11 wa ushindi Simba SC jana |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC inaondoka
leo Dar es Salaam kurejea visiwani Zanzibar, ambako imeweka kambi ya kujiandaa
na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC Jumatano ijayo.
Simba
inarejea Zanzibar, baada ya jana kuendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa kuichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea Ligi Kuu
msimu huu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya
Simba yalitiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho Ngassa, ambaye hilo ni
bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ndani ya mechi nne na la pili jumla tangu
ajiunge na timu hiyo katika mechi saba alizocheza, wakati la Prisons lilifungwa
na Elias Maguri.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 12 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi Azam
FC pointi mbili katika nafasi ya pili, ingawa timu zote zimecheza mechi sawa,
nne.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zikwishafungana bao 1-1, Prisons wakitangulia
kupata bao dakika ya sita baada ya Maguri kuwatoka mabeki wa Simba kupiga shuti
lililomgonga Shomary Kapombe na kumchanganya kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja na kutinga
nyavuni.
Baada ya bao
hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa Prisons waliendelea
kuwa wagumu, hadi walipojisahau kidogo sekunde za mwishoni za kipindi cha
kwanza na Felix Sunzu akatumia pasi ya Amiri Maftah kusawazisha dakika ya 45.
Kipindi cha
pili, Simba walirudi na moto na kuanza moja kwa moja kulishambulia mfululizo
lango la Prisons na dakika ya 55 Ngassa akafunga kwa shuti dhaifu, ambalo kipa wa
Prisons, David Abdallah alidaka lakini mpira ukamtoka na kuingia nyavuni.
Mechi hiyo
ilichezeshwa na refa, Paul Soleji kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Jesse Erasmo,
mshika kibendera namba moja, Mwarabu Mumba mshika kibendera namba mbili, wote
kutoka Morogoro, wakati refa wa Akiba alikuwa Israel Nkongo wa Dar es Salaam.
Dakika ya 87
Amir Maftah alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Khalid Fupi wa Prisons,
hivyo ataukosa mchezo ujao dhidi ya Yanga Jumatano na hiyo ni nafasi kwa
chipukizi Paul Ngalema.
Hiyo inakuwa
kadi ya pili nyekundu kwa Simba ndani ya mechi nne, awali katika mechi ya pili
dhidi ya JKT Ruvu, Emmanuel Okwi alilimwa kadi ya aina hiyo kwa kumpiga kiwiko
Kessy Mapande na akafungiwa mechi tatu.
Simba sasa
inarejea kambini kwake visiwani Zanzibar kuendelea na maandalizi ya mchezo wa
Jumatano, wakati watani wao, Yanga walioweka kambi Changanyikeni, Dar es Salaam
kesho watacheza na African Lyon Uwanja wa Taifa.
Smba: Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’,
Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/Salim
Kinje, Ramadhan Chombo/Jonas Mkude, Christopher Edward/Daniel Akuffo, Felix
Sunzu na mrisho Ngassa.
Prisons: 18.David Abdallah, 03.Aziz Sibo, 05.Laurian
Mpalile, 16.Lugano Mwangama (Nahodha), 15.David Mwantika, 13.Khalid Fupi, 07.Misango
Magai, 12.Fred Chudu/22.Julius Kwaga, 14.Elias Maguri, 17.Peter Michael/Sino
Augustino na 19.John Matei/11.Hamisi Ally.
MSIMAMO
WA LIGI KUU BARA
P W D L GF GA GD P
Simba SC 4 4 - - 9 2 7 12
Azam FC 4 3 1 - 6 1 5 10
Coastal 3 2 1 - 5 3 2 7
Prisons 4 1 2 1 4 4 - 5
JKT Oljoro 3 1 2 1 2 1 1 5
Mtibwa Sugar 3 1 1 1 3 1 2 4
Yanga SC 3 1 1 1 4 4 - 4
Toto African 3 - 3 1 3 2 1 3
Ruvu Shooting 3 1 - 2 4 5 -1 3
African Lyon 3 1 - 2 2 5 -3 3
JKT Ruvu 4 1 - 3 3 10 -7 3
Polisi Moro 3 - 2 1 - 1 -1 2
Kagera Sugar 3 - 1 2 2 4 -2 1
JKT Mgambo 3 - - 3 1 3 -2 0
0 comments:
Post a Comment