Boban |
Na Mahmoud Zubeiry
HATIMAYE
kiungo tegemeo wa Simba SC, Haruna Moshi Shaaban, ameungana na wenzake jioni
hii kambini visiwani Zanzibar kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya wapinzani wao
wa jadi, Yangas SC, Jumatano.
Boban
hakucheza mechi iliyopita ya Ligi Kuu kati ya Simba na Prisons kwa sababu
alikuwa anasumbuliwa na homa ya matumbo na hakwenda kambini wenzake, kwa kuwa
alikuwa anajisikilizia afya yake.
Simba SC
inaendelea vizuri na maandalizi yake ya pambano dhidi ya watani wao wa jadi,
Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislam,
Kwerekwe, visiwani Zanzibar na kambi yao ipo Chukwani.
Morali ya
kambi ipo juu na wachezaji wote wako fiti, wakijifua kwa shauku kubwa ili
kumvutia kocha Mserbia, Milovan Cirkovick awape nafasi ya kucheza Oktoba 3,
kuanzia sa 1:00 usiku.
Simba inatarajiwa
kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuanzia saa 2:00 leo kumenyana
na All Stars ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki, kujiandaa na mpambano dhidi
ya watani wao wa jadi, Yanga..
Simba imerejea
leo Zanzibar, baada ya jana kuendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, kwa kuichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea Ligi Kuu msimu
huu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya
Simba yalitiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho Ngassa, ambaye hilo ni
bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ndani ya mechi nne na la pili jumla tangu
ajiunge na timu hiyo katika mechi saba alizocheza, wakati la Prisons lilifungwa
na Elias Maguri.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 12 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi Azam
FC pointi mbili katika nafasi ya pili, ingawa timu zote zimecheza mechi sawa,
nne.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zikwishafungana bao 1-1, Prisons wakitangulia
kupata bao dakika ya sita baada ya Maguri kuwatoka mabeki wa Simba kupiga shuti
lililomgonga Shomary Kapombe na mpira kupoteza mwelekeo na kumchanganya kipa na
Nahodha wa Simba, Juma Kaseja na kutinga nyavuni.
Baada ya bao
hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa Prisons waliendelea
kuwa wagumu, hadi walipojisahau kidogo sekunde za mwishoni za kipindi cha
kwanza na Felix Sunzu akatumia pasi ya Amiri Maftah kusawazisha dakika ya 45.
Kipindi cha
pili, Simba walirudi na moto na kuanza moja kwa moja kulishambulia mfululizo
lango la Prisons na dakika ya 55 Ngassa akafunga kwa shuti dhaifu, ambalo kipa wa
Prisons, David Abdallah alidaka lakini mpira ukamtoka na kuingia nyavuni.
Mechi hiyo
ilichezeshwa na refa, Paul Soleji kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Jesse Erasmo,
mshika kibendera namba moja, Mwarabu Mumba mshika kibendera namba mbili, wote
kutoka Morogoro, wakati refa wa Akiba alikuwa Israel Nkongo wa Dar es Salaam.
Dakika ya 87
Amir Maftah alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Khalid Fupi wa Prisons,
hivyo ataukosa mchezo ujao dhidi ya Yanga Jumatano na hiyo ni nafasi kwa
chipukizi Paul Ngalema.
Hiyo inakuwa
kadi ya pili nyekundu kwa Simba ndani ya mechi nne, awali katika mechi ya pili
dhidi ya JKT Ruvu, Emmanuel Okwi alilimwa kadi ya aina hiyo kwa kumpiga kiwiko
Kessy Mapande na akafungiwa mechi tatu.
Kikosi cha
Simba jana kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomari
Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/Salim Kinje, Ramadhan Chombo/Jonas
Mkude, Christopher Edward/Daniel Akuffo, Felix Sunzu na mrisho Ngassa.
Prisons: 18.David Abdallah, 03.Aziz Sibo, 05.Laurian
Mpalile, 16.Lugano Mwangama (Nahodha), 15.David Mwantika, 13.Khalid Fupi, 07.Misango
Magai, 12.Fred Chudu/22.Julius Kwaga, 14.Elias Maguri, 17.Peter Michael/Sino
Augustino na 19.John Matei/11.Hamisi Ally.
0 comments:
Post a Comment