SIKU 80, mechi 14 na taji moja, vimetosha kukamilisha historia ya mtaalamu wa soka kutoka Ubelgiji, Tom Saintfiet ndani ya klabu ya Yanga.
Na Mahmoud Zubeiry |
Hiyo inafuatia kufukuzwa kwa Kocha huyo juzi usiku na nafasi
yake sasa anakaimu Msaidizi wake, Freddy Felix Minziro hadi hapo
atakapopatikana kocha mwingine.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwaambia
Waandishi wa Habari jana asubuhi, makao makuu ya klabu, makutano ya Mitaa ya
Twiga na Jangwani kwamba, matokeo mabaya ndio yamefanya Saintfiet asitishiwe
mkataba.
Aidha, Sanga alikanusha madai kwamba eti kocha huyo
amefukuzwa baada ya kutofautiana na Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji.
“Timu ilipokwenda Mbeya, ikatoka sare na Prisons akalalamikia
huduma, lakini sisi taarifa tulizozipata, yeye alikwenda kulewa na wachezaji.
Kuna mapungufu mengine mengi, ambayo hatuwezi kusema hadharani.
Kwa mfano timu ilipotoka Mbeya, tulitaka iende moja kwa moja
Morogoro, yeye akalazimisha timu irudi Dar es Salaam, tena iende tena Morogoro.
Wachezaji wakachoka sana na hii tunaamini ilichangia hata kufungwa na Mtibwa.
Timu iliporudi kutoka Morogoro, tukaamua iingie kambini, yeye
akapinga akisema timu kubwa kama Barcelona Ulaya, hazikai kambini, yaani
anataka atupangie kazi sisi, tukaona huyu mtu haendani na maadili ya uongozi na
hatufai, tukaamua kusitisha mkataba wake,” alisemsa Sanga.
Saintfiet ameiongoza Yanga katika mechi 14 tu ndani ya siku
80 tangu ajiunge nayo Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin
Bozidar Papic na katika mechi hizo amefungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na
Atletico ya Burundi 2-0.
Katika mechi hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati, Kombe la Kagame, ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi
moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi.
Pamoja na kufukuzwa kwa kocha, Yanga imemtangaza rasmi beki
wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Lawrence
Mwalusako kukaimu nafasi ya Katibu wa klabu hiyo na Dennis Oundo kuwa kaimu
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.
Hatua hiyo, inafuatia kusimamishwa kazi kwa Sekretarieti
nzima ya klabu, akiwemo Katibu Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis
Sendeu, kutokana na kile ilichoeleza utendaji usioridhisha.
Wengine waliokumbwa na panga hilo ni Masoud Saad, aliyekuwa
Ofisa Utawala, Philip Chifuka aliyekuwa Mhasibu na Hafidh Saleh aliyekuwa
Meneja ambaye anahamishiwa kwenye majukumu mengine.
Mbali na Mwalusako na Oundo, kiungo wa zamani wa klabu hiyo,
Sekilojo Johnson Chambua anatajwa kupewa nafasi ya Umeneja, wakati nafasi ya Msemaji
wa klabu iliyoachwa wazi na Louis Sendeu, inaelezwa atapewa mdogo wa mke wa
Ridhiwani Kikwete, aliyehesabu kura za Abdallah Bin Kleb katika uchaguzi mdogo
wa klabu, Julai 14.
Ni ukweli usiopingika kwamba wana Yanga wengi wamesikitishwa
na uamuzi wa kufukuzwa kwa Mbelgiji huyo, siku 80 tangu apokewe kwa sherehe
kubwa akiwasili nchini kwa ajli ya kufanya kazi Jangwani.
Wanakumbuka walivyosherehekea naye ubingwa wa Kagame.
Wanakumbuka alivyokuwa akiiongoza vema timu hiyo na zaidi wanakumbuka ahadi
zake, ambazo hajapewa fursa ya kuzitimiza, ikiwemo ubingwa wa Afrika.
Uongozi wa Yanga unawajibika kwa wanachama na mwisho wa siku
juu ya uendeshwaji wa timu, hakuna anayeweza kuwaingilia kwa sababu hilo ndilo
jukumu walilopewa na wenye timu yao.
