Na Mahmoud Zubeiry |
KILA siku najaribu kutafuta suluhisho la mataizo ya soka
yetu- matatizo ni mengi. Mengi sana, ila kubwa ni kukosa viongozi wabunifu,
weledi, watendaji bora, wawajibikaji na wenye mipango thabiti.
Rafiki yangu Tom Saintfiet, kocha Mbelgiji wa Yanga, jana lilimtoka
neno, nasema lilimtoka kwa sababu ilitokana na hasira, baada ya mechi kati ya
timu yake na Coastal Union kuchelewa kuanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo nusura uvunjike, baada ya Saintfiet kutoa timu
uwanjani kutokana na kucheleweshwa kwa muda wa kuanza, ambao kimakubaliano
ulikuwa saa 10:00 jioni.
Lakini Coastal walichelewa kufika uwanjani (walifika saa
10:05 jioni ) na kuanza kwanza kupasha misuli moto, jambo ambalo lilimkera
Saintfiet na kusistiza waachane na mazoezi yao mechi ianze, lakini makocha wa
timu hiyo ya Tanga, Juma Mgunda na Habib Kondo waliendelea na biashara yao.
Saintfiet akatoa timu yake uwanjani, kabla ya kwenda
kubembelezwa na viongozi wake, ndipo akarejesha timu na mpira ukaanza saa 10:31
jioni. Kabla ya kuingiza timu uwanjani, akiwa kwenye chumba cha kubadilishia
nguo, alisema kwa hasira; “Hii ndio maana soka ya nchi hii haiwezi kuendelea,
nchi hii haiwezi kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika wala Kombe la Dunia kwa
sababu kama hizi,”alisema.
Hiyo ni sehemu ndogo sana kati ya sehemu kubwa ya matatizo ya
soka yetu, ambayo unaweza kuiita uswahili na hiyo ni desturi kubwa katika
maisha ya kila siku ya Watanzania wengi, kutozingatia muda na ahadi.
Kwangu, bado naamini tatizo kubwa ni viongozi. Nchi haijapata
viongozi wa soka ambao, wanaweza kuwapa matumaini Watanzania. Wiki iliyopita
mada yangu ilikuwa ni kuhusu namna ambavyo TFF (Shirikisho la Soka Tanzania)
lilivyopoteza udhamini wa michuano ya Kombe la Taifa kwa kushindwa kusoma
ishara za nyakati.
Na nikaahidi, leo nitazungumzia namna ambavyo TFF wanashindwa
kuwapa ushauri na mwongozo wawekezaji katika soka yetu.
Wawekezaji kwenye soka ni neno lenye maana pana na si
wadhamini tu kama wengi wanavyodhani- yeyote ambaye anawekeza nguvu na mali
yake kwa manufaa ya soka ya Tanzania, basi huyo ni mwekezaji na mdau mkubwa.
Hii inatuhusu hata waandishi, mashabiki, wamiliki wa timu na
kadhalika, wakiwemo wadhamini.
Wafanyabiashara watano maarufu, Mohamed Dewji, Thomas Molel
‘Askofu’, Sam Ruhuza, Merey Balhaboub na Alex Kajumulo wote wamewahi kumiliki
timu ambazo zimewahi kushiriki Ligi Kuu, lakini walichemsha kutokana na
kujikuta wanaziendesha kwa hasara.
TFF ndio wenye soka yao, wanapaswa kuwa na kitengo maalum cha
ushauri na mwongozo kwa wadau kama hawa, ili waepuke kuendesha timu kwa hasara-
lakini haiko hivyo. Mtu anawekeza mamilioni yake kuanzisha timu, lakini mwisho
wa siku anakuja kugeuka adui wa wenye soka yao, kwa sababu tu ni watu ambao ama hawajui, au wameweka mbele
maslahi binafsi.
Anapambana na hila za hujuma na upendeleo, ambazo mara nyingi
zinaanzia kwa viongozi wa TFF, wenye imani bila Simba na Yanga mambo hayawezi
kwenda- hapo hapo watu wanaota mabadiliko, wanaota mapinduzi. Yatoke wapi?
