Brandts kulia akisaini mkataba na Yanga. Kushoto ni Sanga akisaini kwa upande wa Yanga |
YANGA SC, jana imeingia mkataba wa mwaka mmoja na
kocha Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, wiki moja tangu imfukuze
Mbelgiji, Tom Saintfiet aliyeitumikia klabu hiyo kwa siku 80 tu.
Na Mahmoud Zubeiry |
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo jana,
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba wamepata kocha mzoefu
wa soka ya Afrika ambaye amefanya kazi APR ya Rwanda.
“Tulikuwa na makocha wengi katika mchakato, tumekuwa
makini kutokana na matatizo yaliyojitokeza awali, tumekuwa makini na aina ya
mikataba tunayoingia na makocha, ili tusije tukarudia makosa, tumezungumza naye
matatizo yaliyotokea na kocha aliyemtangulia, ameridhika, ameona tuko sahihi,
naye amesema yuko tayari kutimiza masharti ya mwajiri wake mpya,”alisema Sanga.
Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na
klabu ya PSV Eindhoven ya Holanzi, aliwasili juzi majira ya saa 3:45 usiku
katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na ndege ya KLM
na kupokewa na Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako na viongozi wengine,
Abdallah Ahmad Bin Kleb, Seif Ahmad ‘Magari’ na Majjid Suleiman.
Yanga, imetimiza malengo yake ya kuwa kocha mpya,
kabla ya kucheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada
ya kumfukuza Mbelgiji, Tom Saintfiet, kutokana na kuwasili kwa Brandts, ambaye
ataanza kazi mara moja leo.
Kikosi cha Yanga kipo kambini, hoteli ya Uplands,
Changanyikeni, Dar es Salaam na kabla ya kucheza na Simba Jumatano, kesho
kitacheza na African Lyon, Uwanja wa Taifa pia.
Baada ya kusaini mkataba, kocha huyo alisema kwamba
atajitahidi kadiri ya uwezo wake, kuhakikisha anaiongoza timu hiyo kushinda
mechi ya Jumatano dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC ingawa anajua utakuwa
mtihani mgumu.
Alisema kwanza anaushukuru uongozi wa klabu hiyo
kuwa kumuamini, na anaafiki kwa kiasi kikubwa kupewa nafasi ya kurithi mikoba
ya Mbelgiji, Tom Saintfiet, aliyetupiwa virago wiki iliyopita, baada ya
kuitumikia Yanga kwa siku 80.
“Muhimu kwangu, nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu
kuipa matokeo mazuri klabu kwa asilimia mia moja. Nilikuwa Uholanzi, nikapigiwa
simu na Mwenyekiti, Yussuf Manji, akaniambia anataka nije kufanya kazi Yanga,
nilikuwa nina ofa nyingi, ila nilivutiwa naye (Manji), aliponiambia falsafa na
sera za klabu, anataka kuindeleza klabu.
Kitu kingine ni kuhusu timu, kama kocha, kweli
tuntaka kushinda kila mechi, lakini tunataka kucheza soka ya kuvutia. Jambo
muhimu kwangu ni kufanya kila mchezaji mmoja mmoja acheze vizuri, na timu
icheze vizuri, kwa sababu hakuna bora zaidi ya timu,”alisema.
Brandts pia alizungumzia nidhamu, akisema;
“Kuzingatia nidhamu, ni muhimu si hapa tu Afrika, hata Asia na Ulaya kwa
sababu, ukitaka kuamka saa moja kamili amka saa moja kamili na ukitaka kujenga
timu nzuri, muhimu kujituma, hata mimi nilipokuwa nacheza ilikuwa hivyo pia, ni
muhimu kujivunia timu unayochezea na kila mchezaji anatakiwa kujivunia kuchezea
Yanga,”alisema.
Kuhusu kazi, alisema; “Kitu kingine, kuna mechi
kesho na kuna mechi Jumatano, dhidi ya Simba itakuwa ngumu sana, tutafanya kila
tunachoweza kuhakikisha tunashinda, naijua Yanga nimekuja hapa miaka miwili, ni
timu nzuri. Sasa nakwenda kujaribu kuboresha timu, najiona mwenye bahati
kusaini mkataba na timu hii,”alisema.
Brandts alikuja mwaka jana na mwaka huu kwa ajili ya
michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, akiwa na APR ya Rwanda na
mara zote, Yanga iliibuka bingwa, mwaka jana ikifundishwa na Mganda Sam Timbe
na mwaka huu ikifundishwa na Mbelgiji, Saintfiet.
