Azam FC |
Na
Princess Asia
AZAM FC leo inashuka kwenye Uwanja wake wa Chamazi,
kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na
mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC, Septemba 11, mwaka huu.
Coastal jana ilifungwa mechi ya nne kati ya tano za
kujipima nguvu ilizocheza na leo itataka kurejesha matumaini ya mashabiki wake
ambao wamekwishaanza kukata tamaa, kiasi cha kutokuwa na imani na benchi la
ufundi la timu yao.
Ilifungwa 3-2 na Bandari mjini Mombassa, baadaye 2-0
Tanga, ilifungwa 2-1 na Polisi mjini Morogoro na kabla ya kufungwa na Yanga
jana 2-1, iliifunga JKT Oljoro 1-0.
Azam imetoka kushinda mechi mbili mfululizo za
kujipima nguvu, ya mwisho ikiifunga 1-0 Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja huo huo wa
Chamazi, bao pekee la kiungo Ibrahim Mwaipopo dakika ya 34, baada ya kupunguza
mabeki wawili wa Prisons na kutumbukiza mpira nyavuni.
Mchezo uliotangulia, Azam iliichapa mabao 8-0
Transit Camp Uwanja huo huo wa Chamazi, John Bocco ‘Adebayor’ akifunga mabao
mawili sawa na Papie, mshambujliaji mpya aliye kwenye majaribio kutoka Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kipre Herman Tcheche na Abdulhalim Humud.
Azam inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao
ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo
wake wa kwanza katika historia ya Ngao hiyo.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya
Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa
soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba
kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001,
Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi
ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare
ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa
kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na
Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na
Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na
beki mahiri Shomari Kapombe, aliyemajeruhi kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment