Na
Mahmoud Zubeiry
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame, Yanga SC ya Dar es Salaam wametua Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere,
Dar es Salaam mida hii, wakitokea Rwanda walipokuwa kwa wiki moja kwa ziara ya mechi
mbili za kirafiki, ya mwisho jana wakishinda mabao 2-1 dhidi ya Polisi kwenye
Uwanja wa Amahoro.
Hata hivyo, Yanga imetua bila beki wake mpya, Mbuyu Twite
iliyemsajili kutoka St Eloi Lupopo, ingawa alikuwa anachezea APR na Katibu Mkuu
wa Yanga, Celestine Mwesigwa amesema kuna mambo anakamilisha na atatua Dar es
Salaam ndani ya saa 48 kuanzia leo.
“Na tuna imani Jumamosi katika mechi yetu na Coastal
Union Uwanja wa Taifa atakuwepo kutambulishwa rasmi,”alisema Mwesigwa.
Kuhusu mpango wa Simba SC, kumfungulia kesi Polisi
na kumvizia akitua tu nchini imkamate kwa kuwatapeli dola za Kimarekani 30,000,
Mwesigwa alisema; “Simba sio Polisi, na Yanga ni klabu ambayo inafanya mambo
yake kwa utaratibu, kwa hivyo hatuna wasiwasi na hilo,”alisema.
Kabla ya kusaini Yanga, inadaiwa Twite alisaini Simba
na kupewa dola za Kimarekani 30,000 lakini baadaye akarudisha fedha hizo
kupitia viongozi wa APR na Lupopo, ingawa Simba walikataa kuzipokea.
Lakini tayari Simba SC wamesajili beki mwingine
kutoka Kenya, Paschal Ochieng kama mbadala wa beki huyo wa kimataifa wa Rwanda-
na sasa inachodai ni fedha zake.
Yanga ilimaliza ziara yake jana nchini Rwanda kwa
ushindi wa mabao 2-1, wafungaji Stefano Mwasyika aliyesawazishia, baada ya
Fabrice kutangulia kuifungia Polisi na Nahodha Msaidizi, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ akafunga la pili.
Katika mchezo wa awali Ijumaa, Yanga waliwachapa mabingwa
wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati, Rayon Sport mabao 2-0 kwenye Uwanja huo
huo wa Amahoro mjini Kigali.
Yanga ambao siku moja kabla ya mechi hiyo ya kwanza,
walitembelea Ikulu ya Rwanda, walipoalikwa na rais Paul Kagame kupeleka Kombe
la Afrika Mashariki na Kati, ambalo tangu mwaka 2002 mfadhili wake mkuu na
mlezi wake ni Rais Kagame, siku hiyo mabao yake yalitiwa kimiani na Hamisi
Kiiza dakika ya pili na Simon Msuva dakika 12.
Awali, Yanga ilikuwa icheze pia na mabingwa wengine
wa zamani wa Kombe la Kagame, APR, lakini kutokana na timu hiyo kukabiliwa na
mgogoro hivi sasa uliosababisha kufukuzwa kwa kocha Mholanzi, Ernest Brandy na
nafasi yake kupewa kocha mzalendo kwa muda, imeshindwa kucheza.
Yanga itaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa
sekondari ya Loyola kujiandaa na Ligi Kuu ya Bara, inayotarajiwa kuanza
Septemba 15 na Jumamosi itacheza na mabingwa wa Ligi Kuu 1988, Coastal Union.
Yanga ilikwenda Rwanda na msafara wa watu 42,
wakiwemo wachezaji 28, Maofisa watano wa benchi la Ufundi na viongozi wanane.
Viongozi walio na timu Kigali ni Mwenyekiti, Yussuf
Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Mama
Fatma Karume, Francis Kifukwe na Seif Ahmed ‘Magari’ sambamba na Wajumbe wa
Kamati ya Utendaji, Abdallah Bin-Kleb na Salum Rupia.
Benchi la ufundi ni kocha mkuu; Tom Saintfiet, Kocha
Msaidizi Fred Felix Minziro, Kocha wa makipa, Mfaume Athumani, Meneja Hafidh
Saleh, Daktari, Sufiani Juma na Mtunza vifaa Mahmoud Omary ‘Mpogolo’, wakati
wachezaji ni makipa: Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed. Mabeki
Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika,
David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Ibrahim Job, Ladisalus
Mbogo; viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Simon
Msuva, Shamte Ally, Omega Seme, Idrisa Rashid, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima,
Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nurdin Bakari na washambuliaji; Hamis Kiiza
‘Diego’, Jerry Tegete na Didier Kavumbangu.
Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili
mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga
Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na
Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo,
Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba
katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye
ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka
1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara
‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo,
Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said
Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa,
Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120,
Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia
kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za
Waganda.
Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo,
Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya
makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa
raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa
Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa
Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu
wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
0 comments:
Post a Comment