Mwaka jana, APR ilitolewa mapema katika kundi lake
Morogoro, lakini mwaka huu ilifika hadi Nusu Fainali na kutolewa na Yanga.
Mholanzi huyo aliyeifundisha APR ya Rwanda tangu
2010, hakuongezewa mkataba baada ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame, Agosti mwaka huu amepewa ukocha wa Yanga, baada ya Mbrazil
Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Mtaalamu huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956
mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV Eindhoven, alichezea pia Roda JC
Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya
Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia
mwaka 1978.
Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na
Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote
katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia
Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye
aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa
2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo
mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa
uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa
Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla
ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, ambako ‘riziki’
yake imeisha miezi miwili iliyopita na sasa amepata maisha mapya Yanga.
Akiwa APR, Brandts alifungwa mechi zote mbili na
Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mbelgiji Tom Saintfiet katika Kombe la Kagame,
moja ya makundi 2-0 na nyingine ya Nusu Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa,
ikiifunga Azam FC 2-0 kwenye fainali.
Brandts atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili
Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo
Haruna Niyonzima anayeingia katika msimu wa pili, ambao alifanya nao kazi APR.
Brandts anakuwa kocha wa 19 kuifundisha Yanga, tangu
mwaka 1991, na katika kipindi chote hicho ni makocha watatu tu, waliorudishwa
kazini, baada ya kuondoka, ambao ni Syllersaid Mziray (sasa marehemu), Mmalawi
Jack Chamangwana na Mserbia Kostadin Papic.
Baadhi ya makocha waliamua kuondoka wenyewe, lakini
wengi wao walifukuzwa na tawala mbalimbali zilizopita katika klabu hiyo katika
kipindi chote hicho.
Kwa nini nimeanzia 1991, ndicho kipindi ambacho
vurugu vurugu za kufukuza makocha zilipoanza katika klabu hiyo, tofauti na
miaka ya nyuma tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1939.
Mapema mwaka 1991, Yanga ilimchukua kocha maarufu
zamani nchini, Syllersaid Salmin Kahema Mziray, ambaye aliondoka kwa watani wa
jadi, Simba SC, baada ya kushushwa cheo kutoka Simba A hadi Simba B.
Mziray aliiongoza Yanga kwa miaka miwili, akiwa
anasaidiwa na Charles Boniface Mkwasa na akaiwezesha kutwaa ubingwa wa Bara na
Muungano mfululizo, sambamba na kuwafikisha Fainali ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, ambako walifungwa kwa matuta na watani wa jadi, Simba SC.
Lakini baada ya hapo, marehemu Mziray aliondoka
Yanga kutokana na kupata ofa nzuri kutoka Pan African, wakati huo ikiwa
inafadhiliwa na Murtaza Dewji, ambaye alikuwa anaipigania irejee Ligi Kuu.
Yanga iliajiri tena kocha wa kigeni baada ya muda
mrefu, ikimleta Mrundi, Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ 1993 (sasa marehemu) ambaye
aliendelea kufanya kazi na Mkwasa na katika mwaka wake wa kwanza, akaiwezesha
timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame mjini Kampala, Uganda.
Tauzany aliporejea katika Ligi Kuu akaendelea vizuri
na kazi, lakini haikuchukua muda akaingia kwenye mgogoro na mfadhili wa klabu
hiyo wakati huo, Abbas Gulalamli (sasa marehemu).
Tauzany alitumia vyombo vya habari kupambana na
Gulamali na ilifikia hadi akawa anachafua jina lake kwa kusema anafanya
biashara haramu. Ilikuwa vita kali na mbaya zaidi hata Mrundi hiyo alikuwa
anakubalika mbele ya wanachama, hivyo kumfukuza ikawa tabu.
Alichokifanya Gulamali, akamrejesha kocha ambaye
alifanya kazi na kupendwa mno Yanga, Tambwe Leya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC), ambaye awali alifanya kazi mwaka 1975 na 1976, akiiwezesha
Yanga kuifunga Simba katika mechi ya kihistoria Nyamagana kabla ya kuipa Kombe
la kwanza la Kagame 1975, kwa kuwafunga hao hao Simba 2-0 Uwanja wa Amaan,
Zanzibar.
Tambwe alitua nchini mwishoni mwa mwaka 1994 na
jukumu lake alilopewa ni Ukurugenzi wa Ufundi, ambapo yeye akaamua kutengeneza
timu nzuri ya vijana, iliyopewa jina Black Stars.
