Charles Kilinda |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA Mkuu wa JKT Ruvu, Charles Kilinda jana alikacha
kuzungumzia kipigo cha mabao 4-1 walichopewa na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara na kumuachia msaidizi wake, Azishi Kondo.
Tofauti na ilivyo ada yake, kiungo huyo wa zamani wa Yanga, Kilinda
ambaye huwa mwepesi kuzungumza wakati wowote, kabla na baada ya mechi, jana
hakuingia kabisa kwenye chumba cha mikutano.
Msaidizi wake, beki wa zamani wa timu hiyo, Kondo alizungumzia
kipigo hicho kama matokeo ya soka na zaidi akasema kilichangiwa na kukosekana
kwa wachezaji wake muhimu, waliokuwa majeruhi.
“Mabao manne ni mengi kwa kweli, imetokana na makosa, ndiyo mambo
ya mpira, tumefungwa kwa sababu za kisoka,”alisema mdogo huyo wa Kocha Msaidizi
wa Coastal Union, Habib Kondo.
Mdogo huyo wa beki wa zamani wa Simba SC, Adolph Kondo
alisema kwamba wachezaji kadhaa waliocheza mechi iliyopita ambayo walifungwa
mabao 2-0 na Simba, kama kipa namba moja, Shaaban Dihile, Amos Mgisa na George
Minja jana wote walikuwa majeruhi.
Kuhusu madai kwamba, JKT imeshuka kiwango kwa kusajili ‘wazee’
kama Credo Mwaipopo, Kondo alisema; “Si kweli kwamba Credo ni mkongwe, hapana,
Credo bado mdogo tu, sema alicheza Yanga, klabu kubwa, ni mchezaji mzuri,
alikuwa nje, karudi, tumemsajili na leo kacheza vizuri,”alisema.
Credo aliyecheza Yanga 2006 hadi 2008, akiwa anaibukia kisoka
nchini, baada ya hapo alikwenda Sweden kucheza soka ya kulipwa hadi aliporejea
msimu huu na kusaini timu hiyo ya jeshi.
JKT Ruvu jana ilipoteza mechi ya pili ya Ligi Kuu kati ya
tatu, ikifungwa 4-1 na kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hadi mapumziko Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0,
yaliyotiwa kimiani na Nahodha, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ dakika ya nne na
Didier Kavumbangu dakika ya 31, mabao yote yakitokana na kazi nzuri ya kiungo
mshambuliaji Simon Msuva.
Bao la kwanza ulikuwa mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna
Niyonzima, baada ya Msuva kuangushwa karibu kabisa na eneo la hatari la JKT
Ruvu na bao la pili dogo huyo aliyesajiliwa kutoka Moro United iliyoshuka
daraja, alimpa pasi mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kavumbangu.
Kipindi cha pili, Yanga walirudi tena kwa kasi na kufanikiwa
kupata bao la tatu dakika ya 52, mfungaji Simon Msuva kabla ya Didier
Kavumbangu kufunga la nne dakika ya 65.
JKT ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 68 mfungaji
Credo Mwaipopo.
Kikosi cha JKT jana kilikuwa; Said Mohamed, Kessy Mapande,
Stanley Nkomola, Damas Makwaya, Charles Timoth, Ally Khan, Haroun Adolf, Said
Ahmed ‘Ortega’/Jimmy Shoji, Omar Changa/Furaha Tembo, Hussein Bunu na Sosstenes
Manyasi/Credo Mwaipopo.
0 comments:
Post a Comment