Tom ameondolewa. Kocha mcheshi, asiye mwoga mbele ya vyombo
vya habari, na ambaye katika kipindi kifupi cha kuwapo kwake nchini alijiengea
umaarufu mkubwa kwa kazi nzuri na ushirikiano pia na wadau.
Kwaheri Tom, kocha ambaye akiwa Ethiopia alipewa jina la
utani Mtakatifu na vyombo vya habari kutokana na jinsi alivyokubalika, wakati
akiifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo.
Tumesikia sababu za uongozi kumfuta kazi Tom, na hata bila ya
kuzijadili huu ni mwendelezo wa desturi ya Yanga kutodumu na makocha. Sijui kwa
sababu gani.
Tangu mwaka 1991, Saintfiet anakuwa kocha wa 18 kutupiwa
virago Yanga na katika kipindi chote hicho ni makocha watatu tu, waliorudishwa
kazini, baada ya kuondoka, ambao ni Syllersaid Mziray (sasa marehemu), Mmalawi Jack
Chamangwana na Mserbia Kostadin Papic.
Baadhi ya makocha waliamua kuondoka wenyewe, lakini wengi wao
walifukuzwa na tawala mbalimbali zilizopita katika klabu hiyo katika kipindi
chote hicho.
Kwa nini nimeanzia 1991, ndicho kipindi ambacho vurugu vurugu
za kufukuza makocha zilipoanza katika klabu hiyo, tofauti na miaka ya nyuma
tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1939.
Mapema mwaka 1991, Yanga ilimchukua kocha maarufu zamani
nchini, Syllersaid Salmin Kahema Mziray, ambaye aliondoka kwa watani wa jadi,
Simba SC, baada ya kushushwa cheo kutoka Simba A hadi Simba B.
Mziray aliiongoza Yanga kwa miaka miwili, akiwa anasaidiwa na
Charles Boniface Mkwasa na akaiwezesha kutwaa ubingwa wa Bara na Muungano mfululizo,
sambamba na kuwafikisha Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
ambako walifungwa kwa matuta na watani wa jadi, Simba SC.
Lakini baada ya hapo, marehemu Mziray aliondoka Yanga
kutokana na kupata ofa nzuri kutoka Pan African, wakati huo ikiwa inafadhiliwa
na Murtaza Dewji, ambaye alikuwa anaipigania irejee Ligi Kuu.
Yanga iliajiri tena kocha wa kigeni baada ya muda mrefu,
ikimleta Mrundi, Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ 1993 (sasa marehemu) ambaye
aliendelea kufanya kazi na Mkwasa na katika mwaka wake wa kwanza, akaiwezesha
timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame mjini Kampala, Uganda.
Tauzany aliporejea katika Ligi Kuu akaendelea vizuri na kazi,
lakini haikuchukua muda akaingia kwenye mgogoro na mfadhili wa klabu hiyo wakati
huo, Abbas Gulalamli (sasa marehemu).
Tauzany alitumia vyombo vya habari kupambana na Gulamali na
ilifikia hadi akawa anachafua jina lake kwa kusema anafanya biashara haramu. Ilikuwa
vita kali na mbaya zaidi hata Mrundi hiyo alikuwa anakubalika mbele ya wanachama,
hivyo kumfukuza ikawa tabu.
Alichokifanya Gulamali, akamrejesha kocha ambaye alifanya
kazi na kupendwa mno Yanga, Tambwe Leya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), ambaye awali alifanya kazi mwaka 1975 na 1976, akiiwezesha Yanga
kuifunga Simba katika mechi ya kihistoria Nyamagana kabla ya kuipa Kombe la
kwanza la Kagame 1975, kwa kuwafunga hao hao Simba 2-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Tambwe alitua nchini mwishoni mwa mwaka 1994 na jukumu lake
alilopewa ni Ukurugenzi wa Ufundi, ambapo yeye akaamua kutengeneza timu nzuri
ya vijana, iliyopewa jina Black Stars.
