Stewart kushoto, akizungumza na wachezaji wake katika moja ya mechi za Kagame |
UKIKUTANA na mfanyakazi wa Azam wa muda mrefu, ukamuomba
akusimulie historia ya timu ya Azam, utagundua kitu kimoja, halikuwa wazo la
mmoja kati ya wamiliki halali wa sasa, kuwa na timu hiyo.
Na Mahmoud Zubeiry |
Ni hivi; Azam FC ilianzishwa na kikundi cha wafanyakazi wa
kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu
yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, lengo la wafanyakazi hao wa kampuni
inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya
kujiburudisha, baada ya kazi.
Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka
2004, wafanyakazi hao waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la
Nne, wakitumia jina la Mzizima FC.
Ilikuwa wanapokwenda kucheza mechi, wanapitisha michango
kiwandani kwa wafanyakazi na mabosi, wanakwenda kucheza.
Baada ya Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya S.S. Bakhresa,
Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni
zote za Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam
Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika.
Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo
timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11,
mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC.
Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi
mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King,
aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa
zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na
Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa makipa.
Baadaye ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin kutoka
Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo katika timu
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Ilisajili pia wachezaji nyota, wazoefu, wakiwamo kutoka nje
ya Tanzania, ambao walichanganywa na chipukizi wachache walioipandisha timu
hiyo, kama John Bocco ‘Adebayor’.
Baadaye Itamar alipewa Ukocha Mkuu, baada ya Santos kutupiwa
virago, lakini Itamar naye aliondolewa mwaka jana na nafasi yake akapewa
Muingereza Stewart Hall, ambaye amefanikiwa kuipa taji la kwanza Azam, Kombe la
Mapinduzi Januari mwaka huu na Aprili akaiwezesha kushika nafasi ya pili katika
Ligi Kuu, ikiwapiku vigogo, Yanga.
Azam ambayo kwa kuwa washindi wa pili wa Ligi Kuu watacheza
Kombe la Shirikisho mwakani, mwezi uliopita walicheza fainali za michuano
miwili, na yote wakafungwa na kuambulia nafasi ya pili, nyuma ya vigogo wa soka
Tanzania, Simba na Yanga.
Kwanza ilikuwa fainali ya Kombe la Urafiki walipofungwa na
Simba kwa penalti baada ya sare ya 2-2 na wiki tatu baadaye wakacheza fainali
ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, ambako walifungwa na Yanga
2-0.
Kufungwa kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, hakukuwaumiza
sana Simba SC, lakini kipigo cha Jumamosi kinaonekana kuvuruga amani kidogo
katika klabu hiyo. Kuna tuhuma za hujuma, kwamba wapo baadhi ya wachezaji
walicheza chini ya kiwango kuihujumu timu na hata ukiwasikiliza baadhi ya
viongozi wa timu hiyo, unaweza kuamini moja kwa moja kuna hali hiyo ndani ya Azam.
Tayari hatua zimechukuliwa, kocha Stewart Hall ameachiahwa
kazi na Mrisho Ngassa, mmoja wa watuhumiwa wa hujuma ameuzwa ‘kwa hasira’ Simba
SC .
Juzi (Alhamisi), wachezaji wa Azam na makocha wapya wa klabu
hiyo, pamoja na baadhi ya maofisa wa klabu hiyo, asubuhi ya leo waliangua
kilio, tena kile cha kamasi wakati wakimuaga Muingereza Stewart.
Wachezaji walioongoza kwa kilio Uwanja wa Chamazi asubuhi ya
leo, ni Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Salum
Abubakar ‘Sure Boy’, Hajji Nuhu na Erasto Nyoni, wakati kwa maofisa,
aliyeongoza ni Jemedari Said na makocha ni Vivek Nagul.
Stewart mwenyewe pia alibubujikwa machozi wakati anaagana na
family yake, aliyoishi kwa zaidi ya mwaka kwa furaha, amani, upendo na
mafanikio.
Stewart alifukuzwa Jumatano katika klabu hiyo kwa kosa la
kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan
Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame dhidi ya Yanga.
Kikao cha Jumanne cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya
Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kiliafiki kuvunjwa kwa ndoa
hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye
alikuwa anafundisha timu ya vijana, akisaidiwa na Kali Ongala.
