Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea leo
kwa mechi tatu kupigwa kwenye viwanja tofauti, macho na masikio ya wengi
yakielekezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako mabingwa watetezi, Simba SC
watakuwa wakimenyana na Ruvu Shooting ya Pwani.
Simba imeshinda mechi zake zote mbili za awali, dhidi ya
African Lyon mabao 3-0 na JKT Ruvu 2-0 na inahitaji ushindi katika mchezo wa
leo, ili kurudi kileleni, baada ya Azam jana kuifunga Mtibwa Sugar na kuukamata
usukani wa ligi.
Simba leo itamkosa mshambuliaji wake hatari, Mganda Emanuel
Arnold Okwi lakini kocha Mserbia, Milovan Cirkovick anatarajiwa kumrudisha
uwanjani mshambuliaji Mzambia, Felix Mumba Sunzu.
Bado safu ya ushambuliaji ya Simba ina wakali wengine kama Mghana,
Daniel Akuffo na mzalendo Mrisho Ngassa, ambao wakiongozwa na viungo mahiri
kama Haruna Moshi ‘Boban’ na Mwinyi Kazimoto, moto unatarajiwa kuwa ule ule.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya Mgambo JKT na
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na African Lyon na Prisons kwenye
Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Katika mechi za jana, Yanga ilipata ushindi wa kwanza ndani
ya mechi tatu za ligi hiyo, baada ya kuifunga JKT Ruvu mabao 4-1 kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Hadi mapumziko Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0,
yaliyotiwa kimiani na Nahodha, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ dakika ya nne na
Didier Kavumbangu dakika ya 31, mabao yote yakitokana na kazi nzuri ya kiungo
mshambuliaji Simon Msuva.
Bao la kwanza ulikuwa mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna
Niyonzima, baada ya Msuva kuangushwa karibu kabisa na eneo la hatari la JKT
Ruvu na bao la pili dogo huyo aliyesajiliwa kutoka Moro United iliyoshuka
daraja, alimpa pasi mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kavumbangu.
Kipindi cha pili, Yanga walirudi tena kwa kasi na kufanikiwa
kupata bao la tatu dakika ya 52, mfungaji Simon Msuva kabla ya Didier
Kavumbangu kufunga la nne dakika ya 65.
JKT ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 68 mfungaji
Credo Mwaipopo.
Katika mchezo wa leo, Yanga ilicheza vizuri, wachezaji
wakionana kwa pasi nzuri ndefu na fupi, tofauti na ilivyokuwa kwenye iliyopita
mjini Morogoro, ambako walifungwa 3-0 na Mtibwa Sugar.
Ikumbukwe mechi ya kwanza, Yanga ililazimishwa sare ya bila
kufungana na Prisons mjini Mbeya.
Yanga jana ilicheza chini ya kocha Msaidizi, Freddy Felix
Minziro, baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet kusitishiwa
mkataba juzi usiku, kufuatia kutofautiana na uongozi.
Kwenye Uwanja wa Chamazi, wenyeji Azam FC waliifunga Mtibwa
Sugar 1-0, bao pekee la Kipre Herman Tchetche, wakati Uwanja wa Sheikh Amri
Abeid Arusha wenyeji JKT Oljoro 1-0 wameifunga Polisi Morogoro, bao pekee la
Paul Ndonga dakika ya 13 na Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga wenyeji Coastal Union wamelazimishwa sare ya bila kufungana na
Toto Africans.
MSIMAMO WA LIGI KUU
BARA
P W D L GF GA GD P
Azam FC 3 2 1 - 3 1 2 7
Simba SC 2 2 - - 5 - 5 6
Coastal 3 1 2 - 2 1 1 5
JKT Oljoro 3 1 2 1 2 1 1 5
Mtibwa Sugar 3 1 1 1 3 1 2 4
Yanga SC 3 1 1 1 4 4 - 4
Ruvu Shooting 2 1 - 1 3 3 - 3
JKT Ruvu 3 1 - 2 3 7 -4 3
African Lyon 2 1 - 1 1 3 -2 3
Toto African 3 - 3 1 3 2 1 3
Prisons 2 - 2 - 1 1 - 2
Polisi Moro 3 - 1 2 - 2 -2 1
Kagera Sugar 2 - 1 1 - 1 -1 1
JKT Mgambo 2 - - 2 1 3 -2 0
0 comments:
Post a Comment