Kibaden wa tatu kutoka kushoto enzi zake, akiwa na kikosi cha Simba SC miaka ya 1970 |
Na Mahmoud Zubeiry
SASA ni miaka 35, tangu mmoja wa washambuliaji hodari kabisa
kuwahi kutokea ardhi ya Tanzania, Abdallah ‘King’ Kibadeni, aweke rekodi ya
kufunga mabao matatu katika mechi moja, kwenye mapambano ya watani wa jadi,
Simba na Yanga.
Kibadeni |
Wengi wamejaribu kutaka kuvunja rekodi hiyo na wa mwisho
alikuwa ni Mganda, Emmanuel Okwi aliyeishia kwenye mabao mawili katika mechi
iliyopita ya watani, ambayo Yanga ililala 5-0.
Ilishindikana mtu kuvunja rekodi hiyo mbele ya ‘Yanga
Mdondo’, Mei 6, mwaka huu na je itawezekana kweli Oktoba 3, kila timu
ikionekana kupania na iko vizuri? Labda!
Kucheza Simba au Yanga ni fahari kwa mchezaji wa Tanzania.
Lakini ni fahari zaidi iwapo atakuwa mchezaji ambaye atashiriki mechi baina ya
timu hizo.
Inakuwa fahari zaidi iwapo mchezaji atafunga bao au mabao
katika mechi ya watani wa jadi, kwani huwafanya maelfu ya mashabiki wa timu
yake walitaje jina lake na kushangilia kwa raha zao. Wengine, hupewa zawadi kutokana
na kufunga kwenye mechi hizo za watani.
Wapo waliolewa sifa na kupotea kwenye ramani ya soka haraka,
kwa sababu tu ya kuvimba kichwa baada ya kufunga mabao mfululizo kwenye mechi
za watani.
Said Sued 'Scud', alifunga bao pekee la ushindi kwenye mechi
ya watani wa jadi, akiwa anaichezea Yanga alitikisa nyavu za Simba dakika ya
saba katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi Kuu Mei
18, mwaka 1991.
Huo ukiwa msimu wake wa kwanza kwenye klabu hiyo, hakika
ilikuwa furaha kubwa kwake, kwani tangu hapo aliaminika na kuwa mchezaji wa
kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
Chipukizi huyo wa wakati huo, alipata ngekewa ya kuifunga
tena Simba katika mchezo uliofuata wa marudiano wa ligi baina ya watani wa
jadi, likiwa pia bao pekee la ushindi Agosti 31, mwaka huo huo 1991, jambo
ambalo lilimfanya awe maarufu zaidi.
Lakini katika mastaajabu ya wengi, Scud hakurejea kwenye
kikosi cha Yanga cha mwaka 2002 na huo ukawa mwisho wa umaarufu wake kwenye
soka ya Tanzania.
Kama wapo wanaodhani Scud alifanya kubwa sana katika historia
ya watani wa jadi, watakuwa wapo mbali kabisa na ukweli, kwani Kibadeni,
maarufu kama Chifu Mputa ama King, au Ndululu kama walivyokuwa wakimuita
Wakenya, anaweza kusimama na kusema ana kubwa la kujivunia katika historia ya
mechi baina ya Simba na Yanga ambalo hadi kitabu hiki kinaingia sokoni lilikuwa
halijavunjwa.
Abdallah Kibadeni ndiye mchezaji pekee hadi sasa aliyeweza
kufunga mabao matatu peke yake katika mchezo mmoja kwenye mechi za watani wa
jadi katika Ligi.
Hiyo ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977 katika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, sasa Uwanja wa Uhuru, wakati Yanga ilipotandikwa 6-0 na Simba.
Siku hiyo, Kibadeni alitikisa nyavu za Yanga katika dakika za
10, 42 na 89, wakati mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi, yalitiwa kimiani na
Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 na jingine Selemani Sanga wa
Yanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20 katika harakati za kuokoa krosi ya
Ezekiel Greyson 'Jujuman'.
Hivyo siku hiyo mbali na Simba kushangilia kulipa kisasi cha
kulala 5-0 kwa Yanga, Juni Mosi mwaka 1968, Kibadeni alikuwa ana sherehe
binafsi za kutumbukiza tatu peke yake kwenye mechi baina ya watani hao, jambo
ambalo liliwashinda wengi kabla yake kati ya waliowahi kuvaa jezi za Simba au
Yanga.
Hakuna cha Sunday Manara 'Computer' wala Maulid Dilunga
'Mexico' aliyewahi kufanya hivyo zaidi ya King Kibadeni pekee. Sasa baada ya
miaka 35 tangu Kibadeni awaokoteshe Yanga mipira nyavuni mara tatu, miamba hiyo
inakutana tena Jumatano ya wiki ijayo, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, je
rekodi hiyo itavunjwa? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
0 comments:
Post a Comment