Imeelezwa baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya
Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa
kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya
kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa
kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake,
lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye
mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne kufukuzwa
Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil
mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na
Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
Kitu ambacho kinajitokeza kwa haraka ni jinsi ambavyo Azam
imewekeza katika timu yake, kuliko timu nyingine yoyote Tanzania, lakini bado
inashindwa kuongoza katika soka ya nchi hii na ndiyo maana hawataki kuamini
kama wanazidiwa kwa halali na Simba na Yanga.
Lakini ipo haja ya wamiliki na viongozi wa Azam kuwa makini
sana na watu ambao wamewazunguka, kwa sababu wakati mwingine wanaweza kutumia
mianya kama hii ya timu kupoteza mechi, kupandikiza sumu ndani ya timu, ambayo
mwisho wa siku itawasaidia wao kutimiza malengo yao.
Azam ni timu nzuri na imesajili vizuri mno na unaweza kuona
kwenye Kombe la Kagame, bado kuna wachezaji wazuri wapya kama George Odhiambo
‘Blackberry’ hawajatumika vizuri. Nataka tu kuwaambia Azam, mafanikio ambayo
wamepata ndani ya miaka minne ya kucheza Ligi Kuu ni makubwa.
Ni kweli Tukuyu Stars walipanda Ligi kuu mwaka 1986 na moja
kwa moja kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu, lakini soka ya wakati huo siyo soka leo-
utandawazi umebadilisha mambo mengi sana na unapoambiwa soka inahitaji mbinu na
mipango ili kupata matokeo mazuri, ni zaidi ya masuala ya kiufundi.
Haya ni mambo ambayo taratibu Azam wanakwenda wanajifunza,
wanazidi kukusanya uzoefu na itafika wakati nao watakuwa magwiji wa hizo mbinu
na mipango, ambayo niseme wazi mimi siiafiki kabisa, kwa sababu mimi ni muumini
wa soka inayozalisha matoeo halisi uwanjani.
Ila kwa kuwa wakubwa wameshindwa kupambana na huo mchezo
mchafu na ili hata timu nyingine zigombee ubingwa, ziweze kupambana na magwiji
nazo lazima ziige. Ukweli ni kwamba soka yetu inachafuka, lakini kama ndio
staili ambayo wakubwa wameiafiki, tutafanya nini?
Namalizia kwa kuwaambia Azam, wasiruhusu wajanja
wakawavuruga, wamefanikiwa kuwa na timu nzuri iliyokaa pamoja muda mrefu.
Wamefanikiwa kuwa na wachezaji wazuri sambamba na makocha pia.
Kama wanahisi kambi yao iliingiliwa, wakubali matokeo na
wajipange wasithubutu kurudia makosa. Simba na Yanga wana kinga zao za
kupambana na hujuma, kuwapa ahadi ya fedha wachezaji wake wakishinda mechi,
naamini Azam wanazidi kujifunza juu ya namna ya kuicheza soka ya Tanzania.
Mrisho Ngassa inawezekana kweli kwa mapenzi yake
aliyoyadhihirisha kwa Yanga akawa hana madhara kwenye mechi dhidi ya timu hiyo,
lakini vipi mechi dhidi ya Simba, au mechi nyingine zote ambazo Azam itacheza
msimu mzima ujao ikiwemo Kombe la Shirikisho?
Tayari Azam wamekwishachukua maamuzi mazito. Stewart amebaki
historia Chamazi na Ngassa pia. Narudi kule kule kwenye historia ya timu,
halikuwa wazo la akina Bakhresa kumiliki klabu- lakini imetokea tu na wao
wameamua kuwa na timu, tena kwa mikakati mizuri ambayo unaweza kuona mikakati
yake inavyoendelea vizuri.
Uwanja ule Chamazi, nani mwingine nao hata Simba na Yanga.
Akademi ya uhakika ambayo wachezaji wanalelewa na kutunzwa vizuri. Azam iko
anga nyingine kwa sasa. Kitu ambacho Azam inakosa kwa sasa ni utawala huru,
ambao hautaweza kuingiliwa na wamiliki wake kama ilivyo klabu nyingine kubwa
duniani.
Hilo lingekuwapo, sidhani kama Stewart angeingia kwenye
kumbukumbu ya orodha ya makocha wa Azam, kwani kama ingeshindikana kwa Santos,
basi maamuzi ya Itamar kuwafukuza Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Patrick Mutesa
Mafisango (sasa marehemu) yasingepingwa na wamiliki na jiulize angeondoka kwa
sababu gani?
Kwa kukosa utawala huru, Azam itaendelea kuwa kuti kavu na
kocha yeyote atakayerithi nafasi ya Stewart alijue hilo.
0 comments:
Post a Comment