// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); KAMISAA WA SIMBA AUMIA, TFF YAMUENGUA LIGI KUU KWA KUWASILISHA RIPOTI YA POTOFU YA MCHEZO - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE KAMISAA WA SIMBA AUMIA, TFF YAMUENGUA LIGI KUU KWA KUWASILISHA RIPOTI YA POTOFU YA MCHEZO - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, September 26, 2012

    KAMISAA WA SIMBA AUMIA, TFF YAMUENGUA LIGI KUU KWA KUWASILISHA RIPOTI YA POTOFU YA MCHEZO

    Manahodha wa Ruvu Shooting, Benjamin Haule kulia na wa Simba, Juma Kaseja wakisalimiana mbele ya marefa wa mechi hiyo.

    Na Mahmoud Zubeiry
    KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 25 mwaka huu) kupitia ripoti za mechi 21 za Ligi Kuu ya Vodacom ambazo zimeshachezwa mpaka sasa, na kumuondoa George Komba aliyekuwa Kamisaa kwenye mechi namba 20 kati ya Simba na Ruvu Shooting, upungufu uliojitokeza katika ripoti yake.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, klabu ambazo zimeandikwa barua za onyo ni African Lyon kwa kwenda uwanjani na jezi tofauti na zile ilizoonesha kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (pre match meeting), Mtibwa Sugar kwa kuchelewa kuwasilisha leseni za wachezaji wake wakati wa mechi na Ruvu Shooting kwa ushangiliaji uliopita kiasi kwenye mechi yao dhidi ya Simba.
    Amesema Kamati pia imethibitisha kadi nyekundu ya Emmanuel Okwi kwa kumpiga kiwiko Kessy Mapande wa JKT Ruvu, hivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 25(1) anakosa mechi tatu na kulipa faini ya sh. 500,000. Mchezaji huyo atakosa mechi namba 20, 27 na 80.
    Amesema kwa upande wa waamuzi, Ronald Swai ameandikiwa barua ya onyo kutokana na upungufu alioonesha kwenye mechi kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Amesema wamiliki wa viwanja vya Mkwakwani, Tanga na Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya wameandikiwa barua ya kuvifanyia marekebisho viwanja vyao katika maeneo mbalimbali yenye upungufu ikiwemo uzio wa kutenganisha wachezaji na washabiki.
    Aidha, Wambura amesema beki Faustine Lukoo wa Polisi Moro ambaye kwa mujibu wa ripoti ya mwamuzi aliyemtoa nje kwa kadi nyekundu alimtukana mchezaji mwenzake kwenye mechi dhidi ya African Lyon na Katibu wa Oljoro JKT aliyemwaga maji kwenye chumba cha timu ya Polisi Moro, masuala yao ni ya kinidhamu, hivyo yamepelekwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi kwa ajili ya hatua zaidi.
    Amesema klabu ambazo timu zao mpaka sasa zinacheza mechi bila kuwa na logo ya mdhamini, suala hilo limepelekwa kwa wadhamini Vodacom kwa vile wenyewe ndiyo wanaogawa vifaa hivyo.
    Wakati huo huo: Rais wa TFF, Leodegar Tenga atakutana na waandishi wa habari kesho mchana, kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.
    Katika hatua nyingine, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyokutana jana kusikiliza rufaa ya Mussa H. Mahundi, Abou O. Sillia na Alex Mgongolwa dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Soka Iringa (IRFA), iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa IRFA uliofanyika Septemba 8 mwaka huu Mufindi, Iringa, na kuomba uchaguzi huo ufanyike upya kwa kuendeshwa na kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, imetupilia mbali rufaa hiyo.
    Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratias Lyatto, baada ya kupitia maelezo ya warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejiridhisha kuwa rufani iliyowasilishwa mbele yake na Mahundi, Sillia na Mgongolwa ilikosa sifa ya kuwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya 8(2), Ibara ya 21(3) na 24(2). Kwa kutozingatia matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imetupa rufani hiyo.
    Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya IRFA kuchukua hatua dhidi ya Abuu Changawa kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya 28(6) kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi wa IRFA siku ya uchaguzi.
    TFF pia, imewashukuru wadau waliofanikisha kwa njia mbalimbali ziara ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys iliyofanyika hivi karibuni katika mikoa ya Mbeya na Njombe.
    Wadau hao ni Chama cha Soka Mbeya Mjini (MUFA) chini ya Mwenyekiti wake Suleiman Haroub, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA), Stanley Lugenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Njombe (NDFA).
    Wengine ni Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Makambako (MDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), na klabu za Mbozi United, Kyela United, Tanzania Prisons na Mbeya City.
    Serengeti Boys inaendelea na kambi yake jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya mchujo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi ya Misri itakayochezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMISAA WA SIMBA AUMIA, TFF YAMUENGUA LIGI KUU KWA KUWASILISHA RIPOTI YA POTOFU YA MCHEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top