John Bocco 'Adebayor' |
Na
Princess Aisa
MAKALI ya mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael
Bocco ‘Adebayor’ yameongezeka mno tangu arejee kutoka Afrika Kusini, alikokuwa
anafanya majaribio ya kujiunga na Super Sport United, ambako inaelezwa alifuzu.
Bocco amekuwa akifunga sana mabao katika mazoezi ya
timu hiyo, Uwanja wa Chamazi na hata uwezo wake wa kumiliki mpira, kuwatoka
mabeki, kasi na kupaa juu kupiga vichwa, vimeongezeka pia.
Hizi ni habari njema kwa Azam washindi wa pili wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayofundishwa na kocha wake Raia wa Serbia
Boris Bunjak, kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya mabingwa Simba SC,
Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bocco ambaye alifunga mabao mawili, wakati Azam
inaichapa mabao 8-0 Transit Camp Jumamosi Uwanja wa Chamazi, mengine yakifungwa
na Papie, mshambujliaji mpya aliye kwenye majaribio kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kipre Herman Tcheche na Abdulhalim Humud kila
mmoja nae alifunga mabao mawili, alifanya majaribio kwa wiki mbili na Super
Sport.
Katika majaribio, imeelezwa Bocco amefuzu na Azam
inataka ilipwe dola za Kimarekani 200,000 ili kumuuza, ingawa klabu ya Afrika
Kusini inaonekana kutaka kutoa dau dogo chini ya hapo. Imeelezwa wiki hii viongozi wa Super Sport wanatarajiwa
kuja nchini kujadili zaidi juu ya kumnyakua mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu
msimu uliopita.
Azam inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao
ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo
wake wa kwanza katika historia ya Ngao hiyo..
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya
Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa
soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba
kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001,
Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi
ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare
ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa
kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na
Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na
Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na beki
mahiri Shomari Kapombe, aliyemajeruhi kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment