Jeshi la Jiwe |
Na Mahmoud Zubeiry
“Amri Kiemba na Jonas Mkude ndio viungo pekee wakabaji katika
Simba kwa sasa ambao siku za karibuni hawapangwi- mi nitabaki kuwa mwandishi na
mchambuzi, lakini Profesa Milovan Cirkovick ni kocha na mtaalamu, hivyo anajua
anachokifanya”.
Hii ni sehemu ya makala yangu ya BIN ZUBEIRY Septemba 9,
mwaka huu, kwa wasomaji wangu wazuri bila shaka watakuwa wanaikumbuka vema.
Niliandika makala hii, wakati huo Simba inaboronga na katika
upangaji wa kikosi, Kocha Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick alikuwa hampi
nafasi kiungo Amri Kiemba ‘Jeshi la Jiwe’.
Baada ya makala hii, naamini ujumbe ulifika na akaanza kumpanga
Kiemba, ambaye jana amecheza mechi ya nne tangu Ngao ya Jamii na katika mechi
zote timu imecheza vema na kushinda, mchango wake ukionekana ‘wazi wazi’.
Nilisema katika makala yangu ya Septemba 9, katika soka,
kitaalamu mabeki wakiwa wanamrudishia mipira mingi kipa basi kuna tatizo kwenye
kiungo pale chini katika kuiunganisha timu na hilo ndilo lilikuwa linajitokeza Simba
wakati ule.
Simba ilikuwa inacheza vizuri ikiwa na mpira, kwa sababu ina
viungo wengi wachezeshaji, lakini tatizo linakuja mpira unapohamia kwa
wapinzani- wanapita kiulaini na safu ya ulinzi ya klabu hiyo inafikiwa mno,
tena kwa urahisi.
Mipira ilikuwa ikipenyezwa mno kwenye eneo la hatari la
Simba- sasa nikasema ni vema kabla ya kuanza kuwatazama mabeki, Simba waimulike
safu yao ya kiungo.
Tazama jinsi Kiemba anavyoiongoza timu kwa sasa, yaani mabeki
wanakula raha tu na hata idadi ya mipira ambayo Juma Kaseja amekuwa akirudishiwa
imepungua mno, kwa sababu yupo mtu anayeiunganisha timu pale nyuma.
Kiemba |
Jana Simba imefungwa bao la kwanza katika Ligi Kuu, baada ya
mechi tatu na bao lenyewe ni makosa ya watu wawili, Kaseja na Nyosso, kupeana pasi
kwenye eneo la hatari bila umakini. Kaseja alimpa pasi Nyosso, kabla hajaumiliki
sawa sawa mpira, mtu akaupitia akaenda kufunga.
Kuna tatizo ambalo Nyosso anatakiwa alifanyie kazi, kuweza kumiliki
mpira katika mguu wa pili, fuatilia sana beki huyo kuna mguu ambao hauwezi
kabisa kumiliki mpira.
Ili kujijengea uwezo wa kumiliki mpira kwa miguu yote miwili,
Nyosso anatakiwa kufanya mazoezi ya kupiga danadana za miguu yote- kuuchezea
sana mpira kwa mguu wa pili. Akiwa mazoezini autumie sana huo mguu unaokataa
mpira, ili uuzoee mpira.
Lakini hata Kaseja anatakiwa kuonyesha maana ya kuzoeana kwake
na Nyosso kwa kutompa pasi katika mazingira yale, kwa sababu jana halikuwa bao
la kwanza beki huyo anamfungisha kipa wake- si mnakumbuka lile la Davies Mwape?
Mshambuliaji akimuweka Nyosso kulia kwake, basi atafanikiwa
na beki huyo anachoweza kufanya ni kumkwatua tu. Kwa sababu ule mguu mwingine
hauwezi kuupitia mpira.
Nikirejea kwenye mada, naamini sasa tatizo la Simba
limegundulika na limepatiwa tiba, si beki. Ilikuwa kiungo wa chini. Ila sasa,
Kiemba ni bindamu na ni mchezaji, kuna kuugua, kuumia au kuwa nje kwa adhabu,
nani mbadala wake?
Yupo dogo Mkude, Milovan anapaswa kumuweka tayari huyu kijana
katika programu zake. Nilikuwa nawakumbusha tu, maana kipindi kile wachambuzi
uchwara wa kibongo ‘walizomoka’ vitu ambavyo sivyo. Endelea kusoma
bongostaz.blogspopt.com ya BIN ZUBEIRY.
0 comments:
Post a Comment