Kavumbangu |
Na
Prince Akbar
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi, Didier
Kavumbangu amewasili jana usiku kujiunga na klabu yake mpya, Yanga SC ya Dar es
Salaam, akitokea Atletico ya Burundi.
Kavumbangu anatarajiwa kuanza mazoezi leo jioni na
wenzake, kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Yanga, ambao ni mabingwa wa Afrika Mashariki na
Kati, walianza maandalizi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana na Kocha
Mkuu wa klabu hiyo, Mbelgiji Tom Saintefiet aliwataja wachezaji ambao
hawakufika jana kuwa ni Hamisi Kiiza, ambaye ameitwa timu ya taifa ya Uganda,
The Cranes, Ibrahim Job na David Luhende ambao bado wapo kwao Mwanza, wakati
Juma Abdul bado ni majeruhi.
Tom alisema wachezaji wengine waliokosekana mazoezini
jana ni wale ambao wapo timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20,
Ngorongoro Heroes, Frank Damayo, Omega Seme na Simon Msuva.
Yanga ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati,
Jumamosi kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wafungaji
Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hilo lilikuwa taji la tano la michuano hiyo kwa
Yanga kihistoria, baada ya awali kutwaa mataji ya Kombe hilo katika miaka ya
1975 Zanzibar, 1993, 1999 Uganda na 2011 Dar es Salaam na mara zote hizo, ikiwa
chini ya makocha wa kigeni.
Mwaka 1975 Yanga ilibeba Kombe hilo, ikiwa chini ya
kocha kutoka Jamhuri ya Kodemokrasia ya Kongo (DRC), Tambwe Leya (sasa
marehemu), 1993 chini ya kocha kutoka Burundi, Nzoyisaba Tauzany pia marehemu,
1999 chini ya Raoul Shungu kutoka DRC na mwaka jana chini ya Mganda Sam Timbe.
Wiki hii ziliibuka habari kwamba, baada ya kuipa
Yanga Kombe la Kagame,Tom ameomba kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Kenya,
Harambee Stars, lakini mwenyewe alisema baadaye akizungumza na BIN
ZUBEIRY kwamba tangu amejiunga na klabu hiyo mwezi uliopita hajawahi
kuomba kazi sehemu nyingine yoyote.
Mtakatifu Tom alisema anashangazwa mno na habari
hizo za kizushi, za kizandiki zenye kulenga kumchonganisha yeye na mwajiri
wake, Yanga SC.
“Nakumbuka niliwahi kuomba kazi Chama cha Soka Kenya
(KFF) kufundisha timu yao ya taifa (Harambee Strars), lakini ilikuwa ni muda
mrefu sana hata kabla sijaomba kazi Yanga,”alisema.
Blog moja iliyowahi kuandika Iddi Kipingu anagombea
Uenyekiti Yanga, wiki hii iliandika habari yenye kichwa kisemacho; “WIKI MOJA
BAADA YA KUIPA UBINGWA: KOCHA WA YANGA TOM SAINTFIET ATUMA MAOMBI YA
KUIFUNDISHA HARAMBEE STARS,”.
Akiizungumzia habari hiyo, Mtakatifu alisema; “Ni
uongo, tangu nimesaini mkataba na Yanga, sijawahi kuomba kazi pengine
popote,”alisema.
0 comments:
Post a Comment