Hamadi Waziri |
Na Prince Akbar
HAMADI Waziri, mmoja wa makipa wa akiba wa Simba,
amesema anafurahi kuwa katika timu hiyo pamoja na kipa bora kabisa nchini, Juma
Kaseja kwani anajifunza mambo mengi kutoka kwa Tanzania One huyo.
Akizungumza mjini Arusha, juzi baada ya mechi dhidi
ya Mathare United ya Kenya, Hamadi aliyesajiliwa kutoka JKT Oljoro alisema
kwamba Kaseja ni kipa mwenye uwezo wa hali ya juu na kuwa naye pamoja
ananufaika mno kwa kujifunza mambo mengi kutoka kwa kipa huyo.
“Kaseja pamoja na kuwa na Nahodha wetu, pia ni kaka
yetu ambaye anatuongoza vizuri, kwa kweli binafsi nafurahia sana fursa
hii,”alisema.
Lakini pia kipa huyo chipukizi aliyeonyesha uwezo
mkubwa kwa siku chache za kuwa na klabu huyo, alisema pia anafurahi mno kuwa
chini ya kocha maalum kwa makipa, James Kisaka ambaye anawafundisha vizuri.
“Niseme tu mimi sijawahi kuwa chini ya kocha wa
makipa ambaye anafundisha vizuri kama kocha Kisaka, naamini kabisa hii ni fursa
nzuri kwangu kukuza uwezo wangu ili siku moja nitimize ndoto zangu za kuwa kipa
bora nchini,”alisema Waziri.
Makipa wote wa akiba wa Simba, Waziri na Albert
Mweta juzi walionyesha viwango vizuri katika mchezo wa kirafiki wa klabu hiyo
dhidi ya Mathare United ya Kenya, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Mweta aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Toto African
ya Mwanza juzi alianza na kumaliza dakika 45 bila kufungwa, kabla ya kufungwa
bao moja kipindi cha pili, tena baada ya mabeki Paschal Ochieng na Juma Nyosso
kuchanganyana.
Akiwa langoni, Mweta aliokoa hatari kadhaa na
kuonyesha kwamba ni kipa aliye tayari hata mechi kubwa na alipoingia Hamadi naye
pia alionyesha kiwango kizuri na kuokoa michomo kadhaa ya hatari.
Makipa hao, walidaka jana kwa sababu kipa namba moja
wa Simba, Juma Kaseja alikuwa mgonjwa. Katika mchezo huo, bao la penalti dakika
ya 81 lililofungwa na kiungo Kiggi Makassy, lilitosha kuipa Simba ushindi wa
mabao 2-1, kabla ya kuingia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC wiki
mbili zijazo mjini Dar es Salaam.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao
na kipindi cha pili, Simba SC inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick
ilipata bao la kuongoza dakika ya 53, mfungaji mshambuliaji kutoka Ghana,
Daniel Akuffo aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Amir
Maftah.
Mathare walisawazisha bao hilo dakika ya 68,
mfungaji Daniel Mwaura aliyeipasua ngome ya Simba SC, iliyokuwa ikiogozwa na
Paschal Ochieng na Juma Nyosso.
Beki wa Mathare alimuangusha kwenye eneo la hatari,
Uhuru Suleiman dakika ya 80 na ushei na refa akaamuru ipigwe penalti,
iliyopachikwa kimiani kiufundi kwa guu la kushoto la Kiggi Makassy.
Simba ilicheza vizuri mechi hiyo, Haruna Moshi
‘Boban’ akirudishwa katika nafasi ya kiungo baada ya kupatikana kwa
washambuliaji halisi. Alicheza kwa utulivu, akigawa vizuri mipira na hata
kuwapokonya mipira viungo wa timu pinzani.
Dakika za mwishoni ilishuhudiwa Boban akipitia mpira
kwa nguvu miguuni mwa mshambuliaji wa Mathare, baada ya Maftah kupitwa,
kuashiria kwamba kijana amebadilika si yule wa kukaba kwa macho.
Felix Sunzu na Akuffo walikuwa wanapishana vizuri
pale mbele na waliitia misukosuko ngome ya Mathare- zaidi ni kwamba wawili hawa
wanahitaji muda zaidi wa kucheza pamoja ili kutengeneza safu kali ya
ushambuliaji ya Simba SC.
Juma Kaseja na Mrisho Ngassa hawakushiriki kabisa
mechi hiyo kwa sababu walikuwa wagonjwa na Keita alimpisha Nyosso baada ya
kuumia.
Simba itamenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya
Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya
Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa
soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba
kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001,
Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi
ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare
ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa
kuifunga Yanga mabao 2-0.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa;
Wilbert Mweta/Hassan Waziri, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah/Paul Ngalema,
Paschal Ochieng, Komabil Keita/Juma Nyosso, Salum Kinje/Ramadhan Chombo
‘Redondo’, Mwinyi Kazimoto/Haruna Shamte, Haruna Moshi, Felix Sunzu, Abdallah
Juma/Amri Kiemba na Daniel Akuffo/Uhuru Suleiman.
0 comments:
Post a Comment