Tauzany na kikosi cha Yanga chenye mastaa kibao
nchini wakati huo, akafungwa mabao 4-1 na Simba SC na hapo ndipo timu nzima na
kocha wao wakafukuzwa, wakabaki wachezaji saba tu ambao waliunganishwa na yosso
wa Tambwe kutengeneza kikosi kipya, kilichofanya vizuri hadi kufika Robo
Fainali ya Kombe la Washindi 1996.
Tambwe naye akaondolewa kwa visa na badala yake
akaajiriwa kocha mzalendo, Sunday Burton Kayuni 1997 ambaye naye pia hakudumu,
kwani alikfukuzwa na akaajiriwa kocha wa muda kutoka Uingereza, Steve McLennan
mwaka huo huo 1997.
McLennan, kocha Mzungu wa kwanza mimi kufanya naye
kazi Yanga, aliondolewa naye na nafasi yake akakaimu kwa muda aliyekuwa Msaidizi
wake, Juma Pondamali ‘Mensah’.
Siwezi kusahau siku alipofukuzwa McLennan, alimfuata
msaidizi wake ambaye aliachiwa timu na kumuuliza; “Juma nani ni kocha mzuri,
mimi au wewe?” Pondamali akawa anacheka tu, wapo kwenye basi timu inatoka
Zanzibar kwenye mechi za Ligi ya Muungano.
Yanga ikaajiri kocha wa muda, ambaye alikuwa
hajulikani kabisa, Tito Oswald Mwaluvanda (sasa marehemu) ambaye katika
kujikosha kwa wanachama, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo wakati huo, Rashid
Ngozoma Matunda (sasa marehemu pia) akawa anamtambulisha kama Msimamizi wa
mazoezi, wakati timu inatafuta kocha. Msimamizi wa mazoezi alichukua ubingwa wa
Ligi Kuu na Ligi ya Muungano 1998, tena akiweka rekodi ya ushindi mnono zaidi
katika Ligi ya Bara, mabao 8-0 waliyoifunga Kagera Shooting Stars (sasa Kagera
Sugar), tena ikiwa inafundishwa na kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati
huo, Zacharia Kinanda ‘Arrigo Sachi’ (sasa marehemu), Edibilly Jonas Lunyamila
akifunga mabao matano peke yake. Mungu amrehemu Kinanda, lakini siku hiyo
Lunyamila alimfikishia ujumbe, kwani kocha huyo alikuwa hamtaki Eddy katika
timu ya taifa- hivyo zile bao tano alizofunga ilikuwa ujumbe tosha, kwamba
alikuwa anakosea.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Mwaluvanda aliifikisha
Yanga hadi hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, akiweka rekodi mbili kuifanya
hiyo iwe klabu ya kwanza Tanzania kucheza hatua hiyo, yeye kuwa kocha wa kwanza
mzalendo na wa mwisho hadi sasa kuifikisha timu katika hatua hiyo.
Lakini pamoja na yote, mwaka 1998 mara tu baada ya
Yanga kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, marehemu Mwaluvanda
aliyekuwa anasaidiwa na Freddy Felix Isaya Kataraiya Minziro ‘Majeshi’
wakaondolewa wote na akaajiriwa kocha kutoka DRC, Raoul Jean Pierre Shungu
aliyeingia na msaidizi wake, Abeid Mziba ‘Tekero’.
Hii ilimuuma sana Mwaluvanda, kwa sababu ili kuingia
hatua ya makundi ilibidi azitoe Rayon ya Rwanda iliyokuwa inafundishwa na
Shungu na baadaye Coffee ya Ethiopia, lakini marehemu akawa anasema afadhali
angeletwa kocha mwingine, si yule ambaye ameitoa timu yake kwenye mashindano.
Wakubwa wakishaamua huwezi kupingana nao.
Shungu aliipa Yanga Kombe la tatu la Kagame, katika
michuano iliyofanyika mjini Kampala, Uganda 1999, lakini mwaka 2000 akaondolewa
na akaajiriwa Charles Boniface Mkwasa ‘Master’, ambaye naye mwishoni mwa mwaka
2001, akatupiwa virago pia.
Tangu 2002 hadi sasa ni miaka 10 tu, lakini katika
kipindi hicho Yanga imefundishwa na makocha 11, tena wengine wakifukuzwa na
kurudishwa kwenye kipindi hicho.
