MICHUANO ya soka ya Kombe la taifa imeshindwa kufanyika
mwaka huu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limedhihirisha haitafanyika
tena.
Na Mahmoud Zubeiry |
Sababu ni kwamba imekosa mdhamini- baada ya mdhamini wake wa
awali, Kampuni Bia Tanzania (TBL)
iliyokuwa ikidhamini michuano hiyo kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager
kuachia michuano hiyo.
Wazi, TBL wamejitoa Taifa Cup baada ya kupata dili la
kujitangaza kupitia timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo awali
ilikuwa inadhaminiwa na kampuni nyingine ya Bia nchini, Serengeti (SBL).
Mkataba wa udhamini wa Taifa Stars na SBL ulimalizika
Desemba mwaka jana na TFF ikashindwa kukubaliana dau la mkataba mpya na SBL, na
kuingia mkataba mpya naTBL. TFF waliuita mkataba huo ni mnono sana. Kweli
kabisa, kwa sababu TBL walipanda dau, kutoka lile walilokuwa wakitoa SBL.
SBL walianza kuidhamini Stars mwaka 2006, ikiwa haina na
haijawahi kuwa na mdhamini. Katika kipindi hicho, SBL ilitekeleza vema mkataba
wake wa udhamini na timu hiyo na kuonekana dhahiri kuvuka mipaka katika
kuhakikisha timu inakuwa na maandalizi mazuri na kujenga hamasa ya mashabiki
kurejesha mapenzi kwa timu yao ya taifa.
Kwa kiasi kikubwa, Tanzania walibaki mashabiki wawili tu wa
soka, mmoja wa Simba na mwingine wa Yanga, lakini timu ya taifa haikuwa
ikipendwa kabisa.
Mechi za timu ya taifa zilikuwa hazivutii mashabiki kabisa
na hakuna kingine kilichosababisha hali hiyo zaidi ya kushuka kwa kiwango cha
timu yenyewe na uongozi mbovu uliokosa dira ya maendeleo kwa soka ya nchi hii.
Wengi wanaamini hata SBL walijitokeza kuisaidia timu ya
taifa, ili kuunga mkono jitihada za rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alianza kwa kutimiza ahadi yake ya kuipatia timu
hiyo kocha wa kigeni, kwa kumleta Mbrazil Marcio Maximo.
Ndiyo, kwa sababu wakati huo timu hiyo ilikuwa haiuziki kwa
yoyote na hata TBL hawakuwa wakiitaka wakati huo.
SBL imefanya mambo mengi yenye kuonekana wakati wake
ikiidhamini Stars tangu 2006 hadi mwaka jana Desemba mkataba ulipoisha.
Iligharamia kambi za muda mrefu kuanzia nyumbani na ugenini,
ili kuhakikisha timu yetu inajengwa vema na kuwa ya ushindani.
Huwezi kusahau kambi za mafunzo Bulyanhulu mkoani Shinyanga,
baadaye Brazil na nchi za Scandinavia.
Chini ya Maximo kwa udhamini wa SBL tulishuhudia timu yetu
imekuwa ya ushindani tena na kukaribia kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika
mwaka 2008 nchini Ghana kama si kufungwa na Msumbiji katika mechi ya mwisho
nyumbani.
Hadhi ya timu ya taifa ilipanda na tulishuhudia timu kubwa
kama Brazil na Ivory Coast zikipokea mwaliko wa kuja kucheza nasi mechi za
kirafiki hapa.
Matunda ya udhamini wa SBL ni timu yetu kufuzu kucheza
Fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory
Coast mwaka 2009 na kwa mara ya kwanza Watanzania waliwashuhudia wachezaji wao
kwenye luninga wakicheza michuano mikubwa ya Afrika.
Kweli, baadaye timu yetu iliporomoka na zaidi ilitokana na
matatizo ya ndani ya shirikisho, nidhamu za wachezaji na ‘ujuaji’ wetu
Waandishi na wachambuzi uchwara wa Tanzania uliotugharimu tukampoteza kocha
mzuri, Marcio Maximo.
Lakini hata katika wakati mgumu, wakati wa kuporomoka kwa
timu ya taifa, bado SBL iliendelea kuwa bega kwa bega na timu ya taifa- hata
baada ya Maximo kuondoka na hatimaye mwaka juzi timu ya Bara ikatwaa Kombe la
Challenge baada ya miaka 15.
Tanzania Bara, ambayo huundwa na asilimia 90 ya wachezaji wa
Taifa Stars inayoundwa kwa mseto wa wachezaji wa Bara na visiwani Zanzibar,
ambayo kwenye Challenge hushiriki kama nchi kamili, ilitwaa Kombe hilo mara ya
mwisho mwaka 1994 nchini Kenya.
Kombe la Challenge lilirejea Bara chini ya kocha aliyerithi
mikoba ya Maximo, Mdenmark Jan Borge Poulsen, ambaye naye tayari ameondolewa na
nafasi yake kachukua Mdenmark mwenzake, Kim Poulsen.
SBL wamekuwa wavumilivu na kuendelea kuidhamini Stars bila
ya kujali matokeo mabaya, ambayo yalisababisha mashabiki waanze kuizomea timu
yao.
Wakati wa mchakato wa kuitoa Taifa Stars SBL kuihamishia TBL
niliandika nikitoa angalizo kwa TFF, nikiwaambia wanapaswa kuzingatia kwamba,
TBL tayari ni wadhamini wakuu wa Kombe la Taifa, ni wadhamini wakuu wa klabu za
Simba na Yanga.