Tauzany na kikosi cha Yanga chenye mastaa kibao nchini wakati
huo, akafungwa mabao 4-1 na Simba SC na hapo ndipo timu nzima na kocha wao
wakafukuzwa, wakabaki wachezaji saba tu ambao waliunganishwa na yosso wa Tambwe
kutengeneza kikosi kipya, kilichofanya vizuri hadi kufika Robo Fainali ya Kombe
la Washindi 1996.
Tambwe naye akaondolewa kwa visa na badala yake akaajiriwa
kocha mzalendo, Sunday Burton Kayuni 1997 ambaye naye pia hakudumu, kwani
alikfukuzwa na akaajiriwa kocha wa muda kutoka Uingereza, Steve McLennan mwaka
huo huo 1997.
McLennan, kocha Mzungu wa kwanza mimi kufanya naye kazi Yanga,
aliondolewa naye na nafasi yake akakaimu kwa muda aliyekuwa Msaidizi wake, Juma
Pondamali ‘Mensah’.
Siwezi kusahau siku alipofukuzwa McLennan, alimfuata msaidizi
wake ambaye aliachiwa timu na kumuuliza; “Juma nani ni kocha mzuri, mimi au
wewe?” Pondamali akawa anacheka tu, wapo kwenye basi timu inatoka Zanzibar kwenye
mechi za Ligi ya Muungano.
Yanga ikaajiri kocha wa muda, ambaye alikuwa hajulikani
kabisa, Tito Oswald Mwaluvanda (sasa marehemu) ambaye katika kujikosha kwa
wanachama, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo wakati huo, Rashid Ngozoma
Matunda (sasa marehemu pia) akawa anamtambulisha kama Msimamizi wa mazoezi,
wakati timu inatafuta kocha.
Msimamizi wa mazoezi alichukua ubingwa wa Ligi Kuu na Ligi ya
Muungano 1998, tena akiweka rekodi ya ushindi mnono zaidi katika Ligi ya Bara,
mabao 8-0 waliyoifunga Kagera Shooting Stars (sasa Kagera Sugar), tena ikiwa
inafundishwa na kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati huo, Zacharia
Kinanda ‘Arrigo Sachi’ (sasa marehemu), Edibilly Jonas Lunyamila akifunga mabao
matano peke yake.
Mungu amrehemu Kinanda, lakini siku hiyo Lunyamila
alimfikishia ujumbe, kwani kocha huyo alikuwa hamtaki Eddy katika timu ya
taifa- hivyo zile bao tano alizofunga ilikuwa ujumbe tosha, kwamba alikuwa
anakosea.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Mwaluvanda aliifikisha Yanga hadi
hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, akiweka rekodi mbili kuifanya hiyo iwe
klabu ya kwanza Tanzania kucheza hatua hiyo, yeye kuwa kocha wa kwanza mzalendo
na wa mwisho hadi sasa kuifikisha timu katika hatua hiyo.
Lakini pamoja na yote, mwaka 1998 mara tu baada ya Yanga
kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, marehemu Mwaluvanda aliyekuwa
anasaidiwa na Freddy Felix Isaya Kataraiya Minziro ‘Majeshi’ wakaondolewa wote
na akaajiriwa kocha kutoka DRC, Raoul Jean Pierre Shungu aliyeingia na msaidizi
wake, Abeid Mziba ‘Tekero’.
Hii ilimuuma sana Mwaluvanda, kwa sababu ili kuingia hatua ya
makundi ilibidi azitoe Rayon ya Rwanda iliyokuwa inafundishwa na Shungu na
baadaye Coffee ya Ethiopia, lakini marehemu akawa anasema afadhali angeletwa
kocha mwingine, si yule ambaye ameitoa timu yake kwenye mashindano. Wakubwa wakishaamua
huwezi kupingana nao.
Shungu aliipa Yanga Kombe la tatu la Kagame, katika michuano
iliyofanyika mjini Kampala, Uganda 1999, lakini mwaka 2000 akaondolewa na
akaajiriwa Charles Boniface Mkwasa ‘Master’, ambaye naye mwishoni mwa mwaka
2001, akatupiwa virago pia.
