Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC imeahirisha
safari yake ya kwenda Zanzibar kuweka kambi ya kujiandaa na pambano la Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3,
mwaka huu, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na sasa badala ya asubuhi, itaondoka
jioni saa 9:00 leo.
Simba SC
imefanya mazoezi katika ufukwe wa Cocoa Beach, Dar es Salaam leo asubuhi na
jioni itaondoka kwenda kisiwani humo kwa maandalizi ya kuendeleza ‘mila’ ya
kuwanyanyasa wapinzani wao jadi, Yanga.
Wekundu hao
wa Msimbazi wanakwenda Zanzibar na Jumamosi watarejea mara moja Dar es Salaam
kucheza na Prisons na baada ya hapo, watapanda bosi kurejea visiwani humo
kuendelea na maandalizi yao.
Katika
mchezo huo, Simba SC, iko hatarini kumkosa mshambuliaji wake hodari wa
kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, iwapo Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, itaamua kufuata kanuni za Ligi zinavyosema.
Okwi alipewa
kadi nyekundu ya moja kwa moja, kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa JKT
Ruvu, akilipa kisasi cha kuzewa rafu Jumatano iliyopita, Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam na kwa mujibu wa kanuni hilo ni kosa la kufungiwa mechi tatu.
Hata hivyo,
Okwi anaweza kuokoka, iwapo tu ripoti za refa na Kamisaa zitambeba, ingawa hilo
ni gumu, kwa sababu hakupewa kadi ya moja kwa moja kwa kucheza rafu wala
kuushika mpira kwa makusudi, bali kupiga na hilo adhabu yake ni kukaa jukwaani
mechi tatu.
Tayari Okwi
amekosa mechi moja ya juzi dhidi ya Ruvu Shooting na wakati, Kamati ya Ligi Kuu
inakutana kesho, inatarajiwa kumuongezea mechi mbili zaidi, dhidi ya Prisons na
dhidi ya Yanga na baada ya hapo atakuwa huru kuendelea kumtukia mwajiri wake.
Siyo siri,
kuelekea pambano la watani wa jadi, Okwi ni homa kwa Yanga, hasa wakikumbuka
namna alivyowanyanyasa katika mechi iliyopita, akifunga mabao mawili kwenye
ushindi wa 5-0 na kusababisha mawili.
0 comments:
Post a Comment