza kucheza vizuri
nafasi hiyo tu, hizo nyingine analazimishwa kwa sababu ni mchezaji nyota na
wenye timu yao hawataki aanzie benchi.
Lakini wapo watu waliosajiliwa maalum kwa ajili ya nafasi
hizo, tena wengi mno. Katika nafasi ambazo Yanga imewekeza vizuri kwenye timu
yake, basi ni mabeki wa pembeni.
Kulia peke yake wapo watatu, Nsajigwa, Abdul na Taita na
kushoto pia wapo watatu, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika, sasa
kama beki wa kati anapelekwa pembeni, hawa waliosajiliwa kwa ajili ya kucheza
nafasi hizo wacheze wapi?
Hapa sasa unaweza kuona Twite anaivuruga Yanga kwa
kulazimishwa kucheza na kitu kingine ambacho sielewi Yanga ni kuwachezesha
mbele mabeki wa pembeni, wakati timu ina viungo wengi tu wa pembeni.
Mara nyingi makocha wengi duniani hutumia mabeki mbele katika
kujihami na sana hutokea katika mechi ngumu, kama fainali kocha anajua
anakutana na timu yenye kushambulia sana, hivyo anaongeza wakabaji uwanjani.
Lakini kwa Yanga, sasa imekuwa desturi tangu wakati wa Sam
Timbe, hata Tom Saintfiet, ingawa juzi Kaimu Kocha Mkuu, Freddy Felix Minziro alibadilisha
mfumo huo na tuliona kasi ya mashambulizi Yanga iliongezeka na ikapata ushindi
mnono wa 4-1 dhidi ya JKT Ruvu.
Lakini kwa nini Minziro alimpanga Twite beki ya kulia, wakati
Nsajigwa, Taita na Juma Abdul wapo na hawakuwa wagonjwa?
Hakuna sababu ya Yanga kulazimisha kumchezesha Twite, waachwe
mabeki wote wanne wa kati, wapiganie namba mazoezini ili pia na kujenga nidhamu
ya uwajibikaji, au labda tuambiwe naye amesaini mkataba kama alisoaini Juma
Kasaeja na Yanga mwaka 2009, lazima acheze.
0 comments:
Post a Comment