Tangu 2002 hadi sasa ni miaka 10 tu, lakini katika kipindi
hicho Yanga imefundishwa na makocha 11, tena wengine wakifukuzwa na kurudishwa
kwenye kipindi hicho.
Alipoondolewa Master Mkwasa, akaajiriwa Mmalawi Jack Lloyd
Chamangwana ambaye mwaka 2003, alifukuzwa na mwaka 2004 akaajiriwa kocha kutoka
DRC, Jean Polycarpe Bonghanya ambaye naye hakudumu, mwaka huo huo akaondolewa na
kurudishwa Syllersaid Mziray.
Marehemu Mziray alikuwa anasoma ishara za nyakati tu, naye alipoona
upepo unaelekea kuwa mbaya akamuachia timu aliyekuwa Msaidizi wake, Kenny
Mwaisabula.
Mwaisabula akaendelea na kazi hadi msimu wa 2005, lakini
baadaye mwaka huo akaondolewa na kurejeshwa Chamangwana., ambaye alifanya kazi
hadi 2007 alipompsha Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’.
Micho aliondoka kwa sababu ambazo hadi leo bado hazieleweki,
kwani alikubalika na timu ilikuwa inafanya vizuri. Alipoondoka Micho, timu
akabakia nayo, aliyekuwa kocha wa makipa, Mkenya Razack Ssiwa.
Ssiwa akaiongoza Yanga kutwaa Kombe la Tusker mwaka 2007
mjini Mwanza, lakini aliporudi kwenye ligi, timu inafanya vibaya, naya
akatupiwa virago na kurejeshwa Chamangwana.
Chamangwana naye akaondolewa na kuajiriwa tena Mserbia,
Profesa Dusan Savo Kondic, aliyekuja na Wasaidizi wawili, Spaso Sokolovoski na
Civojnov Serdan. Kondic naye mwaka 2010 akafukuzwa na kuajiriwa Mserbia
mwenzake, Kostadin Papic, ambaye naye alifukuzwa na kuajiriwa Mganda Sam Timbe.
Timbe pamoja na kuipa timu Kombe la nne la Kagame mwaka jana,
alifukuzwa miezi miwili baadaye na kurejeshwa Papic, ambaye pia hata kabla
msimu uliopita wa Ligi Kuu haujamalizika, akatupiwa virago na kuajirwa
Mbelgiji, Saintfiet.
Saintfiet amehitimisha historia yake Yanga ndani ya siku 80,
akicheza mechi 14, akishinda 12, sare moja na kufungwa mbili- huku akiacha Kombe la tano la Kagame
Yanga. Kwaheri Mtakatifu Tom, hiyo ndiyo Yanga!
MAKOCHA YANGA TANGU 1991
1.
1991:
Syllersaid Mziray(marehemu)
2.
1993:
Nzoyisaba Tauzany (marehemu) (Burundi)
3.
1995:
Tambwe Leya (marehemu) (DRC)
4.
1997:
Sunday Kayuni
5.
1997:
Steve McLennan (Uinegereza)
6.
1998:
Tito Mwaluvanda(marehemu)
7.
1999:
Raoul Shungu (DRC)
8.
2001:
Charles Boniface Mkwasa
9.
2002:
Jack Chamangwana (Malawi)
10. 2004: Jean Polycarpe Bonganya (DRC)
11. 2004: Syllersaid Mziray (marehemu)
12. 2005: Kenny Mwaisabula
13. 2006: Jack Chamangwana (Malawi)
14. 2007: Milutin Sredojevic ‘Micho’ (Serbia)
15. 2007: Razack Ssiwa (Kenya)
16. 2007: Jack Chamangwana (Malawi)
17. 2008: Dusan Kondic (Serbia)
18. 2010: Kostadin Papic (Serbia)
19. 2011: Sam Timbe (Uganda)
20. 2011: Kostadin Papic (Serbia)
21. 2012: Tom Saintfiet (Ubelgiji)
0 comments:
Post a Comment