Hemed Morocco |
Na Mahmoud Zubeiry
HEMED
Morocco, kocha wa Mafunzo ya Zanzibar na timu ya taifa ya visiwani humo, Zanzibar Heroes yupo kwenye mazungumzo na uongozi wa
Coastal Union ya Tanga, ili awe kocha mpya wa timu hiyo kufuatia kubwagwa
manyanga kwa Juma Mgunda.
Habari kutoka
ndani ya Coastal, mabingwa wa Ligi Kuu 1988, zimesema kwamba mazungumzo
yanaendelea vizuri na watakapofikia makubaliano, watatangaza rasmi.
Mgunda, alijiuzulu
jana akisema ameamua kufanya hivyo mapema, kabla ya mambo hayajaribika, ili
mwalimu mpya anayekuja afanye kazi vizuri.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Mgunda alisema kwamba anaachia timu baada ya kucheza
mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akiwa ameshinda moja na kutoa
sare mbili.
“Kama
utaweza kuona naiacha timu ikiwa kwenye hali nzuri kuliko Yanga, ambao
wamefungwa mechi moja, sare moja na kushinda moja, naondoka kwa moyo mkunjufu,
sina kinyongo na mtu,”alisema.
Mgunda alisema
hiyo ndio hulka yake tangu anacheza Coastal Union, kuwa na moyo swafi na
ataendelea kuwa hivyo. “Mimi ni mpenzi wa Coastal Union, hakuna asiyejua, na
kwa manufaa ya timu, naondoka,”alisema.
Kumekuwa
kama kuna kampeni ya kumvuruga Mgunda kazini ambayo imekuwa ikiendeshwa kwenye
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa kumzomea kila timu inapocheza, hatimaye ameamua
kuwaachia timu.
Kwa sasa
Coastal, imebaki na kocha Msaidizi, Habib Kondo ambaye msimu uliopita alikuwa
kocha wa Villa Squad ya Kinondoni, iliyoshuka daraja na jioni hii anaiongoza
timu hiyo ya Barabara ya 13, katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar.
Mgunda
anakuwa kocha wa pili wa Ligi Kuu kuachia timu, baada ya Mbelgiiji, Tom
Sainftiet ambaye amefukuzwa Yanga, baada ya kutofautiana na uongozi, akiwa
ameiongoza timu kwenye mechi mbili tu za Ligi Kuu, akitoa sare moja na kufungwa
moja.
0 comments:
Post a Comment