Yanga SC |
Na
Mahmoud Zubeiry
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame, Yanga SC ya Dar es Salaam, wameanza vyema ziara yao ya mechi za
kujipima nguvu nchini Rwanda, baada ya jioni hii kuichapa Rayon Sport mabao 2-0 kwenye
Uwanja wa Amahoro mjini Kigali.
Yanga ambao jana walitembelea Ikulu ya Rwanda,
walipoalikwa na rais Paul Kagame kupeleka Kombe la Afrika Mashariki na Kati,
ambalo tangu mwaka 2002 mfadhili wake mkuu na mlezi wake ni Rais Kagame, mabao
yake yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza dakika ya pili na Simon Msuva dakika 12.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally
Mustafa ‘Barthez’, Nsajigwa Shadrack/Stefano Mwasyika, Oscar Joshua/Mbuyu Twite,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’/Frank Damayo, Simon
Msuva, Haruna Niyonzima/Omega Seme, Didier Kavumbangu, Hamisi Kiiza/Jerry Tegete
na Nizar Khalfan/Shamte Ally.Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah
Ahmad Bin Kleb ameiambia BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Kigali
kwamba, timu yao ilicheza vema na kuwazidi kabisa uwezo wenyeji wao.
Alisema Yanga ilikuwa ina uwezo wa kufunga mabao
zaidi, kama washambuliaji wake wangetumia vema nafasi zote walizotengeneza.
Bin Kleb alisema kwamba Yanga itashuka tena dimbani
kumenyana na Polisi Jumapili na kwa mujibu wa ratiba ya awali, wanatakiwa
kurejea Dar es Salaam Jumatatu.
Awali, Yanga ilikuwa icheze pia na mabingwa wengine
wa zamani wa Kombe la Kagame, APR, lakini kutokana na timu hiyo kukabiliwa na
mgogoro hivi sasa uliosababisha kufukuzwa kwa kocha Mholanzi, Ernest Brandy na
nafasi yake kupewa kocha mzalendo kwa muda, imeshindwa kucheza.
Katika ziara hiyo, Yanga haijaambatana na mfungaji
bora wa Kombe la Kagame, Said Bahanuzi ambaye amebaki Dar es Salaam kwa
matatizo ya kifamilia. Yanga imekwenda Rwanda na msafara wa watu 42, wakiwemo
wachezaji 28, Maofisa watano wa benchi la Ufundi na viongozi wanane.
Viongozi walio na timu Kigali ni Mwenyekiti, Yussuf
Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Mama
Fatma Karume, Francis Kifukwe na Seif Ahmed ‘Magari’ sambamba na Wajumbe wa
Kamati ya Utendaji, Abdallah Bin-Kleb na Salum Rupia.
Benchi la ufundi ni kocha mkuu; Tom Saintfiet, Kocha
Msaidizi Fred Felix Minziro, Kocha wa makipa, Mfaume Athumani, Meneja Hafidh
Saleh, Daktari, Sufiani Juma na Mtunza vifaa Mahmoud Omary ‘Mpogolo’, wakati
wachezaji ni makipa: Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed. Mabeki
Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika,
David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Ibrahim Job, Ladisalus
Mbogo; viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Simon
Msuva, Shamte Ally, Omega Seme, Idrisa Rashid, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima,
Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nurdin Bakari na washambuliaji; Hamis Kiiza ‘Diego’,
Jerry Tegete na Didier Kavumbangu.
Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili
mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga
Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na
Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo,
Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba
katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye
ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka
1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara
‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo,
Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said
Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa,
Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120,
Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia
kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za
Waganda.
Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo,
Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya
makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa
raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa
Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa
Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu
wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
Msuva katika mechi ya leo |
Kiiza katika mechi ya leo. PICHA ZOTE NA SALEH ALLY, MHARIRI KIONGOZI GAZETI LA CHAMPIONI |
0 comments:
Post a Comment