Ngassa |
Na Mahmoud Zubeiry
OKTOBA 3, mwaka huu, nyasi za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
zitawaka moto kwa mpambano mkali wa wapinzani wa jadi katika soka ya Tanzania,
Simba na Yanga, huo ukiwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, baina ya miamba hiyo.
Kama kuna wachezaji ambao tayari wamekwishaanza kuupa joto
kali mchezo huo, basi miongoni mwao ni Mrisho Khalfan Ngassa, kiungo
mshambuliaji aliye katika msimu wa kwanza Simba SC katika mkataba wake wa miaka
miwili.
Akiwa ana jezi ya Simba, hiyo itakuwa mechi yake ya kwanza dhidi
ya Yanga, timu yake ya zamani, ambayo aliichezea tangu mwaka 2007 hadi 2010 alipotimkia
Azam FC, ambayo Agosti imemtoa kwa mkopo kwa Wekundu wa Msimbazi, walioongeza
naye mkataba wa mwaka mmoja.
Wengi hata mashabiki wa Simba SC, wanaamini Ngassa ni Yanga
na yupo Msimbazi kwa ajili ya kazi na maslahi na kuelekea mechi ya watani
Oktoba 3, anakabiliwa na changamoto ya kufanya kile ambacho walifanya wachezaji
waliomtangulia wenye historia kama ya kwake.
Bahati mbaya kwake Ngassa, tangu anaingia hadi anatoka Yanga
hakuwahi kutikisa nyavu za Simba, zaidi alitoa pasi kwa wafungaji na alikuwa
chachu ya ushindi katika mechi kadhaa.
Sasa Mrisho yupo Simba na mashabiki pamoja na kutaka kuona
kiwango chake siku hiyo, ambayo klabu hiyo itamkosa Mganda Emmanuel Okwi anayetumikia
adhabu, pia watataka kuona je, atawafunga Yanga?
Kufunga, kwanza ni nia ya mchezaji anayokuwa nayo hata kabla
hajaingia uwanjani na ndipo akiwa kazini atajituma kutafuta kutimiza nia yake
na hata akishindwa, jitihada huonekana, je Mrisho ana nia ya kuifunga Yanga?
Mrisho ana uwezo na ni kati ya wachezaji ambao kwa sasa
dhahiri wanawatia homa mabeki wa Yanga kuelekea mchezo huo- unaweza pia kusema
ni moja ya chachandu za mpambano huo ujao wa watani.
Kabla ya Ngassa, ni orodha ndefu ya wachezaji waliotoka Simba
kwenda Yanga na kutoka Yanga kwenda Simba, tangu enzi za akina Emanuel Mbele
'Dubu', lakini ni wachache waliong'ara kote kote.
Athumani Mambosasa (sasa marehemu), Zamoyoni Mogella, Method
Mogella (sasa marehemu), Hamisi Gaga (sasa marehemu), Deo Njohole, Akida
Makunda, Alphonce Modest, Monja Liseki, Shaaban Ramadhan, Eustace Bajwala,
Joseph Katuba (sasa marehemu) wote hao ni baadhi ya wachezaji waliotoka Simba
na kwenda kucheza Yanga.
Maulid Dilunga 'Mexico', Ezekiel Greyson 'Jujuman', Justin
Mtekere (wote marehemu), Ally Yussuf 'Tigana', Yussuf Macho, Godwin Aswile,
Ismail Suma, Steven Nemes, Nico Bambaga, Bakari Malima, Willy Martin, Edibily
Lunyamila, Mtwa Kihwelo, Omar Hussein 'Keegan', Athumani China, Mohamed Hussein
'Mmachinga', Mohamed Banka, Amri Kiemba wote pia ni baadhi ya wachezaji
waliotoka Yanga na kucheza Simba.
Athumani China akiwa Yanga, aliifunga Simba bao la mapema,
dakika ya tatu, Oktoba 9, mwaka 1991 kwenye Ligi ya Muungano, wakati watoto wa
Jangwani wakiibuka na ushindi wa 2-0. Bao la pili la Yanga lilifungwa na
Abubakar Salum 'Sure Boy' dakika ya 54.
China tena aliifunga Yanga akiwa Simba, lilikuwa bao la pili
katika ushindi wa 4-1 kwa Wekundu wa Msimbazi, Julai 2, mwaka 1994. Ally Yussuf
Suleiman 'Tigana', pia alifunga mabao kote kote, Thomas Kipese kadhalika naye
aliwafunga Simba na baadaye Yanga.
Akida Makunda aliihama Simba kuingia Yanga akiwa hana
kumbukumbu ya kufunga bao kwenye mechi ya watani, lakini mara baada ya kutua
kwa wana Jangwani aliingia kwenye orodha ya nyota waliofunga mabao kwenye mechi
baina ya wababe hao wa soka ya Tanzania.
Ilikuwa Februari 21, mwaka 1998 katika mchezo wa kwanza wa
Ligi Kuu Tanzania Bara, wakati huo ikidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania
(TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, wakati Makunda alipofunga bao
lililoelekea kuwatoa Yanga kifua mbele kwenye mchezo huo, dakika ya 46.
Lakini Athumani Macheppe alizima shangwe za wana Yanga zikiwa
zimesalia dakika mbili mchezo huo kumalizika kwa bao lake safi.
