Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC
inashuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na
Prisons ya Mbeya katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mchezo
ambao utaanza saa 1:00 usiku na kuonyeshwa moja kwa moja Televisheni ya Super
Sport ya Afrika Kusini.
Huo utakuwa
mchezo wao wa mwisho kabla ya kushuka dimbani Jumatano kumenyana na wapinzani
wao wa jadi, Yanga SC katika mfululizo wa ligi hiyo.
Aidha, Simba
SC itahitaji ushindi katika mchezo wa leo, ili kurejea kileleni, kufuatia Azam
FC jana kuitandika JKT Ruvu 3-0 kupaa kileleni, sasa ikiwazidi Wekundu wa
Msimbazi pointi moja.
Lakini mbele
ya Prisons, kwa wenye kukumbuka historia ya mechi baina ya timu hizo, kabla
haijashuka Daraja, kama imerejea na makali yale yale, mchezo wa leo utakuwa
mgumu.
Katika mchezo
wa leo, kocha Mserbia wa Simba, Milovan Cirkovick anatarajiwa kuwakosa wakali
wake wawili, Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye ni mgonjwa na Emmanuel Okwi,
anayetumikia adhabu.
Boban aliingia
dakika za mwishoni kwenye mechi iliyopita ya Ligi Kuu kati ya Simba na Ruvu
Shooting, kwa sababu alikuwa anaumwa na hakwenda kambini wenzake, kwa kuwa
alikuwa anajisikilizia afya yake.
Kuna
uwezekano mkubwa Boban akapanda boti na wenzake na baada ya mechi ya leo, dhidi
ya Prisons.
Japo Boban
hakuwa kambini Zanzibar, lakini Simba SC inaendelea vizuri na maandalizi yake
ya pambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, ikifanya
mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislam, Kwerekwe, visiwani Zanzibar na kambi
yao ipo Chukwani.
Morali ya
kambi ipo juu na wachezaji wote wako fiti, wakijifua kwa shauku kubwa ili
kumvutia kocha Mserbia, Milovan Cirkovick awape nafasi ya kucheza Oktoba 3,
kuanzia sa 1:00 usiku.
Simba inarejea
leo Dar es Salaam kucheza mechi na Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, na baada
ya mchezo huo itarejea tena visiwani humo kuendelea na maandalizi ya mchezo wa
Jumamosi ijayo.
Hata hivyo,
katika mechi ya Yanga pia, Simba itamkosa mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel
Okwi ambaye amefungiwa na Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, chini ya
Mwenyekiti wake, Wallace Karia, sambamba na kumtoza faini ya Sh. 500,000 kwa
kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa JKT Ruvu, Kessy Mapande.
Okwi
alifanya hivyo akilipa kisasi cha kuchezewa rafu Jumatano iliyopita, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Tayari Okwi
amekosa mechi moja dhidi ya Ruvu Shooting na wakati, na sasa atakosa mechi
mbili zaidi, dhidi ya Prisons na dhidi ya Yanga na baada ya hapo atakuwa huru
kuendelea kumtumikia mwajiri wake.
Siyo siri,
kuelekea pambano la watani wa jadi, Okwi alikuwa ni homa kwa Yanga, hasa
wakikumbuka namna alivyowanyanyasa katika mechi iliyopita, akifunga mabao
mawili kwenye ushindi wa 5-0 na kusababisha mawili.
0 comments:
Post a Comment