Mtaalamu Boban |
Na Mahmoud Zubeiry
LABDA leo,
lakini jana wamemsubiri hadi boti ya mwisho hakushuka. Haruna Moshi Shaaban, mchezaji
pekee ambaye hayupo kambini Simba SC, alitarajiwa kuungana na wenzake jana,
visiwani Zanzibar kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya wapinzani wao wa jadi,
Yangas SC, lakini wapi.
Sasa uongozi
wa Simba utamsikilizia mchezaji huyo leo kama atatimiza wajibu wake na tofauti
na hapo, watachukua.
Boban hakucheza
mechi iliyopita ya Ligi Kuu kati ya Simba na Ruvu Shooting, kwa sababu alikuwa
anaumwa na hakwenda kambini wenzake, kwa kuwa alikuwa anajisikilizia afya yake,
ila kuanzia jana alitarajiwa kuungana na wenzake kambini.
Kuna uwezekano
mkubwa Boban akapanda boti na wenzake na baada ya mechi ya kesho, dhidi ya
Prisons.
Japo Boban
hayupo kambini Zanzibar, lakini Simba SC inaendelea vizuri na maandalizi yake
ya pambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, ikifanya
mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislam, Kwerekwe, visiwani Zanzibar na kambi
yao ipo Chukwani.
Morali ya
kambi ipo juu na wachezaji wote wako fiti, wakijifua kwa shauku kubwa ili
kumvutia kocha Mserbia, Milovan Cirkovick awape nafasi ya kucheza Oktoba 3,
kuanzia sa 1:00 usiku.
Simba
itarejea Dar es Salaam kesho kucheza mechi na Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa,
kisha kurejea tena visiwani humo kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Jumamosi
ijayo.
Hata hivyo,
katika michezo miwili ijayo, Simba itamkosa mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel
Okwi ambaye amefungiwa na Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, chini ya
Mwenyekiti wake, Wallace Karia, sambamba na kumtoza faini ya Sh. 500,000 kwa
kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa JKT Ruvu, Kessy Mapande.
Okwi
alifanya hivyo akilipa kisasi cha kuchezewa rafu Jumatano iliyopita, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Tayari Okwi
amekosa mechi moja dhidi ya Ruvu Shooting na wakati, na sasa atakosa mechi
mbili zaidi, dhidi ya Prisons na dhidi ya Yanga na baada ya hapo atakuwa huru
kuendelea kumtumikia mwajiri wake.
Siyo siri,
kuelekea pambano la watani wa jadi, Okwi alikuwa ni homa kwa Yanga, hasa
wakikumbuka namna alivyowanyanyasa katika mechi iliyopita, akifunga mabao
mawili kwenye ushindi wa 5-0 na kusababisha mawili.
0 comments:
Post a Comment