Na
Mahmoud Zubeiry
HALI
ya afya ya msanii mkongwe nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu kama Bi Kidude inaendelea
vizuri katika hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam alipolazwa na wakati
wowote kuanzia kesho anaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani, ila familia imemstaafisha
rasmi sanaa.
BIN
ZUBEIRY
alifika katika wadi namba 202 hospitali ya Hindu Mandal, jioni hii kumjulia
hali Bi Kidude, mwimbaji maarufu na mkongwe haswa wa muziki wa Taarabu duniani
na ‘alhamdulillah’, Bi Mkubwa anaendelea vizuri.
Watu
wanapishana kuingia na kutoka kumsalimia Bi Kidude, wengine wakitoka nje ya
nchi, baadhi mashabiki wake na baadhi ndugu na jamaa.
Kulia kwangu ni Bi Hidaya, anayemuuguza Bi Kidude hospitalini, tukizungumza huku tukipiga soga na mgonjwa pia ambaye yuko mbele yetu jioni ya leo, Hindu Mandal. |
Lakini
jambo moja tu Bi Kidude analaani vikali ni taarifa za kuzushiwa kufariki dunia
mwishoni mwa wiki. “Watu wamenizushia kufa Zubeiry, na wewe hukuja kuniona,
ulifikiri nimekufa? Mi mzima, si unaniona, cheki,”alisema Bi Kidude na kuuvuta
mkono wa BIN ZUBEIRY kwa nguvu akiuminya ‘kibaunsa’ kuonyesha nguvu za
misuli yake, kwamba yeye yuko mzima.
Bi
Kidude alikuwa mcheshi wakati anazungumza na watu mbalimbali waliomtembelea
hospitali na alimuambia BIN ZUBEIRY kwamba anasumbuliwa na
maradhi ya sukari, ambayo ni maradhi yake kwa muda mrefu, ila yalimzidia kwa
kukiuka taratibu za vyakula.
“Kweli
nilikuwa naumwa, ngozi yote ilivuka hii, nilikonda sana, ila sasa Alhamdulillah
mi mzima, mi mzima, naweza kuondoka,”alisema.
Mwonekano
wa Bi Kidude ni mtu mwenye afya njema japokuwa amelala kitandani wadi namba 202,
Hindu Mandal na sasa anainuka kwenda mwenyewe msalani.
Amezuiwa
kuvuta sigara tangu alazwe hospitalini hapo na inaonekana kwa hamu ya sigara anaomba
aondoke hata sasa hivi. Amewekewa waangalizi wawili, wa kike na wa kiume, wote
wakiwa ni wanafamilia.
Hidaya
Abdi Omar, mkwe wa Kidude ambaye ni mmoja wa waangalizi wake hospitalini hapo
amesema kesho Bi Mkubwa huyo atafanyiwa vipimo ambayo kama vitakuwa namna
ambavyo madaktari wa hospitali hiyo wanataka, ataruhusiwa.
Hidaya
ni mke wa mtoto wa mdogo wake wa kiume Bi Kidude, aitwaye, Abdallah Baraka
ambaye hivi sasa ni marehemu. “Bi Kidude hakubahatika kuzaa, lakini ndugu zake
wamezaa, mimi ni mke wa mtoto wa kaka yake Bi Kidude, na kwa sasa ndiye naishi na
huyu bibie kulingana utu uzima na hali yake pia,”anasema Hidaya.
Hidaya
anasema msimamo wa familia umekwishapita kwamba Bi Mkubwa huyo sasa
hataruhusiwa kufanya kazi yoyote ya sanaa, atakuwa wa kupumzika tu acheze na
wajukuu.
“Hatapanda
tena jukwaani popote, sasa basi tena, akae tu apumzike, familia imekwishaamua,”alisema.
Familia hiyo hiyo imeamua Bi Kidude asipigwe picha yoyote akiwa wadini.
Ndugu
zake wote watatu ambao ni wadogo zake Bi Kidude wamekwishafariki dunia na kwa
sasa Bi Kidude anakula matunda ya watoto wa ndugu zake hao, ambao kwa sasa ndio
wanamlea.
Hakuna
promota yeyote wa tamasha au kiongozi wa serikali, au chombo chochote cha sanaa
aliyekwenda kumjulia hali Bi Kidude wadini, zaidi baadhi ya wasanii wanapiga
simu tu na kwa hilo wala Bi Mkubwa huyo hajali, watu wanaokwenda kumuona na kumfariji
kwake wanatosha.
Bi
Kidude alianza kusumbuliwa na maradhi mwezi uliopita, lakini baadaye akapata
ahueni na kufanya mahojiano hadi na vyombo vya habari, lakini ghafla mambo yakabadilika
tena na amerudi hospitali, ila kwa sasa unaposoma habari hii yuko vizuri Hindu
Mandal.
Bi
Kidude ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya muziki wa
mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko
wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana
katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Fatuma
binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar
katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni
mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi
Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni
kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni
kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu
wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi
miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Bi
Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na
alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti Binti
Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar
kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi
yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko
wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti
alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa
makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa
mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa
na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia
Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa
kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso
aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni
katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na
uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar
ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi
Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya 'wanja'
na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa
dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na
ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna
aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu
wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja
na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo
mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona
hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni,
hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi
anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na
miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na
kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi
Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa,
Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha
pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za
Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX
ilienda kwake.
Nyimbo
alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na
Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Quraan.
0 comments:
Post a Comment