Zacharia Hans Poppe |
Na Prince Akbar
MWANACHAMA Maarufu wa klabu ya Simba, Zacharia
Hans Poppe amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba ‘Firend of
Simba’ kufuatia kikao kilichoo juzi, katika hoteli ya JB Delmonte.
Hans Poppe anachukua nafasi ya Salum Abdallah
aliyeongoza kundi hilo kwa zaidi ya miaka mitano na kuleta mafanikio makubwa
ndani ya klabu ya Simba, kwa uhamasishaji wa kundi hilo lilijizolea umaarufu
mkubwa ndani ya klabu hiyo.
Mbali na Hans Poppe, wengine waliochaguliwa ni Adam
Mgoyi anayekuwa Makamu Mwenyekiti, nafasi ya Katibu Mkuu imekwenda kwa Mulamu
Nghambi, wakati nafasi ya Katibu msaidizi amechaguliwa Niki Magariza na Juma
Pinto atakuwa msemaji wa kundi hilo.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Hans Poppe
alisema atajitahidi kufanya kila aliwezalo kuhakikisha kundi hilo linafanya
kazi kazi kwa kushirikiana na uongozi kwa lengo la kuleta maelewano yatakayoijenga
Simba imara na kuleta burudani kwa wapenzi na mashabiki.
“Sisi ni marafiki wa Simba, tunachokifanya lazima
kiendane na tasfsiri ya neno lenyewe na isije ikawa tofauti kuwa ni maadui wa
Simba, naomba ushirikiano wa pamoja kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu,”
alisema Hans Poppe katika shukrani zake.
Awali mmoja wa waasisi wa kundi hilo, Jaji mstaafu
Thomas Mihayo alisema mwelekeo na dira ya kundi hilo lilipotea, hivyo kuwa na
imani kwa viongozi wapya kufanya kazi ambayo itakuwa na faida kwa maendeleo ya
Simba.
Jaji Mihayo alisema kundi hili limekuwa na malengo
mazuri lakini kinachokwamisha sasa hivi ni wanachama wake kutokuwa wamoja na
kuwataka kurudisha umoja na kufuatialia kwa mambo ambayo yanapangwa kwa ajili ya utekelezaji.
Viongozi wa zamani waliomaliza muda wake ni Salum
Abdallah (Mwenyekiti),Johnson Masabala (Makamu Mwenyekiti) na Issa Batenga
aliyekuwa katibu wa kundi hilo.
HANS POPPE NI NANI?
Kama anavyotambulishwa,
jina lake ni Zacharia Hans Poppe, ambaye alizaliwa mwaka 1956 mjini Dar es
Salaam na kukulia mkoani Iringa.
Baada ya kumaliza elimu
ya sekondari, Zacharia alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambako
alifikia cheo cha Kapteni, kabla ya kuachishwa kazi na kuhukumiwa kifungo cha
maisha jela, kwa tuhuma za uhaini, dhidi ya serikali ya awamu ya kwanza, ya
hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1983.
Lakini mwaka 1995,
Zacharia aliachiwa huru kwa msamaha wa rais wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan
Mwinyi, mwezi mmoja kabla hajamuachia Ikulu ya Tanzania, Benjamin William
Mkapa, rais wa awamu ya tatu.
Kama zinavyosema sheria
za nchi, mtu aliyehukumiwa kifungo, hana haki ya kugombea wadhifa wowote au
kuajiriwa tena, Zacharia naye hakuweza kurejea kazini, badala yake akaamua
kujiajiri, kwa kuanzisha miradi yake mwenyewe, ambayo leo ikiwa ni miaka 17
baadaye, miradi hiyo imesimama imara.
HANS POPE NA SIMBA SC:
Alianza kuipenda Simba
SC mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na zaidi mwenyewe
anasema, mechi ambayo ilimfanya ajitamke rasmi yeye ni Simba damu ilikuwa dhidi
ya wapinzani wa jadi, Yanga Juni 23, mwaka 1973, ambayo Wekundu wa Msimbazi,
walishinda 1-0, bao pekee la Haidari Abeid ‘Muchacho’ dakika ya 68.
“Nakumbuka ilikuwa ni
ligi ya mtoano, tuliitoa Yanga tukaenda hadi kuchukua ubingwa kwa kuwafunga
Lake kule Kigoma, kipindi kile Simba ilikuwa inaundwa na vijana wadogo wadogo
tu, ilikuwa raha sana.
