Yanga SC |
Na
Mahmoud Zubeiry
YANGA ya Dar es Salaam leo inashuka kwenye Uwanja wa
nyumbani, Taifa kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa kirafiki
kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iliyopangwa kuanza Septemba 15,
mwaka huu.
Beki Kevin Yondan amepona na leo anaweza kuanza na
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika safu ya ulinzi, lakini viungo Nizar Khalfan, Rashid
Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’ na Athumani Iddi ‘Chuji’ bado ni wagonjwa tangu timu
ilipokuwa Rwanda wiki iliyopita.
Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet, raia wa Ubelgiji
aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, wakati viungo hao wataikosa mechi ya
leo, wachezaji wengine watatu, beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima na
mshambuliaji Didier Kavumbangu hawana asilimia 100 ya kucheza mechi ya leo.
Huo utakuwa mchezo wa 11 kwa Yanga chini ya Mtakatifu
Tom na katika mechi zote alipoteza moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye
michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambayo
waliibuka mabingwa. Mechi za Kagame, Yanga ilifungwa moja na katika mechi za
kirafiki haikufungwa hata moja.
Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili
mfululizo Julai mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC
mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said
Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo,
Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba
katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye
ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka
1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara
‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo,
Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said
Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa,
Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120,
Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia
kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za
Waganda.
Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo,
Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya
makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa
raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa
Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa
Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu
wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
Kwa upande wa Coastal, huo utakuwa mchezo wa tano wa
kujipima nguvu awali ikishinda mechi moja na kufungwa tatu. Tayari umetokea mgawanyiko
baina ya viongozi wa Coastal kuhusu benchi la ufundi la klabu hiyo,
linaloongozwa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda, akisaidiwa na Habib Kondo, Kocha wa
mazoezi ya viungo, Ally Jangalu na Kocha wa makipa, Bakari Shime.
Baadhi
ya viongozi wa Coastal wanaunga mkono, lakini wengine wanapingana na wazo hilo,
wakidai bado ni mapema sana na hasa ikizingatiwa timu ipo kwenye mechi za
kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hali
ilikuwa mbaya zaidi Jumatano wiki hii, baada ya Coastal kufungwa mabao 2-0 na
Bandari ya Mombassa, Kenya katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa
Mkwakwani mjini Tanga.
Baada
ya mchezo huo, mashabiki wa Coastal waliwatia kashikashi makocha Juma Mgunda na
Msaidizi wake Habib Kondo wakidai hawafai na kutaka waondolewe, hali ambayo
ilifanya waondolewe uwanjani kwa msaada wa Polisi.
Hali
hiyo ilijitokeza kwa mara ya pili, baada ya Jumatatu pia wiki hii timu hiyo
ikicheza na JKT Oljoro ya Arusha pamoja na kushinda bao 1-0, mashabiki
walilalamikia kiwango kibovu na kuzomea makocha.
REKODI
YA SAINTFIET YANGA
1.
Yanga Vs JKT Ruvu 2-0
2.
Yanga Vs Atletico (Burundi) 0-2
3.
Yanga Vs Waw Salam (Sudan Kusini) 7-1
4.
Yanga Vs APR (Rwanda) 2-0
5.
Yanga Vs Mafunzo (Z’bar) 1-1 (5-3penalti)
6.
Yanga Vs APR (Rwanda) 1-0
7.
Yanga Vs Azam 2-0
8.
Yanga Vs African Lyon 4-0
9.
Yanga Vs Rayon (Rwanda) 2-0
10. Yanga Vs Polisi (Rwanda) 2-1
0 comments:
Post a Comment