Sendeu akimkabidhi jezi Kavumbangu leo Jangwani |
Na Prince Akbar
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu
ametambulishwa rasmi leo katika klabu yake ya Yanga, makao makuu ya klabu,
makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kukabidhiwa jezi namba
21.
Akimtambulisha mchezaji huyo, Ofisa Habari wa Yanga, Louis
Sendeu alisema kwamba mchezaji huyo kutoka Atletico Olympique ya Burundi,
amesaini mkataba wa miaka miwili.
Kavumbangu amefanya mazoezi leo na wenzake Uwanja wa Loyola,
Mabibo, Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza baada ya kutambulishwa kwenye mkutano huo,
Didier alisema anashukuru kutua Yanga, kwa sababu ni timu ambayo amekuwa
akiisikia muda mrefu tangu akiwa mdogo na atajitahidi kufanya vizuri,
kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo.
“Nimefurahi kuja Yanga, nimefurahia mapokezi mazuri, na mimi
naahidi nitafanya vizuri kuwafurahisha mashabiki,”alisema Kavumbangu.
Katika kikao hicho pia, mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi
alikanusha uvumi kwamba amesaini Simba. “Nina mkataba wa miaka miwili na Yanga,
hizo habari ni uzushi, mimi mchezaji wa Yanga,”alisema.
Yanga, ambao ni mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati,
walianza maandalizi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana na Kocha Mkuu
wa klabu hiyo, Mbelgiji Tom Saintefiet aliwataja wachezaji ambao hawajaanza
mazoezi ni Hamisi Kiiza, ambaye ameitwa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes,
Ibrahim Job na David Luhende ambao bado wapo kwao Mwanza, wakati Juma Abdul
bado ni majeruhi.
Tom alisema wachezaji wengine waliokosekana mazoezini jana
ni wale ambao wapo timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20,
Ngorongoro Heroes, Frank Damayo, Omega Seme na Simon Msuva.
Yanga ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Jumamosi
kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wafungaji Hamisi
Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hilo lilikuwa taji la tano la michuano hiyo kwa Yanga
kihistoria, baada ya awali kutwaa mataji ya Kombe hilo katika miaka ya 1975
Zanzibar, 1993, 1999 Uganda na 2011 Dar es Salaam na mara zote hizo, ikiwa
chini ya makocha wa kigeni.
Mwaka 1975 Yanga ilibeba Kombe hilo, ikiwa chini ya kocha
kutoka Jamhuri ya Kodemokrasia ya Kongo (DRC), Tambwe Leya (sasa marehemu),
1993 chini ya kocha kutoka Burundi, Nzoyisaba Tauzany pia marehemu, 1999 chini
ya Raoul Shungu kutoka DRC na mwaka jana chini ya Mganda Sam Timbe.
Wiki hii ziliibuka habari kwamba, baada ya kuipa Yanga Kombe
la Kagame,Tom ameomba kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Kenya, Harambee
Stars, lakini mwenyewe alisema baadaye akizungumza na BIN ZUBEIRY kwamba tangu
amejiunga na klabu hiyo mwezi uliopita hajawahi kuomba kazi sehemu nyingine
yoyote.
Mtakatifu Tom alisema anashangazwa mno na habari hizo za
kizushi, za kizandiki zenye kulenga kumchonganisha yeye na mwajiri wake, Yanga
SC.
“Nakumbuka niliwahi kuomba kazi Chama cha Soka Kenya (KFF)
kufundisha timu yao ya taifa (Harambee Strars), lakini ilikuwa ni muda mrefu
sana hata kabla sijaomba kazi Yanga,”alisema.
Blog moja iliyowahi kuandika Iddi Kipingu anagombea Uenyekiti
Yanga, wiki hii iliandika habari yenye kichwa kisemacho; “WIKI MOJA BAADA YA
KUIPA UBINGWA: KOCHA WA YANGA TOM SAINTFIET ATUMA MAOMBI YA KUIFUNDISHA
HARAMBEE STARS,”.
Akiizungumzia habari hiyo, Mtakatifu alisema; “Ni uongo,
tangu nimesaini mkataba na Yanga, sijawahi kuomba kazi pengine popote,”alisema.
Sendeu katikati, kulia Kavumbagu kulia na Bahanuzi kushoto leo asubuhi . |
Didier Kavumbangu tayari kakabidhiwa chumba klabuni |
0 comments:
Post a Comment