Kuwapa na timu ya taifa pia, maana yake sasa wao ndio
watakaokuwa wamebeba mustakabali mzima wa soka ya nchi hii, jambo ambalo kwa
mtazamo wangu niliona ni hatari.
TBL kama kampuni, ambayo ina maamuzi yake binafsi ambayo nje
ya misingi ya sheria- hayawezi kuwa na upinzani wala kipingamizi chochote, nilisema,
inaingia mkataba wa kuidhamini timu ya taifa, ikiwa tayari inadhamini Kombe la
Taifa na klabu za Simba na Yanga kwa sababu viongozi wa sasa wa kampuni hiyo
wanaridhia hilo.
Lakini ni hatari ikitokea akaletwa kiongozi mwingine pale
TBL kutoka Afrika Kusini- ambaye atakuwa hana mapenzi na soka. Anaweza kuamua
mara moja, mikataba inayoendelea ikifikia tamati na iwe basi na hakuna
anayeweza kupingana nao.
Lakini soka ya Tanzania itaingia kwenye wakati mgumu sana-
kumpoteza mtu ambaye alikuwa nguzo muhimu kama mdhamini wa klabu za Simba na
Yanga, Kombe la Taifa na timu ya taifa kwa wakati mmoja.
Na nilisema wazi, historia ndio inaleta wasiwasi huu. Mwaka
2001, Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilikuwa inadhaminiwa na TBL, lakini katika
hatua za mwishoni mwa ligi hiyo, kampuni hiyo ilijitoa kwa sababu ambayo sisiti
kusema ndogo tu.
Aliyekuwa Waziri wa Michezo wakati huo, Profesa Juma
Athumani Kapuya kwa utashi wake aliongeza timu mbili katika hatua ya mwisho na
kuwa nane badala ya sita, ambazo wakati huo FAT ilikubaliana na TBL.
TBL ilikerwa na hilo na ikasitisha udhamini wake mara moja
na mwaka huo, ingawa timu ziliitangaza bia ya Safari Lager kwa robo tatu ya
msimu, lakini hazikupata chochote, pole zaidi kwa mabingwa wa mwaka huo, Simba
SC ambao walikosa zawadi.
Wakubwa walisema tu, TBL ya sasa iko chini ya Wazungu na
hawataki mambo yetu ya Kiswahili, hivyo kwa uswahili wa Kapuya kuongeza timu
katika hatua ya mwisho ya ligi hiyo wao wakajitoa na ligi ikabaki yatima.
Nilisema; ipo haja ya kutafakari, uswahili alioufanya Kapuya
wakati huo, kama angeufanya katika kipindi ambacho TBL ingekuwa mdhamini wa
Ligi Kuu, Kombe la Taifa na timu ya taifa, soka ya nchi hii ingekumbwa na janga
kubwa kiasi gani?
Nilisema, kweli TBL wametoa dau kubwa kuliko SBL, lakini ipo
haja ya TFF kutafakari mara mbili faida na athari za kuikabidhi soka yetu yote
kwa TBL.
Sikutaka kuzungumzia malumbano ya mara ya mara na klabu za
Simba na Yanga juu ya utekelezaji wa mikataba yao ya udhamini, ikiwemo kelele
za kucheleweshewa mishahara au kutopewa mabasi mapya makubwa waliyoahidiwa
tangu wasaini mikataba mipya mwaka jana- ila niliwaasa TFF, wawe makini na
maamuzi yao.
Sasa hata mwaka haujapita tangu nimetoa angalizo hilo, leo
TBL wamelitema Kombe la Taifa na hadi unaposomoa makala hii, haijakabidhi
mabasi mapya makubwa waliyoahidi kutoa kwa Simba na Yanga.
Leo TBL wamejitoa Taifa Cup, kipi kitamzuia mtu yeyote kutilia
shaka mustakabali wa udhamini wao katika klabu za Simba na Yanga, ikiwa huko
nyuma waliitema Ligi Kuu?
Kupitia Ligi Kuu, bia za TBL zilikuwa zinatangazwa kwenye
jezi za klabu zote nchini zikiwemo Simba na Yanga na walijitoa sasa washindwe
vipi kutoa matangazo yao kwenye jezi za klabu hizo mbili tu?
TFF walishindwa kusoma ishara za nyakati wakaingia kichwa
kichwa kwa TBL na kuwapa mkataba wa
kudhamini timu ya taifa, hawakujua nini kitatokea mbele. TBL ipo kibiashara
zaidi na daima wataendelea kuangalia maslahi yao zaidi juu ya kile wanachotoa,
kama kitaendana na wanachopata- sijui TFF wanafikiria nini.
Wakati nawasilisha mada hii, najipanga kwa ajili ya
kuwasilisha mada kuhusu udhaifu wa TFF kuwashauri wadhamini juu ya namna ya
kuwekeza fedha zao kwenye soka kwa manufaa ya soka yetu na wao pia wanufaike
kibiashara.
Hilo litakuwa Jumapili kunako majaaliwa ‘inshaallah’. Kwa
sasa, tuendelee tu kuhuzunika kwa kupoteza Kombe la Taifa, huku tukiomba Mungu
alete kheri zake ajitokeza mdhamini mwingine wa kuibeba michuano hiyo ya
kihistoria Tanzania, tangu enzi za mababu ikiitwa Gossage. Wasalam.
0 comments:
Post a Comment