Hans Poppe |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI
wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba hadi
sasa klabu yake haijapata barua ya hukumu ya pingamizi zao dhidi ya wachezaji
Mbuyu Twite na Kevin Yondan kuidhinishwa kuchezea Yanga kutoka Kamati ya
Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza na
BIN
ZUBEIRY leo, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
amesema kwamba kutokana na kutopatiwa hati hiyo ya hukumu, wanashindwa kukata rufaa,
Mahakama ya Usuluhishi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), CAS.
“Tumekwishawaandikia
barua ya kuwaomba hati ya hukumu, lakini bado hadi leo hawajatupa, sasa
tunashindwa kuelewa nini lengo lao, tunafikiria wanajua tukikata rufaa CAS tutashinda,
sasa wamejawa hofu na wanaogopa kutoa hukumu kwa maandishi,” alisema Hans
Poppe.
Septemba 10,
mwaka huu Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, chini ya Mwenyekiti wake,
Alex Mgongolwa ilitoa maamuzi ambayo hayakuwaridhisha walalamikaji, Simba SC
juu ya Twite na Yondan na sasa wanataka kulipeleka suala hilo CAS.
Kamati hiyo,
iliitaka Simba kuthibitisha madai yake ya kuingia mkataba na Yondan na
kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati hiyo.
“Kwa mujibu
wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu
zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
Kwa vile
Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa
kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe
malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au
mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika,”alisema
Mgongolwa.
Kuhusu suala
la Mbuyu Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni
za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu
zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali.
Hata hivyo, alisema
kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na
kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku
21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Wajumbe sita
kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa.
Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na
Omari Gumbo.
Siku 21
walizopewa Yanga kurudisha fedha za Twite alizochukua Simba, zinamalizika
Oktoba 3, mwaka huu siku ambayo watani hao wa jadi katika soka ya Tanzania,
watamenyana katika mchezo wa Ligi Kuu, mzunguko wa kwanza.
0 comments:
Post a Comment