Mbwana Samatta, tegemeo la Mazembe |
Na
Prince Akbar
WASHAMBULIAJI wawili chipukizi wa kimataifa wa
Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu, leo wanatarajiwa
kuiongoza timu yao, Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
kwenye Uwanja wao wa nyumbani, mjini Lubumbashi katika mchezo wa Ligi ya
Mabingwa Afrika, Kundi B.
Mbwana ni mchezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha
Mazembe kwa mwaka wa pili sasa, lakini Ulimwengu alipandishwa kikosi hicho kwa
mara ya kwanza mwezi uliopita, baada ya kukaa kikosi cha wachezaji wa akiba
tangu asajiliwe katikati ya mwaka jana.
Ulimwengu alikuwa kwenye benchi kwa dakika zote 90 wakati
Mazembe, ikiifunga Zamalek ya Misri
mabao 2-1 kwenye Uwanja wa chuo cha Jeshi, Al-Qahirah mjini Cairo, katika
mchezo uliopita wa michuano hiyo ambao, Mtanzania mwenzake, Samatta ‘Sama Goal’
alifunga bao la ushindi dakika ya 44, akiunganisha pasi ya Tressor Mputu Mabi.
Katika mchezo huo wa Kundi B, Himoonde alitangulia
kuifungia Mazembe inayofundishwa na Lamine N'Diaye dakika ya 34, pasi ya Mputu,
lakini Omotoyossi akaisawazishia Zamalek inayofundishwa na kocha Jorvan Vieira
dakika ya 36, pasi ya Mohamed Ibrahim.
Ushindi huo wa kwanza ugenini kwa Mazembe katika
hatua ya makundi, uliifanya Mazembe ifikishe pointi saba, baada ya kucheza
mechi nne, kushinda mbili, sare moja na Berekum Chelsea na kufungwa moja na Al
Ahly ugenini.
Al Ahly iliyotoa sare ya 1-1 na Berekum Chelsea
nchini Ghana katika mechi yake iliyopita, bado inaongoza kundi hilo kwa pointi
zake 10, wakati wababe wapya wa Ghana wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao
tano na Zamalek wanashika mkia wakiwa hawana pointi hata moja.
Sasa Ahly na TPM zinawania uongozi wa kundi ili
kujihakikishia kutinga Nusu Fainali kabla ya mechi za mwisho za Kundi hilo,
ambazo Ahly watamaliza na Zamalek Cairo na Mazembe watamaliza Berekum Chelsea
nchini Ghana. Kila heri vijana wa Kitanzania na ndio maana ya kusema kila la
heri TPM.
0 comments:
Post a Comment