Ni Simba ambayo mwaka
1974 iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kuchukua hili Kombe ambalo linaitwa
la Kagame, wakati huo linaitwa la Afrika Mashariki na Kati na pia ilifika Nusu
Fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), tukatolewa kwa fitina
na Waarabu (Mehallal El Kubra),”anakumbusha Zacharia.
Zacharia anasema
aliendelea kuwa mpenzi wa Simba, hadi baadaye akaamua kuwa mwanachama.
Lakini siku zote
alikuwa pembeni, hadi lilipoundwa kundi la Friends Of Simba ndipo akaamua
kujiunga nalo, ili naye aweze kutoa michango yake zaidi.
Anasema wakati wa
uongozi wa Mwenyekiti, Hassan Daalal ambao ulionekana kuelemewa na majukumu ya
timu, ndipo alipata umaarufu zaidi ndani ya Simba, kutokana na kusaidia zaidi.
Anasema uongozi wa Daalal
baada ya kugundua umuhimu wake ukaamua kumpa jukumu la kusimamia fedha na
anasema alifanikiwa kudhibiti fedha na kuanzisha mpango wa kuiwezesha klabu
kujitegemea katika mambo mbalimbali, ikiwemo suala la usajili badala ya
kutembeza bakuli.
Anasema kutokana na
kufanya vizuri katika jukumu hilo, wengi miongoni mwa wanachama na viongozi wa
Simba wakamuomba agombee Uenyekiti. “Lakini siku zote kuna kitu kilikuwa
kinanipa shinda. Nilikuwa sijui ni msamaha wa aina gani niliopewa na rais,
unajua rais anaweza pia kutoa msamaha wa kufuta na kosa pia,”anasema.
“Lakini nilijaribu sana
kufuatilia ili kujua aina ya msamaha wangu, nilikwenda hadi Magereza, lakini
hawakunipa jibu, mwishowe nikaamua kuacha tu, sasa nilipojaribu kuomba uongozi
Simba, ndipo TFF wakatumia kipengele cha mimi kuwahi kufungwa
kuniengua,”anasema.
Hata hivyo, Zacharia
anasema kwamba umefika wakati sheria hiyo irekebishwe kwa mtu anayetoka jela
awekewe muda maalum wa kuzuiwa kushiriki katika madaraka na ajira, kabla ya
kuruhusiwa kurejea kwenye maisha ya kawaida.
“Unajua mtu anapofungwa
lengo ni kumfundisha, ili baadaye akirudi uraiani awe raia mwema, sasa
haiwezekani arudi uraiani halafu amewekewa vipingamizi, mimi naamini ipo haja
ya kurekebisha hii sheria,”anashauri Zacharia.
Zacharia anasema pamoja
na kuukosa Uenyekiti, anashukuru amepata fursa ya kuendelea kuisaidia klabu
yake, baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili.
“Nimesaidia sana
kuiwezesha klabu kukusanya fedha na kutunza, ambazo zimetuwezesha kujitegemea
kufanya usajili wetu kwa takriban asilimia 85.
Na ni fedha ambazo zimetokana na mapato ya milangoni, udhamini wa TBL,
pango za majengo ya klabu na mauzo ya wachezaji (Mbwana Samatta, Patrick Ochan
na Mussa Mgosi) na nyingine kutokana na michango tunayojichangisha,”anasema.
NINI JUKUMU LA KAMATI
YA USAJILI YA SIMBA?
Zacharia anasema
kwamba, Kamati yake hupokea mapendekezo kutoka kwa Kamati ya Ufundi juu ya aina
ya wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa, ndipo wao hutafuta wachezaji.
“Kwanza, Kamati ya
Ufundi inakuwa imekutana na benchi la ufundi, imepewa ripoti ya kitaalamu,
wanajadiliana ndio wanatuletea orodha ya wachezaji wanaotakiwa kwa maana ya
nafasi zao. Sasa sisi tunakwenda kufanya tathmini ya wachezaji gani bora ndani
na nje ya nchi, tukiwapata, tunarudi kwa Kamati ya Ufundi, tunawapa majina,
sasa wao ndio wanakwenda kuwafuatilia uwezo wao na wakiridhika, wanatupa jibu,
sisi ndio tunawasaini,”anasema.
Akifafanua, Zacharia
anasema kwamba hakuna mtu anayesajili kwa fedha zake Simba SC, bali ni fedha za
klabu.
“Sisi Kamati ya Usajili
tunapotaka kumsajili mchezaji, tunakwenda kwa Kamati ya Fedha, sasa wao ndio
wanatuambia uwezo wao unafikia wapi, pale ambako pamezidi sasa tunatoka
tunakwenda kuchangishana na ndugu zetu Friends Of Simba na wadau wengine
tunamalizana na mchezaji,”anasema.