Sahau kuhusu Akida, kama yupo mchezaji ambaye aliyewapa raha
mashabiki wa timu zote hizo, basi ni Said Nassor Yussuf Mwamba, maarufu kama
Kizota enzi zake, aliyefariki dunia Februari 11, mwaka 2007. Kizota ni mchezaji
aliyewasisimua kwa namna yake mashabiki wa Yanga na Simba kutokana na mabao
yake.
Kizota alifariki dunia baada ya kugongwa na gari eneo la
Veterinary, akiwa anatoka kushuhudia mchezo wa marudiano, Kombe la Shirikisho
la Soka Afrika, Raundi ya Awali kati ya wenyeji Simba dhidi ya Textil de Pungue
ya Msumbiji. Alitoka kwa huzuni uwanjani siku hiyo baada ya kushuhudia timu
yake ya zamani, Simba ikitolewa na wageni kwa mikwaju ya penalti 3-1, kufuatia
sare ya jumla ya 2-2.
Mchezo wa kwanza Msumbiji, Simba ililazimisha sare ya 1-1 na
marudiano nayo pia walibanwa kwa sare aina hiyo hiyo, hivyo kufanya mshindi
aamuliwe kwa mikwaju ya penalti. Ntota ya timu ya kiwanda cha nguo Msumbiji
ndiyo iliyong'ara jioni hiyo.
Kama kuna miaka ambayo Kizota alifanya vitu vya 'babu kubwa'
kwenye soka ya Tanzania, basi ni 1993, kwani mapema tu mwaka huo aliibuka
mfungaji bora kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini
Kampala, Uganda, akiiwezesha Yanga pia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa
kuwafunga wenyeji, SC Villa.
Lakini pia, alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Tanzania. Yote
tisa, kumi ni pale Kizota alipofunga mabao mawili peke yake, wakati Yanga
inaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya
Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam.
Ilikuwa ni Machi 27, mwaka huo 1993, wakati Kizota
alipomchambua kipa hodari nchini enzi hizo, Mwameja Mohamed katika dakika za 47
na 57.
Simba ikielekea kulala 2-0, shukrani kwake Edward Chumila
(naye marehemu pia) aliyewafungia Wekundu wa Msimbazi bao la kufutia machozi,
dakika ya 75.
Baada ya kipigo kikali cha mabao 4-1, Julai 2, mwaka 1994,
Yanga ilivunja kikosi ikiwafukuza karibu nyota wake wote wa kikosi cha kwanza
kwa tuhuma za kuhusika kuihujumu timu katika kipigo hicho kilichotokana na
mabao ya George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani na Dua Saidi, bao la
kufutia machozi la Yanga likifungwa na beki imara, Constantine Kimanda.
Kati ya nyota waliotupiwa virago Yanga ni Kizota, ambaye
kutokana na makali yake wakati huo, akiwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania
na miongoni mwa nyota waliotoa mchango mkubwa kwenye kikosi kilichochukua Kombe
la Challenge nchini Kenya, Simba wakamwambia: "Usipate tabu Said, njoo
upumzike huku".
Kizota alitaka kuwaonyesha Yanga kwamba, walifanya kosa
kumwacha na katika mchezo wa marudiano baina ya watani hao wa jadi wa Ligi Kuu
ya Bara, Oktoba 4, 1995, Yanga ikiwa inaelekea kabisa kushinda mchezo huo 1-0,
Said Mwamba alitibua furaha ya wana Jangwani dakika ya 70 kwa kufunga bao safi
la kusawazisha.
Yanga ilitangulia kupata bao kupitia kwa mpachika mabao wake
mahiri enzi hizo, Mohamed Hussein 'Mmachinga' dakika ya 40. Bao la Kizota
liliwachanganya Yanga na dakika tisa baadaye, wakapachikwa bao la pili. Safari
hiyo alikuwa ni Mchunga Bakari 'Mandela' aliyewaambia wana Jangwani; kutangulia
si kufika.
Baada ya msimu huo, Yanga walikiri kosa lao na wakaenda
kumpigia magoti Kizota arejee nyumbani. Kwa sababu Kizota alikuwa anaishi
nyumba ya pili kutoka klabu ya Yanga, akiishi na mkewe Tosha, Mtaa wa Jangwani,
hivyo ilikuwa rahisi kumrubuni na kurejea nyumbani.
Na aliporejea Yanga, Kizota aliifunga tena Simba. Ilikuwa
Novemba 9, mwaka 1996, katika sare ya ajabu ya watani, ya mabao 4-4 mjini
Arusha.
Kizota aliifungia Yanga bao la kusawazisha lililofanya sare
ya 3-3 katika dakika 70, baada ya awali Kipese kuifungia Simba, dakika ya saba,
Edibily Lunyamila kuisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 28, Ahmed
Mwinyimkuu kuifungia Simba la pili dakika ya 43, kabla ya Dua Said kufunga la
tatu dakika ya 60 na Mustafa Hoza kuisawazishia Yanga kwa kujifunga dakika ya
64.
Sanifu Lazaro aliifungia Yanga bao lililoelekea kuwa la
ushindi dakika ya 75, lakini walishindwa kulinda lango lao na kuruhusu bao la
dakika za lala salama, lililofungwa na Duwa Said dakika ya 90, hivyo kuwa sare
ya 4-4.
Je, Mrisho ataweza kufanya vitu Oktoba 3? Bila shaka hilo ni
jambo la kusubiri na kuona.
0 comments:
Post a Comment