Salum Abubakar 'Sure Boy Jr' |
Na
Princess Asia
VIUNGO wawili tegemeo wa Azam FC na ambao hivi sasa
wako juu ile mbaya kimchezo, Ibrahim Mwaipopo na Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’
ni majeruhi na daktari wa timu hiyo, Dk Mwanandi Mwankemwa ‘anaenda mbio’
kuhakikisha wanakuwa fiti kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii, Septemba 11 dhidi ya
Simba.
Viungo hao tegemeo hakuwemo kwenye mechi ya kirafiki
jana dhidi ya Coastal Union ya Tanga, kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Simba.
Katika mechi hiyo iliyokuwa tamu, mabao mawili ya
John Raphael Bocco ‘Adebayor’ katika dakika za 15 na 44, yaliipa Azam FC
ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Chamazi.
Bocco alikuwa mwiba mchungu kweli jana kwa safu ya
ulinzi ya Coastal, kwani pamoja kufunga mawili, lakini alikosa mabao matatu ya
wazi mno katika mechi ambayo, kiungo Abdulhalim Humud alitolewa nje kwa kadi
nyekundu dakika ya 32 kwa rafu na lugha chafu.
Hiyo ni mechi ya tano Coastal inafungwa kati ya sita
za kujipima nguvu ilizocheza kabla ya jana kufungwa 2-1 na Yanga, awali
ilifungwa 3-2 na Bandari mjini Mombassa, baadaye 2-0 Tanga, ilifungwa 2-1 na
Polisi mjini Morogoro na yenyewe iliifunga JKT Oljoro 1-0.
Kwa Azam hiyo ni mechi ya tatu mfululizo ya kujipima
nguvu wanashinda, awali walizifunga 1-0 Prisons ya Mbeya na Transit Camp 8-0.
Azam inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao
ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo
wake wa kwanza katika historia ya Ngao hiyo.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya
Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa
soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba
kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001,
Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi
ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare
ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga
Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na
Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na
Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na
beki mahiri Shomari Kapombe, aliyemajeruhi kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment