Ngassa akiibusu jezi ya Yanga |
Na Prince Akbar
THAMANI ya Mrisho Khalfan Ngassa katika klabu yake mpya, Simba SC kwa mujibu wa Mkataba aliosaini jana ni Sh. Milioni 30, kwa mwaka mbali na mishahara na marupurupu mengine.
Simba ilifanikiwa kumalizana na Ngassa jana na kusaini naye mkataba wa miaka miwili, ambao umemfanya aondoke na zaidi ya Sh. Milioni 35, Milioni 12 akipewa taslimu na nyingine akipewa gari.
Katika mkataba huo wa Simba na Ngassa, mshambuliaji huyo atakuwa akilipwa Sh. Milioni 2 mshahara kwa mwezi, Milioni 1 ipo kwenye fomu ya mkataba na Milioni 1 atakuwa akiongezewa na mtu.
Usajili wa mchezaji huyo, ulikakamilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Hans Pop, ambaye ndiye alitoa fedha hizo na baada ya kumsainisha na kumkabidhi haki yake, ili kumuondolea usumbufu akambadilishia ‘chipu’ ya simu, ili akina Seif Magari wasimpate.
Juzi Simba ilimnunua Ngassa kutoka Azam kwa Sh. Milioni 25, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Yanga akagoma kwa sababu hakushirikishwa katika dili hilo.
Kwa kumuongeza ‘kifurushi’ cha Sh. Milioni 35, ina maana Simba imemsajili Ngassa kwa Sh. Milioni 60 kwa miaka miwili, ambalo ni dau kubwa zaidi la usajili kwa mchezaji huyo tangu aanze kucheza soka.
Yanga ilimsaini kwa Sh. Milioni 25 jumla kutoka Kagera Sugar mwaka 2007 pamoja na uhamisho wake akasaini mkataba wa miaka mitatu, wakati miaka miwili iliyopita, Azam ilimsajili kwa Sh. Milioni 55 pamoja na uhamisho wake (Sh. Milioni 30) ikimsainisha mkataba wa miaka mitatu, ambao ulitarajiwa kumalizika mwakani.
Azam ilifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Na uamuzi huo, ni wa mzee Said Salim Bakhresa mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka iwezekanavyo.
0 comments:
Post a Comment