Uwanja mpya wa Kaunda utakavyokuwa |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya Yanga ipo katika mkakati wa kujenga Uwanja mpya wa
kisasa sambamba na kukarabati jengo la makao makuu ya klabu, liliopo makutano
ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Habari ambazo, BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani
ya Yanga, zimesema kwamba tayari mkandarasi amekwishaptikana na amefikia
makubaliano na uongozi wa klabu hiyo.
Habari zaidi zinasema, Uwanja mpya wa Kaunda utakuwa na uwezo
wa kuchukua mashabiki 40,000 na eneo la maegesho ya magari yasiyopungua 1,000
na zoezi la ujenzi wa Uwanja huo, litaanza kabla ya tarahe ya mwisho ya mwaka
huu.
Inadaiwa mradi huo, utafadhiliwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo,
Yussuf Mehboob Manji, ambaye amedhamiria kufanya mambo mengine makubwa, kubadilisha
kabisa sura na hadhi ya klabu hiyo, ili viendane na klabu nyingine kubwa Afrika.
Wachezaji wakiwa mazoezini Uwanja wa Kaunda wa sasa |
Ili kuhakikisha anapata timu nzuri ya kufanya nayo kazi, Manji
aliwapigania Clement Sanga, Abdallah Bin Kleb, Mussa Katabaro, George Manyama
na Lameck Nyambaya aingie nao madarakani.
Katika timu hiyo, iliyopewa jina ‘Jeshi la Miamvuli’ Sanga
alifanikiwa kuwa Makamu Mwenyekiti, Bin Kleb, Manyama na Katabaro wakipata
Ujumbe wa Kamati ya Utendaji, wakati Nyambaya alizidiwa kura na Aaron Nyanda.
Uwanja wa Kaunda na jengo la sasa la klabu, vilijengwa kwa
nguvu za wanachama wake, chini ya Mwenyekiti wake wa kwanza, Mangara Tarbu
miaka ya 1970 pamoja na msaada wa rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amaan
Karume.
Ingawa historia inasema Yanga ilizaliwa mwaka 1935 na Simba
mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa
utani na upinzani wa jadi, baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs, ambayo mwaka 1938
ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa
ikiitwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs,
vijana wa Dar es Salaam walikuwa wana desturi ya kukutana viwanja vya Jangwani
kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina
Jangwani.
Unavyoonekana Uwanja wa Kaunda hivi sasa |
Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha
timu hiyo, ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa Bandarini na
mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo wa bandarini.
Hiki ndio choo cha Uwanjda wa Kaunda |
Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo
walikuwa wakitembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani, kwamba wao ndiyo zaidi.
Kwa sababu katika kipindi hicho, Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa
soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita
Taliana.
Taliana ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza
ilipopanda hadi Ligi Daraja la Pili Kanda ya Dar es Salaam, mwanzoni mwa miaka
ya 1930. jina la Taliana waliamua kuachana nalo mapema, kabla ya kuingia kwenye
ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
Lakini kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya
vitu pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs, waliweza kutwaa Kombe la Kassum,
lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam.
Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs, 1938 wakati
baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland. Kwa sababu
hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans, jina ambalo
mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema
Yanga.
Miongoni mwa wachezaji wa mwanzoni kabisa wa Yanga ni kipa
Taha Athumani, Saidia Msafiri na Jamil Ramadhan. Waliofuatia walikuwa ni kipa
Abdulhamid Ramadhan, aliyewika na kuisaidia Tanganyika kutwaa Kombe la Gossage
(sasa Challenge) katika miaka ya 1949 na 1950.
0 comments:
Post a Comment