Dk Kigoda |
Na Mashaka Mhando,Tanga
MBUNGE wa Handeni, Dk. Abdallah Kigoda, amewataka wadau wa michezo waliopo ndani na nje ya wilaya hiyo, kujitokeza kusaidia kufanikisha azma ya wilaya ya Uwanja wa Azimio uliopo mjini Chanika, kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu msimu huu.
Akizungumza jana, Dk. Kigoda alisema ili Uwanja huo uweze kutumika katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom nchini kwa ajili ya timu Mgambo JKT iliyopanda daraja msimu huu kutokea wilayani hapa, zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni 150.
Dk. Kigoda ambaye ni Waziri wa Viwanda na Biashara, alisema ametoa kiasi cha shilingi milioni 20 kwa ajili ya kuanza ujenzi na ukarabati wa uwanja huo awamu ya kwanza ambapo tayari wameanza kutengeneza sehemu ya kuchezea (Pitch) kwa kuweka udongo maalumu na kisha kuotesha nyasi zitakazoweza kuhimili mikimiki ya mchezo wa mpira wa miguu.
Alisema bada ya kumaliza kuiweka sawa sehemu hiyo ya kuchezea hatua ya pili itakayofuata ni kupandisha kwa juu kuta za uwanja huo, vyumba vya wachezaji na waamuzi vya kubadilishia nguo, kuweka mageti ya milango na kujenga jukwaa katika upande mmoja wa wageni wa heshima na baadaye kukamilisha sehemu nyingine za majukwaa ili watazamaji watakaofika wapate kukaa.
“Lengo letu raundi ya pili ya Ligi Kuu ichezewe Handeni…Hii ni historia ya pekee kwa wilaya yetu ya Handeni kuwa na timu ya Ligi Kuu hivyo tunao wajibu wa kushikamana watu wote kuhakikisha lengo letu hili linatimia tunawaomba wafadhili, makampuni na watu wengine watusaidie kwani tunahitaji kiasi cha shilingi milioni 150,” alisema.
Dk. Kigoda alisema pindi uwanja huo utakapokamilika utakuwa uwanja wa pili kwa ukubwa mkoani Tanga baada ya ule wa Mkwakwani ambao timu hiyo ya Handeni utautumia kwa michezo yake ya Ligi Kuu ambapo Septemba 15 itakapoanza Ligi hiyo itacheza na Coastal Union kwenye uwanja huo.
Timu ya JKT Mgambo ambayo inamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa JKT kikosi kilichopo Mgambo eneo la Kabuku, imepanda daraja msimu huu pamoja na timu za Polisi Morogoro na Prison ya Mbeya ni timu ambayo wakazi wa wilaya hii wamekuwa na faraja kubwa kupata timu ambayo itashiriki Ligi hiyo kwa mara ya kwanza.
0 comments:
Post a Comment