Alipoondolewa Master Mkwasa, akaajiriwa Mmalawi Jack
Lloyd Chamangwana ambaye mwaka 2003, alifukuzwa na mwaka 2004 akaajiriwa kocha
kutoka DRC, Jean Polycarpe Bonghanya ambaye naye hakudumu, mwaka huo huo
akaondolewa na kurudishwa Syllersaid Mziray. Marehemu Mziray alikuwa anasoma
ishara za nyakati tu, naye alipoona upepo unaelekea kuwa mbaya akamuachia timu
aliyekuwa Msaidizi wake, Kenny Mwaisabula.
Mwaisabula akaendelea na kazi hadi msimu wa 2005,
lakini baadaye mwaka huo akaondolewa na kurejeshwa Chamangwana., ambaye
alifanya kazi hadi 2007 alipompsha Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’.
Micho aliondoka kwa sababu ambazo hadi leo bado
hazieleweki, kwani alikubalika na timu ilikuwa inafanya vizuri. Alipoondoka
Micho, timu akabakia nayo, aliyekuwa kocha wa makipa, Mkenya Razack Ssiwa.
Ssiwa akaiongoza Yanga kutwaa Kombe la Tusker mwaka
2007 mjini Mwanza, lakini aliporudi kwenye ligi, timu inafanya vibaya, naya
akatupiwa virago na kurejeshwa Chamangwana.
Chamangwana naye akaondolewa na kuajiriwa tena
Mserbia, Profesa Dusan Savo Kondic, aliyekuja na Wasaidizi wawili, Spaso
Sokolovoski na Civojnov Serdan. Kondic naye mwaka 2010 akafukuzwa na kuajiriwa
Mserbia mwenzake, Kostadin Papic, ambaye naye alifukuzwa na kuajiriwa Mganda
Sam Timbe.
Timbe pamoja na kuipa timu Kombe la nne la Kagame
mwaka jana, alifukuzwa miezi miwili baadaye na kurejeshwa Papic, ambaye pia
hata kabla msimu uliopita wa Ligi Kuu haujamalizika, akatupiwa virago na
kuajirwa Mbelgiji, Saintfiet.
Saintfiet amehitimisha historia yake Yanga ndani ya
siku 80, akicheza mechi 14, akishinda 12, sare moja na kufungwa mbili- huku akiacha Kombe la tano la Kagame
Yanga na sasa anakuja Mholanzi Brandts kufungua ukurasa mpya. Kweli makocha
wanaamini, wanaajiriwa ili wafukuzwe, lakini bado huu si msemo wa kuuftaisha
sana, kwani soka soka ni mchezo wa kitalaamu, ambao unahitaji wataalamu kupewa
muda wa kufanya kazi.
Sanga amesema wamemueleza Brandts matatizo yao na
kocha aliyepita, naye amewaona wako sahihi na ameahidi kutekeleza matakwa ya
mwajiri wake. Hii nzuri sana. Hiki ni kipimo kingine kwa Yanga juu ya mahusiano
yake na makocha.
MAKOCHA YANGA TANGU
1991
1. 1991:
Syllersaid Mziray(marehemu)
2. 1993:
Nzoyisaba Tauzany (marehemu) (Burundi)
3. 1995:
Tambwe Leya (marehemu) (DRC)
4. 1997:
Sunday Kayuni
5. 1997:
Steve McLennan (Uinegereza)
6. 1998:
Tito Mwaluvanda(marehemu)
7. 1999:
Raoul Shungu (DRC)
8. 2001:
Charles Boniface Mkwasa
9. 2002:
Jack Chamangwana (Malawi)
10. 2004:
Jean Polycarpe Bonganya (DRC)
11. 2004:
Syllersaid Mziray (marehemu)
12. 2005:
Kenny Mwaisabula
13. 2006:
Jack Chamangwana (Malawi)
14. 2007:
Milutin Sredojevic ‘Micho’ (Serbia)
15. 2007:
Razack Ssiwa (Kenya)
16. 2007:
Jack Chamangwana (Malawi)
17. 2008:
Dusan Kondic (Serbia)
18. 2010:
Kostadin Papic (Serbia)
19. 2011:
Sam Timbe (Uganda)
20. 2011:
Kostadin Papic (Serbia)
21.
2012: Tom Saintfiet (Ubelgiji)
22.
2012: Ernie Brandts (Uholanzi)
0 comments:
Post a Comment