Na Mahmoud Zubeiry |
KWA muda mrefu, kundi
la Friends Of Simba limekuwa likishutumiwa kuwahujumu viongozi waliopo
madarakani na hii iliwahi kutokea hata Kassim Mohamed Dewji mmoja wa waasisi wa
kundi hilo, akiwa madarakani.
Kassim alikuwa Katibu
Mkuu chini ya Mwenyekiti Juma Salum Muhovuge na Makamu, Ramadhani Balozi (wote
marehemu)- lakini uongozi wao pia uliwahi kulishika uchawi kundi la Friends Of
Simba.
Kassim hakuwa mmoja wa
viongozi waliolishika uchawi kundi la Friends, bali alituhumiwa naye kwa pamoja
kuwa kibaraka wa kundi hilo katika kutekeleza mipango yao hasi.
Mwisho wa siku K.D.
alijiuzulu Simba na tangu wakati huo, haujatokea utawala ambao tangu unaingia
madarakani hadi unaondoka haukuwahi kulishika uchawi kundi hilo, kiasi kwamba
hadi likapewa jina na Mwina Kaduguda, Enemies Of Simba, yaani maadui wa Simba.
Kaduguda alikuwa Katibu
Mkuu katika utawala uliopita chini ya Daalal na hata sasa ‘Mr maneno mengi,
vitendo haba’, Ismail Aden Rage akiwa madarakani, Friends imekwishazungumzwa
vibaya.
Hiyo ndiyo picha ya
Friends of Simba ndani ya Simba, lakini bado ukimtazama mtu mmoja mmoja kutoka
wale Friends of Simba, inakuwa vigumu kuamini hilo.
Wanaoneka watu wenye
mapenzi haswa na Simba, ambao wanachoweza ni kusaidia tu timu yao na si zaidi
ya hapo. Friends of Simba ni kundi ambalo linaanza mi naliona, Mungu amrehemu
marehemu Amin Bakhroon katika jitihada za awali za uundwaji wa kundi hilo,
alikuwepo.
Na moja ya kazi za
awali za Friends ni usajili wa beki Paul John Masanja na winga Ephraim Makoye
kutoka Yanga mwaka 2000, ambao hata hivyo haukufanikiwa kutokana na klabu yao
kutowaruhusu, ingawa baadaye wachezaji wote hao walichezea Simba.
Binafsi nimekuwa
nakerwa na tuhuma hizo, kwa sababu naona
haziendani na dhamira ya kundi hilo- zaidi kilichopo ni mambo ya mjini, kupakana
matope ili kuharibiana. Na ni kuharibiana kweli, kwa sababu kwa watu walio
mbali na ukweli wanaweza kuubeba uongo na kusadiki.
Vema, F.O.S. Alhamisi
imepata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti,
Zacharia Hans Poppe katika
kikao kilichofanyika hoteli ya JB Belmonte, katikati ya Jiji.
Hans Poppe anachukua
nafasi ya Salum Abdallah, aliyeliongoza kundi hilo kwa zaidi ya miaka mitano na
kuleta mafanikio makubwa ndani ya Simba, kwa uhamasishaji wa kundi hilo lililojizolea
umaarufu mkubwa ndani ya klabu hiyo.
Mbali na Hans Pope,
wengine waliochaguliwa ni Adam Mgoyi anayekuwa Makamu Mwenyekiti, nafasi ya
Katibu Mkuu imekwenda kwa Mulamu Nghambi, wakati nafasi ya Katibu Msaidizi
amechaguliwa Niki Magariza na Juma Pinto atakuwa Msemaji wa kundi hilo.
Baada ya kuchaguliwa,
Hans Poppe aliahidi kufanya jitihada kuhakikisha
kundi hilo linafanya kazi kwa kushirikiana na uongozi kwa lengo la kuleta
maelewano yatakayoijenga Simba imara na kuleta burudani kwa wapenzi na
mashabiki.
“Sisi ni marafiki wa
Simba, tunachokifanya lazima kiendane na tafsiri ya neno lenyewe na isije ikawa
tofauti kuwa ni maadui wa Simba, naomba ushirikiano wa pamoja kuhakikisha
tunafanikisha malengo yetu,” alisema Hans Poppe katika shukrani zake.
Awali, mmoja wa waasisi
wa kundi hilo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo alisema mwelekeo na dira ya kundi
hilo vilipotea, hivyo kuwa na imani kwa viongozi wapya kufanya kazi ambayo
itakuwa na faida kwa maendeleo ya Simba.
Jaji Mihayo alisema
kundi hili limekuwa na malengo mazuri, lakini kinachokwamisha sasa hivi ni wanachama
wake kutokuwa wamoja na kuwataka kurudisha umoja na kufuatialia kwa karibu mambo
ambayo yanapangwa kwa ajili ya utekelezaji.
Viongozi waliomaliza
muda wao mbali na Salum Abdallah (Mwenyekiti), wengine ni Johnson Masabala
(Makamu Mwenyekiti) na Issa Batenga aliyekuwa katibu wa kundi hilo.
