Na Prince Akbar
TIMU ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya
miaka 17, Serengeti Boys sasa itaivaa Misri kwenye raundi ya pili ya michuano
ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 10 za Afrika kwa vijana chini ya miaka
17 zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Awali Serengeti Boys ilikuwa icheze raundi ya kwanza
dhidi ya Kenya, mechi ya kwanza ikichezwa Septemba 9 mwaka huu jijini Dar es
Salaam. Hata hivyo, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) jana lilituma taarifa
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likielezea kujitoa kwenye michuano hiyo.
Serengeti Boys itaanzia nyumbani Oktoba 14 mwaka
huu, wakati ya marudiano itachezwa nchini Misri kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.
Mshindi baada ya mechi hizo mbili ataingia raundi ya tatu ambayo ndiyo ya
mwisho kabla ya kwenda Morocco.
Katika raundi ya tatu ambayo mechi zake zitachezwa
katikati ya Novemba na ya marudiano mwisho mwa mwezi huo, mshindi kati ya
Tanzania/Misri atacheza na mshindi wa mechi ya Congo Brazzaville dhidi ya
Msumbiji/Zimbabwe ambazo zinapambana katika raundi ya kwanza.
Wachezaji wanaounda kikosi cha Serengeti Boys chini
ya Kocha Jakob Michelsen ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi), Hamad Juma
(Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu).
Mabeki ni Abdallah Salum (Mjini Magharibi), Basil
Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo (Azam), Mgaya Abdul
(Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni), Mohamed
Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James (Kinondoni).
Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha
(Coastal Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed
Haroub (Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru
Said (Morogoro) na Selemani Bofu (JKT Ruvu).
Washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza), Calvin
Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin Friday
(Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy).
0 comments:
Post a Comment