Anasema ndani ya Simba
SC hivi sasa hakuna utaratibu wa mtu mmoja kumsajili mchezaji kwa fedha zake,
kwa sababu hiyo imewahi kuleta matatizo ndani ya klabu miaka ya nyuma na sasa
wamechukua tahadhari.
“Inatokea mtu
anatofautiana na uongozi, anaamua kumtumia mchezaji wake kuihujumu timu, sasa
hiyo haipo tena,”anasema.
Alipoulizwa kuhusu
wachezaji kusajiliwa na kuachwa kabla hawajaitumikia timu, Zacharia anasema;
“Hao ni wale ambao wanaingia nje ya utaratibu tuliojiwekea, inatokea mtu tu
anaamua kumsajili kwa utashi wake na fedha zake. Na ikitokea hafai sisi
tunamkata tu. Ila inatokea mtu anasajili mchezaji, anamleta, tunamuona anafaa,
tunampitisha, ila lazima apite katika utaratibu wetu tuliojiweka na anasaini
mkataba na klabu, si mtu,”anasema.
Lakini Zacharia anasema
kwamba kutokana na kiwango cha mishahara kutoka kwa wadhamini wao wakuu, TBL
(kupitia Kilimanjaro Premium Lager)- inabidi baadhi ya wachezaji ambao
wanalipwa zaidi, fedha zitoke nje ya utaratibu wa kawaida. Ndiyo utaona mtu
katika mkataba wake analipwa kiasi fulani, lakini kiasi kingine kipo katika
makubaliano mengine,”anasema.
Lakini Zacharia anasema
kutokana na mradi wao wa timu za vijana kuendelea vizuri, anaamini itafika
wakati Simba SC haitakuwa ikitumia fedha nyingi katika kusajili na pia itakuwa
ikiingiza fedha nyingi katika kuuza wachezaji.
“Tuna timu nzuri ya
U-17 na U-20 na kama uliona U-20 imeitoa timu ya wakubwa ya Azam FC katika
michuano ya Bank ABC na Jumamosi inacheza fainali na Mtibwa Sugar tukiwa na
matumaini makubwa ya kuchukua Kombe, wachezaji wote wa timu za vijana wanalipwa
mishahara, makocha wao wanalipwa pia, kwa ujumla timu zinahudumiwa vizuri na
tumepata wachezaji wasiopungua watano wa kupandisha kikosi cha kwanza msimu
huu.
Wengine wapo hadi timu
ya taifa ya wakubwa, kama yule kijana Messi (Ramadhani Singano) na Mkude (Jonas
Gerald). Na tayari kuna wachezaji wa timu ya vijana ya Simba wana ofa ya kwenda
kufanya majaribio Ulaya, kwa hivyo unaweza kuona tunaelekea kuzuri,”anasema.
NINI DUKUDUKU LAKE?
Vurugu katika usajili
na uendeshaji soka kwa ujumla, ni vitu ambavyo Zacharia hataki hata kuvisikia.
Anatolea mfano Yanga walivyofanya kwa beki wa APR ya Rwanda, Mbuyu Twite,
kwamba hayo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati.
“Mwenzako
amekwishazungumza na mchezaji, wewe huna sababu ya kwenda kuzungumza naye na
kumrubuni, kupandisha dau, hayo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati.
Tazama kwa mfano
usajili wa Robin van Persrie kutoka Arsenal, Manchester United wamemalizana
naye kistaarabu, japokuwa Manchester City nao walikuwa wanamtaka, lakini
hukuwasikia kumfuata mchezaji eti kuahidi kumpandia dau, huo sio ustaarabu,
mwenzako akishamalizana na mchezaji, wewe tafuta mwingine.
Ona sisi Simba, Yanga
wametupokonya Kevin Yondan, tumemfuata Twite, wamemchukua pia, lakini bado
tumepata beki mwingine mzuri tu, tena zaidi ya hao wote, hakuna haja ya kugombea
mchezaji,”anasema, Zacharia, baba watoto wa tisa, kutoka kwa mama wanne
tofauti.
Mahojiano kati ya BIN
ZUBEIRY na Zacharia Hans Poppe yalifungwa kwa swali kuhusu timu
anazopenda na wachezaji kwa sasa duniani, ambalo majibu yake ni; “Ulaya napenda
Arsenal pale England, Bayern Munich pale Ujerumani na Barcelona kwa Hispania…
kwa wachezaji kwa kweli ni Alex Song, Robin van Persie na Frank Ribbery,”.
0 comments:
Post a Comment