Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
BAADA ya mwezi na ushei wa kuwa kambini nje ya Dar es Salaam,
Alhamisi wiki hii wapenzi wa Simba SC watapata fursa ya kuiona tena timu yao
ikicheza mbele ya mechi yao, itakapomenyana na waliowahi kuwa mabingwa wa Kenya,
Sofapaka FC Uwanja wa Taifa.
Msemaji wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ ameiambia
BIN
ZUBEIRY leo kwamba, mechi hiyo itakuwa ya mwisho kabla ya kucheza na
Azam FC, Septemba 11, mwaka huu katika mechi ya Ngao ya Jamii.
Kamwaga alisema kwamba Simba itarejea kesho Dar es Salaam na
kuendelea na mazoezi katika Uwanja wa Sigara, Chang’ombe ikisubiri kukipiga na
Azam FC.
Kwa sasa kiwango cha Simba, inayofundishwa na Mserbia,
Profesa Milovan Cirkovick, akisaidiwa na Mganda, Richard Hamatre, kipo vizuri
na timu inaonekana iko tayari kwa Ligi Kuu. Pamoja na jana kulazimishwa sare ya
1-1 na Sony Sugar ya Kenya, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, lakini
Simba ilicheza soka safi na washambuliaji wake walikosa mabao ya wazi zaidi ya
matano.
Lakini hata hali mbaya ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika
eneo la kuchezea inachangia kupunguza idadi ya mabao kwa Simba.
Katika mechi tatu ambazo Simba imecheza kwenye Uwanja huo,
imevuna mabao matano na kufungwa matatu, na kikwazo kimekuwa kikionekana ni
hali ya eneo la kuchezea.
Katika mchezo wa jana, bao la Simba lilifungwa na Daniel
Akuffo, wakati Komabil Keita alijifunga katika jitihada za kuokoa na kuwapa
Wakenya bao la kusawazisha.
Awali, Simba ilicheza mechi mbili Arusha, dhidi ya Mathare
United ya Kenya na JKT Oljoro ya Arusha, ambazo zote ilishinda 2-1,
mshambuliaji mpya Daniel Akuffo kutoka Ghana akifunga bao moja kila mechi,
Kiggi Makaasy na Mrisho Ngassa wakifunga mabao mengine.
Kitu moja tu ambacho Milovan anapaswa kuendelea kufanyia kazi
ni makosa ya safu ya ulinzi na mawasiliano duni na makipa wao.
Ilivyo sasa kipa yeyote anayesimama kwenye lango la Simba SC,
kabla ya kuchunga wachezaji wa timu pinzani, anakuwa na jukumu la kwanza la kujihadhari
na mabeki wake wasimfunge, kwani mabeki wote wa kati wa timu hiyo wamekwishaonyesha
‘kipaji cha kujifunga’ katika mechi za karibuni,
Juma Nyosso, Paschal Ochieng na Komabil Keita.
Simba inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 11, mwaka
huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo kihistoria hiyo itakuwa mechi ya
tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kukutanisha timu nje ya
wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na
ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu
ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia
bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba
na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na
mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga
Yanga mabao 2-0.
MABINGWA WA
MECHI ZA NGAO YA JAMII:
Mwaka Mshindi Matokeo
2001 Yanga 2-1 Simba
2010 Yanga
0-0 Simba (3-1penalti)
2011 Simba
2-0 Yanga
0 comments:
Post a Comment