Albert Mweta |
Na
Mahmoud Zubeiry, Arusha
MAKIPA wa akiba wa klabu ya Simba, Albert Mweta na
Hamadi Waziri jana walionyesha viwango vizuri katika mchezo wa kirafiki wa
klabu hiyo dhidi ya Mathare United ya Kenya, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid,
Arusha.
Hamadi Waziri |
Mweta aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Toto
African ya Mwanza jana alianza na kumaliza dakika 45 bila kufungwa, kabla ya
kufungwa bao moja kipindi cha pili, tena baada ya mabeki Paschal Ochieng na
Juma Nyosso kuchanganyana.
Akiwa langoni, Mweta aliokoa hatari kadhaa na kuonyesha
kwamba ni kipa aliye tayari hata mechi kubwa.
Alipoingia Hamadi aliyesajiliwa msimu huu kutoka JKT
Oljoro ya Arusha, naye pia alionyesha kiwango kizuri na kuokoa michomo kadhaa
ya hatari.
Makipa hao, walidaka jana kwa sababu kipa namba moja
wa Simba, Juma Kaseja alikuwa mgonjwa.
Katika mchezo huo, bao la penalti dakika ya 81
lililofungwa na kiungo Kiggi Makassy, lilitosha kuipa Simba ushindi wa mabao
2-1, kabla ya kuingia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC wiki mbili
zijazo mjini Dar es Salaam.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao
na kipindi cha pili, Simba SC inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick
ilipata bao la kuongoza dakika ya 53, mfungaji mshambuliaji kutoka Ghana,
Daniel Akuffo aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Amir
Maftah.
Mathare walisawazisha bao hilo dakika ya 68,
mfungaji Daniel Mwaura aliyeipasua ngome ya Simba SC, iliyokuwa ikiogozwa na
Paschal Ochieng na Juma Nyosso.
Beki wa Mathare alimuangusha kwenye eneo la hatari,
Uhuru Suleiman dakika ya 80 na ushei na refa akaamuru ipigwe penalti,
iliyopachikwa kimiani kiufundi kwa guu la kushoto la Kiggi Makassy.
Simba ilicheza vizuri mechi hiyo, leo hii Haruna
Moshi ‘Boban’ akirudishwa katika nafasi ya kiungo baada ya kupatikana kwa
washambuliaji halisi. Alicheza kwa utulivu, akigawa vizuri mipira na hata
kuwapokonya mipira viungo wa timu pinzani.
Dakika za mwishoni ilishuhudiwa Boban akipitia mpira
kwa nguvu miguuni mwa mshambuliaji wa Mathare, baada ya Maftah kupitwa,
kuashiria kwamba kijana amebadilika si Yule wa kukaba kwa macho.
Feliz Sunzu na Akuffo walikuwa wanapishana vizuri
pale mbele na waliitia misukosuko ngome ya Mathare- zaidi ni kwamba wawili hawa
wanahitaji muda zaidi wa kucheza pamoja ili kutengeneza safu kali ya
ushambuliaji ya Simba SC.
Juma Kaseja na Mrisho Ngassa hawakushiriki kabisa
mechi ya leo kwa sababu walikuwa wagonjwa na Keita alimpisha Nyosso baada ya
kuumia.
Simba itamenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya
Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya
Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa
soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba
kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001,
Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi
ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare
ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa
kuifunga Yanga mabao 2-0.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa;
Wilbert Mweta/Hassan Waziri, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah/Paul Ngalema,
Paschal Ochieng, Komabil Keita/Juma Nyosso, Salum Kinje/Ramadhan Chombo
‘Redondo’, Mwinyi Kazimoto/Haruna Shamte, Haruna Moshi, Felix Sunzu, Abdallah
Juma/Amri Kiemba na Daniel Akuffo/Uhuru Suleiman.
MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
Mwaka Mshindi Matokeo
2001 Yanga 2-1 Simba
2010 Yanga
0-0 Simba (3-1penalti)
2011 Simba
2-0 Yanga
0 comments:
Post a Comment