Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zakaria Hanspope kulia akishuhudia Ngassa anavyosaini |
HAKUNA utata tena. Tamka Mrisho Khalfan Ngassa ni
mchezaji halali wa Simba SC. Mchana huu, klabu ya Simba imefanikiwa kumalizana
na Ngassa na kusaini naye mkataba wa miaka miwili, ambao umemfanya aondoke na
zaidi ya Sh. Milioni 35, Milioni 12 akipewa taslimu na nyingine akipewa gari.
Katika mkataba huo wa Simba na Ngassa, mshambuliaji
huyo atakuwa akilipwa Sh. Milioni 2 mshahara kwa mwezi, Milioni 1 ipo kwenye
mkataba na Milioni 1 atakuwa akiongezewa na mtu.
Nani kakamilisha dili hili? Ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Usajili ya Simba SC, Hans Pop ndiye katoa fedha hizo na baada ya kumsainisha
na kumkabidhi haki yake, ili kumuondolea usumbufu akambadilishia ‘chipu’ ya
simu, ili akina Seif Magari wasimpate.
Jana Simba ilimnunua Ngassa kutoka Azam kwa Sh.
Milioni 25, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Yanga akagoma kwa sababu
hakushirikishwa katika dili hilo.
Leo asubuhi Ngassa alizungumza na Mwenyekiti wa Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Alex Mgongolwa kupinga kuuzwa kwake
katika klabu hiyo, akitokea Azam FC bila kuhusishwa.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo, Ngassa alisema
kwamba hajafanya mazungumzo na Simba SC wala Azam FC juu ya uhamisho. “Mimi
sijui chochote, na sikatai kuhamishwa, kwa sababu mimi soka ni kazi yangu na
ninaweza kucheza popote, ila taratibu zifuatwe tu,”alisema.
Ngassa alisema baada ya kuona mambo yanakwenda
kinyume cha utaratibu, aakaamua kulifikisha suala lake Kamati ya Sheria,
Maadili na Hadhi za Wachezaji ili haki itendeke.
Kwa hatua hiyo, Simba imeamua kuzungumza naye na
kumaliza naye na sasa kijana ataanza mazoezi Simba wiki ijayo, akitoka Mwanza
anakokwenda leo kusalimia wazazi.
Azam ilifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya
mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya
Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC).
Na uamuzi huo, ni wa mzee Said Salim Bakhresa
mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa
bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka iwezekanavyo.
Ngassa alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba
wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga miaka miwili iliyoipita kwa dau la
Sh. Milioni 55, lakini wasiwasi unakuja kwamba, Ngassa ana mapenzi na Yanga na
kwa Simba kumsajili, kuna hatari yaliyotokea akiwa Azam, yatajirudia hata akiwa
kwa Wekundu wa Msimbazi.
Mapema jana mchana, Stewart Hall, kocha Muingereza
wa Azam FC jana alifukuzwa katika klabu
hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga
Mrisho katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY ilizipata kutoka ndani
ya Azam, zilisema kwamba kikao cha jana cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi
ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo
na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa
anafundisha timu ya vijana.
Habari zinasema kwamba, mapema baada ya mechi ya
Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na
kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na
kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea
Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu
kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya
kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Kwa kutua Simba, Ngassa amefuata nyayo za baba yake
mzazi Khalfan Ngassa ambaye alichezea klabu hiyo kati ya 1990 hadi 1992.
0 comments:
Post a Comment