Na Ally Mohamed, Zanziabr
MABINGWA wa zamani wa Zanzibar, Malindi jioni hii
wamelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Mafunzo katika mfululizo wa Ligi
Kuu ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan, Zanziabr.
Malindi walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 30
likifungwa na Amour Suleiman, ambalo lilidumu hadi dakika 45 za kipindi cha
kwanza, kabla ya Mafunzo kusawazisha dakika ya 72 kupitia kwa Ali Juma.
Katika dakika ya 88, Renatus Morris aliipatia Malindi bao la
pili na wakati watazamaji wakiamini Malindi wataondoka na pointi tatu, Jaku
Juma alizima ndoto za Malindi baada ya kuifungia Mafunzo bao la kusawazisha dakika
ya 89.
Kisiwani Pemba, mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Gombani, Pemba
Chipukizi waliifunga Duma, inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) mabao
2-1.
Mabao ya Chipukizi yalifungwa na Faki Mwalim na Abdulkarim
Ali, wakati bao pekee la Duma likifungwa na Maulid Ramadhan.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo mmoja katika
uwanja wa Amaan kisiwani Unguja kwa Mtende Rangers ambaom wamepanda daraja
msimu huu kucheza na Mundu.
Katika mechi za jana, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar,
Super Falcon waliendelea kuboronga katika ligi hiyo licha ya kumtimua kocha wake
wiki iliyopita, baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Jamhuri ya Pemba, kwenye Uwanja
wa Gombani, Pemba, wakati Bandari imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya KMKM Uwanja
wa Amaan, Zanzibar.
Uwanja wa Gombani, Falcon ambao wataiwakilisha Zanzibar
katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, walikubali kipigo cha tatu mfululizo
katika ligi hiyo kwa mabao ya Mfaume Shaaban na Abdallah Mohammed, hiyo ikiwa
mechi ya nane kwa Super Falcon kupoteza.
Bandari iliyopanda Ligi Kuu msimu huu ilipata bao lake la
kwanza dakika ya 37, lililotiwa kimiani na Mussa Omar, kabla ya KMKM kusawazisha
dakika ya 44, mfungaji Mudrik Muhib na Bandari wakapata bao la ushindi dakika 76
kupitia kwa Mohammed Abdallah.
0 comments:
Post a Comment