Hans Poppe kwa pamoja
na Jaji Mihayo wametoa rai nzuri kuhusu mustakabali wa F.O.S.- kwanza
kushirikiana na uongozi uliopo madarakani ili kuondoa dhana potofu.
Matatizo, misigano ni
changamoto za kawaida, ambazo umefika wakati sasa watu wajifunze kuyakabili
hayo mambo badala ya kujenga chuki na uadui usio na msingi.
Na taasisi yoyote bora,
itatokana na wafuasi wasioburuzwa- hivyo katika namna hii malumbano, misigano
lazima viwepo katika kila mtu kuonyesha msimamo wake, mwisho wa siku mwenye
hoja ndiye mshindi.
Naona ipo hoja chini ya
Hans Poppe tukaishuhudia F.O.S. mpya, itakayorejesha imani yake mbele ya
wapenzi, wanachama na wadau wengine wote wa Simba.
Ingawa wengi walianza
kumfahamu Hans Poppe, aliyezaliwa mwaka 1956 mjini Dar es Salaam siku za
karibuni na wengi wakiamini huyu ni mtoto wa Hans Poppe aliyewahi kutuhumiwa
kwa kesi ya uhaini, lakini huyu yupo ndani ya Simba kwa muda mrefu.
Kihistoria, baada ya
kumaliza elimu ya sekondari, Zacharia alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) ambako alifikia cheo cha Kapteni, kabla ya kuachishwa kazi na kuhukumiwa
kifungo cha maisha jela, kwa tuhuma za uhaini, dhidi ya serikali ya awamu ya
kwanza, ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1983.
Lakini mwaka 1995,
Zacharia aliachiwa huru kwa msamaha wa rais wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan
Mwinyi, mwezi mmoja kabla hajamuachia Ikulu ya Tanzania, Benjamin William
Mkapa, rais wa awamu ya tatu.
Kama zinavyosema sheria
za nchi, mtu aliyehukumiwa kifungo, hana haki ya kugombea wadhifa wowote au
kuajiriwa tena, Zacharia naye hakuweza kurejea kazini, badala yake akaamua
kujiajiri, kwa kuanzisha miradi yake mwenyewe, ambayo leo ikiwa ni miaka 17
baadaye, miradi hiyo imesimama imara.
Alianza kuipenda Simba
SC mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na zaidi mwenyewe
anasema, mechi ambayo ilimfanya ajitamke rasmi yeye ni Simba damu ilikuwa dhidi
ya wapinzani wa jadi, Yanga Juni 23, mwaka 1973, ambayo Wekundu wa Msimbazi,
walishinda 1-0, bao pekee la Haidari Abeid ‘Muchacho’ dakika ya 68.
Zacharia aliendelea
kuwa mpenzi wa Simba, hadi baadaye akaamua kuwa mwanachama, lakini siku zote
alikuwa pembeni, hadi lilipoundwa kundi la Friends Of Simba ndipo akaamua
kujiunga nalo, ili naye aweze kutoa michango yake zaidi.
Wakati wa uongozi wa
Mwenyekiti, Hassan Daalal ambao ulionekana kuelemewa na majukumu ya timu, ndipo
Hans Poppe alipata umaarufu zaidi ndani ya Simba, kutokana na kusaidia zaidi.
Baada ya uongozi wa
Daalal kugundua umuhimu wake, ukampa jukumu la kusimamia fedha na alifanikiwa
kudhibiti fedha na kuanzisha mpango wa kuiwezesha klabu kujitegemea katika
mambo mbalimbali, ikiwemo suala la usajili badala ya kutembeza bakuli.
Kutokana na kufanya kwake
vizuri katika jukumu hilo, wengi miongoni mwa wanachama na viongozi wa Simba
wakamuomba agombee Uenyekiti, lakini sheria za nchi kwa sababu amewahi
kutumikia kifungo jela, zikambana.
Akiwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili, Hans Poppe amesaidia sana kuiwezesha klabu kukusanya fedha
na kutunza, ambazo zimeiwezesha klabu kujitegemea kusajili kwa takriban
asilimia 85. Na ni fedha ambazo
zimetokana na mapato ya milangoni, udhamini wa TBL, pango za majengo ya klabu
na mauzo ya wachezaji Mbwana Samatta, Patrick Ochan na Mussa Mgosi na nyingine
kutokana na michango wanayojichangisha..
Unaweza kuona kabisa,
F.O.S. imepata kiongozi mzuri, mwenye rekodi nzuri, busara, weledi na hekima na
vema zaidi ni mzoefu wa mikikimikiki, si mtu ‘laini laini’ na kwa kuwa ahadi
zake zimesikika na hilo ndilo tatizo kubwa kwa sasa, basi na ajue amebeba
matarajio ya wana Simba.
Wakati tunampongeza
Hans Poppe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa F.O.S., lakini anapaswa
kujua anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kurejesha imani ya kundi hilo ndani ya
klabu kwa ujumla. Alamsiki.
0 comments:
Post a Comment