Papic kushoto akiwa na BIN ZUBEIRY enzi zake Yanga |
Na Mahmoud Zubeiry
ALIYEKUWA
kocha wa klabu ya soka ya Yanga ya Dar es Salaam, Kostadin Bozidar Papic amefungua
mashitaka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), dhidi ya klabu hiyo, akidai
malimbikizo yake ya mishahara, dola za Kimarekani 12,300, zaidi ya Sh. Milioni
15 za Tanzania.
Katibu Mkuu
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah Malabeja ameiambia BIN
ZUBEIRY leo mchana kwamba, wamepokea barua kutoka Kitengo cha Sheria
cha FIFA, kiwataka tuitaarifu Yanga kuhusu mashtaka yaliyowasilishwa na kocha
wao huyo zamani, raia wa Serbia.
Angetile amesema
Katika malalamiko yake, Papic anadai kuwa hajalipwa malimbikizo ya mshahara
wake yanayofikia kiasi cha dola 12,300 za Kimarekani. Katika barua yake, kocha
huyo anadai kuwa alikuwa akiwasiliana na maofisa na viongozi waYanga, lakini
hakupata ushirikiano na hivyo kuamua kwenda FIFA.
Angetile alisema
TFF ilifanya juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko hayo ili kujaribu
kumzuia kocha huyo asishtaki FIFA, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.
“Na kama
chombo kinachosimamia uendeshaji wa soka nchini, TFF imesikitishwa na habari
hizo na inaiomba klabu ya Yanga kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa
inawasilisha taarifa zote muhimu na nyaraka zinazohusiana na stahiki za kocha
huyo ili kama ilishamalizana naye, sifa ya klabu ya Yanga isafishwe,”alisema Angetile.
Alisema tayari
wamekwishaiandikia barua Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapema
iwezekanavyo.
“Tukio hilo,
si tu linachafua sifa ya klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania kwa ujumla
kutokana na ukweli kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la malipo ya makocha
nchini, ni dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu zetu na hata timu za taifa
kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya
kazi nchini,”alisema.
Hili ni
tukio la pili kwa Yanga baada ya mchezaji wake mwingine, John Njoroge kuishtaki
klabu hiyo FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa mwezi Januari na Kitengo cha
Usuluhishi wa Migogoro cha FIFA (DRC).
Alisema ushindi
wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza kumlipa mchezaji
huyo kasi cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika adhabu ambayo itailazimisha
TFF kuishusha daraja; kuinyang’anya pointi kwa kiwango kitakachotajwa na FIFA;
kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa pamoja.
“Tunaiomba
Yanga itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa kwenye barua ya FIFA ili
kuepuka hatua hizo, suala la Njoroge ni
moja kati ya matukio mengi yanayohusu ukiukwaji wa taratibu za kuvunja mikataba
yanayofanywa na klabu zetu.
Kuna
malalamiko ya wachezaji wengi dhidi ya klabu zao za zamani kuhusu kutolipwa
stahiki zao. Hivyo TFF inatoa wito kwa klabu kujiepusha na vitendo hivyo kwa
kuwa vinawanyima haki wachezaji, lakini pia vinachafua sifa ya nchi iwapo
wachezaji wanachukua hatua za kwenda kwenye vyombo vya juu,”alisema Wambura.
Aidha, Angetile
amesema kwamba wamekuwa wakisoma kwenye vyombo vya habari kuhusu kutimuliwa kwa
sekretarieti nzima ya Yanga kutokana na kuonekana kuwa ina udhaifu, lakini taarifa
hizo hazijaifikia rasmi TFF.
Alisema kiutaratibu,
Yanga inatakiwa iwsasilishe majina ya maofisa watakaofanya kazi na TFF kwa sasa
na itakapoajiri sekretarieti ya kudumu, basi itume barua nyingine ya
kuwatambulisha watendaji wake.
Alisema kama
Yanga itakuwa imeitimua sekretarieti nzima, basi TFF inapokea taarifa hizo kwa
masikitiko makubwa kwani pamoja na kwamba si nia ya TFF kutetea watendaji
wazembe, lakini klabu hazina budi kufuatilia kwa karibu utendaji wa
sekretarieti zao ili isije ikafikia wakati sekretarieti nzima inaondolewa kwa
makosa ambayo yangeweza kusahihishwa kama kungekuwa na ufuatiliaji wa karibu.
“TFF imekuwa
ikitoa mafunzo kwa watendaji wa klabu ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kwa
mintaarafu ya mpira wa miguu na hivyo kuondolewa kwa timu nzima kama hiyo
kunamaanisha kuwa ni upotevu wa rasilimali ambayo imetumika kuwapa elimu ya
kutenda kazi zao vizuri. TFF ilishafanya kozi ya Event Management kwa ajili ya
watendaji wa klabu; semina ya kuangalia upya maazimio ya Bagamoyo kwa watendaji
na viongozi na pia kozi ya utawala hivyo haipendi juhudi hizi zipotee kirahisi,”alisema
Angetile.
0 comments:
Post a Comment