Kuna nini pale Kenya hata Sofapaka imeweza kudumu na ni timu
ya juzi tu, wakati Pallson, African Lyon (ya Dewji), Mmbanga FC, Kajumulo WS na
Moro United ya Merey zimeshindwa kudumu Tanzania?
Haya ndio mambo ambayo lazima ifike wakati watu wajiulize na
majibu yake yanaweza kusaidia ustawi wa timu nyingine za wadau waliojitokeza
kupiga jeki soka la Tanzania kama Said Salim Bakhresa, au Rahim ‘Zamunda’
Kangezi aliyeipokea Lyon.
Kuandika mambo kama haya, lengo lake ni kuwaonyesha viongozi
wetu wapi wanakosea ili waweze kurekebisha- si kwa ajili ya kujenga chuki na
kununua uadui. Si kwamba kuna mtu hatakiwi au anapigwa vita, la hasha.
Wakati nakua, nilikua nikistaajabu sana moja ya sifa kubwa za
kupata ajira mbali na elimu ni uzoefu- vema katika moja ya sifa za kuwa
kiongozi wa TFF ni uzoefu. Na uzoefu lazima uendane na sifa ya kuweza kuchanganua
mambo na si kuishi kama roboti, kuishi kwa dhana na hisia badala ya kuipa fursa
akili yako ifanyie kazi mambo.
Nasema hivi kwa sababu ya lile neno anatumiwa. Anayejaribu
kuelezea mapungufu ya wakubwa, basi huyo anatumiwa. Kwa nini basi tusiachane na
dhana hiyo na badala yake tuzitathmini hoja zinazotolewa?
Tumepoteza Kombe la Taifa? Ndiyo. Kwa sababu gani? Jibu ndio
msingi wa hoja na si hizo fikra za roboti, aliinunua babu hadi mjukuuu
anatumia. Tujadili hali halisi na tuache kuishi kwa mazoea. Ni ujinga. Samahani
ujinga si tusi, ni moja kati ya maadui watatu, ambao baba wa taifa letu,
marehemu Mwalimu Julius Nyerere alipambana nao mapema tu ili kujenga Tanzania
bora, wengine wakiwa ni maradhi na umasikini.
Hivi karibuni ilifanyika michuano ya Bank ABC Sup8R
ikishirikisha timu nne kutoka kila upande na wakubwa wakasema, michuano hii ni
maalum ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu.
Bank ABC waliwekeza fedha nyingi kwenye michuano hiyo, lakini
ukiirejea michuano ile na hata dhana iliyotajwa na TFF na ukatazama mapungufu
ya michuano katika soka yetu, ambayo yametokana na ukosefu wa wadhamini,
unagundua ushauri bora ulikosekana hapa.
Najiuliza, kwa nini TFF wasingeketi chini na Bank ABC
wakawashauri wawe wadhamini wakuu wa Kombe la FA? Wawe wadhamini wakuu wa Ligi
Kuu ya Vijana? Wawe wadhamini wakuu wa timu za vijana? Wawe wadhamini wakuu wa
timu ya wanawake?
Kombe la FA lina wigo mpana sana, likishirikisha kuanzia
klabu za Ligi ya kata hadi Ligi Kuu na mwisho wa siku kwa mujibu wa kanuni
linatoa mwakilishi wa nchi kwenye michuano ya Afrika.
Timu za vijana zinaweza kumtangaza mdhamini hadi kwenye Kombe
la Dunia, iwapo zitafanya vizuri, jambo ambalo msingi wake ni maandalizi mazuri
kadhalika na timu ya wanawake.
Mfano hii U17, imetinga Raundi ya Pili baada ya Kenya kujitoa
na kama ikiitoa Misri, itabakiza mtihani mmoja ili kufuzu Fainali za Mataifa ya
Afrika kwa vijana wa umri huo, ambako ikiingia Nusu Fainali tu, itakuwa
imejihakikishia kucheza Fainali za Kombe la Dunia.
Mimi nadhani, baada ya kuvaa suruali na shati, kuliko kununua
kofia, bora viatu- sasa na TFF wanapaswa kutazama maeneo ya muhimu ya kuwekeza
kwanza kwa ajili ya ustawi wa soka yetu. Alamsiki!
0 comments:
Post a Comment