Yanga wakisherehekea ubingwa wa Kagame |
Na
Prince Akbar
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga ya
Dar es Salaam wanatarajiwa kuanza tena mazoezi kesho saa 3:00 asubuhi kujiandaa
na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi
huu.
Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mbelgiji Tom Saintefiet
ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba baada ya mapumziko ya siku tano tangu watwae
Kombe la Kagame, kesho waanza tena kujiandaa na Ligi Kuu.
Tom amesistiza wachezaji wote wanatakiwa kuripoti mazoezini
Uwanja wa Kaunda, uliopo makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga
na Jangwani.
Yanga ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati,
Jumamosi kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
wafungaji Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hilo lilikuwa taji la tano la michuano hiyo kwa
Yanga kihistoria, baada ya awali kutwaa mataji ya Kombe hilo katika miaka ya
1975 Zanzibar, 1993, 1999 Uganda na 2011 Dar es Salaam na mara zote hizo, ikiwa
chini ya makocha wa kigeni.
Mwaka 1975 Yanga ilibeba Kombe hilo, ikiwa chini ya
kocha kutoka Jamhuri ya Kodemokrasia ya Kongo (DRC), Tambwe Leya (sasa marehemu),
1993 chini ya kocha kutoka Burundi, Nzoyisaba Tauzany pia marehemu, 1999 chini
ya Raoul Shungu kutoka DRC na mwaka jana chini ya Mganda Sam Timbe.
Mapema jana ziliibuka habari kwamba, baada ya kuipa Yanga
Kombe la Kagame,Tom ameomba kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Kenya, Harambee
Stars, lakini mwenyewe alisema baadaye akizungumza na BIN ZUBEIRY kwamba tangu
amejiunga na klabu hiyo mwezi uliopita hajawahi kuomba kazi sehemu nyingine
yoyote.
Mtakatifu Tom alisema anashangazwa mno na habari
hizo za kizushi, za kizandiki zenye kulenga kumchonganisha yeye na mwajiri
wake, Yanga SC.
“Nakumbuka niliwahi kuomba kazi Chama cha Soka Kenya
(KFF) kufundisha timu yao ya taifa (Harambee Strars), lakini ilikuwa ni muda
mrefu sana hata kabla sijaomba kazi Yanga,”alisema.
Blog moja iliyowahi kuandika Iddi Kipingu anagombea
Uenyekiti Yanga, jana iliandika habari yenye kichwa kisemacho; “WIKI MOJA BAADA
YA KUIPA UBINGWA: KOCHA WA YANGA TOM SAINTFIET ATUMA MAOMBI YA KUIFUNDISHA
HARAMBEE STARS,”.
Akiizungumzia habari hiyo, Mtakatifu alisema; “Ni
uongo, tangu nimesaini mkataba na Yanga, sijawahi kuomba kazi pengine
popote,”alisema.
0 comments:
Post a Comment