Raoul Shungu |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA ipo
kwenye mazungumzo na makocha watatu, wawili kutoka Brazil akiwemo kocha wa
zamani wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Marcio Maximo na
mwingine jina lake halikuweza kupatikana- pamoja na Raoul Shungu wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili mmoja wao aje kufundisha timu hiyo.
Habari
kutoka ndani ya Yanga zimesema kwamba, mazungumzo na Maximo yanaendelea ingawa
bado kuna ugumu, lakini wakati huo klabu hiyo inazungumza na kocha mwingine
Mbrazil.
Pamoja na
Wabrazil hao, Yanga jana ilianza mawasiliano na kocha wake wa zamani, Shungu,
arejee kufundisha timu hiyo.
Mkakati wa
Yanga ni kocha mpya awasili nchini kabla ya Oktoba 3, watakapomenyana na
wapinzani wao wa jadi, Simba SC na kulingana na hali halisi, Shungu ni mwalimu
anayepewa nafasi zaidi kuja kufanya kazi tena Jangwani.
Katika
kipindi cha miaka mitatu ya kufanya kazi kwake Yanga, kutoka 1998 hadi 2000,
Shungu aliipa Yanga Kombe la Afrika Mashariki na Kati, mwaka 1999 katika
fainali zilizofanyika Kampala, Uganda na mataji kadhaa ya nyumbani, likiwemo
Kombe la FA, Nyerere, Muungano na ubingwa wa Bara.
Aliondoka
Yanga baada ya kutofautiana na Mwenyekiti wa klabu hiyo wakati huo, Tarimba
Abbas baada ya kusema amekwenda Ufaransa kusoma kozi fupi ya FIFA, lakini
aliporudi akaambiwa aonyeshe pasipoti yake kama viza ya nchini humo, akawa
anapiga chenga, hivyo akaonekana muongo.
Kilichofuatia,
aliyekuwa kocha wa African Sports ya Tanga wakati huo, Charles Boniface Mkwasa
akaajiriwa kama Meneja wa timu na baada ya muda mfupi, Shungu akaondolewa na
kiungo huyo wa zamani wa Yanga, akapewa Ukocha Mkuu.
Maximo ni
kocha ambaye, wana Yanga wanampenda sana na ilikuwa aje kufundisha timu hiyo
badala ya Mbelgiji aliyetupiwa virago, Tom Saintfiet lakini inadaiwa
‘alilishiwa sumu na wazandiki’, ila kwa sasa wana Jangwani wanajaribu tena
bahati yao.
Yanga ipo
katika mchakato wa kusaka kocha mpya, baada ya kumtimua Saintfiet aliyedumu kwa
siku 80 tu, ambaye sasa nafasi yake anakaimu Msaidizi wake, Freddy Felix
Minziro hadi hapo atakapopatikana kocha
mwingine.
Makamu
Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga amesema asubuhi hii katika Mkutano na
Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na
Jangwani kwamba, matokeo mabaya na kutotii matakwa ya uongozi, ndio vimemfanya
Saintfiet asitishiwe mkataba.
Aidha, Sanga
alikanusha madai kwamba eti kocha huyo amefukuzwa baada ya kutofautiana na
Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji.
“Timu
ilipokwenda Mbeya, ikatoka sare na Prisons akalalamikia huduma, lakini sisi
taarifa tulizozipata, yeye aliwaruhusu wachezaji kwenda kulewa disko baada ya
mechi. Kuna mapungufu mengine mengi, ambayo hatuwezi kusema hadharani.
Kwa mfano
timu ilipotoka Mbeya, tulitaka iende moja kwa moja Morogoro, yeye akalazimisha
timu irudi Dar es Salaam, tena iende tena Morogoro. Wachezaji wakachoka sana na
hii tunaamini ilichangia hata kufungwa na Mtibwa.
Timu
iliporudi kutoka Morogoro, tukaamua iingie kambini, yeye akapinga akisema timu
kubwa kama Barcelona Ulaya, hazikai kambini, yaani anataka atupangie kazi sisi,
tukaona huyu mtu haendani na maadili ya uongozi na hatufai, tukaamua kusitisha
mkataba wake,” alisemsa Sanga.
Saintfiet
ameiongoza Yanga katika mechi 14 tu ndani ya siku 80 tangu ajiunge nayo Julai
mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic na katika mechi
hizo amefungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na Atletico ya Burundi 2-0.
Katika mechi
hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico
ya Burundi.
0 comments:
Post a Comment