Coastal Union |
Na Mahmoud Zubeiry, Tanga
COASTAL Union imeibuka na ushindi wa bao 1-0
dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha katika mchezo wa kirafiki, kujiandaa na Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Bao pekee la mabingwa hao wa 1988, lilitiwa
kimiani na beki mpya aliyesajiliwa kutoka Simba SC, Juma Jabu dakika ya 32
baada ya kupanda mbele kusaidia mashambulizi akiteleza kutokea wingi ya
kushoto.
Katika mchezo huo, Suleiman Kassim 'Selembe' alikosa penalti dakika ya 26, baada ya Aziz Gilla kuangushwa kwenye eneo la hatari na refa Ibrahim Kidiwa kuamuru adhabu hiyo, lakini kipa wa Oljoro alipangua na pamoja na kiungo huyo Mzanzibar kuuwahi mpira kuupiga tena, lakini kipa huyo akaokoa tena
Huo ni ushindi wa kwanza wa Wagosi hao wa
Kaya, ndani ya mechi tatu zsa kujipima nguvu, ikitoka kufungwa 3-2 na Bandari
mjini Mombasa, Kenya na 1-0 dhidi ya Polisi mjini Morogoro.
Pamoja na ushindi huo, mashabiki wa Coastal
hawakuridhishwa na kiwango cha timu na kuanza kubeza uwezo wa makocha wa timu
hiyo, Juma Mgunda na msaidizi wake, Habib Kondo.
Habari za ndani zinasema kwamba Coastal
inafikiria kubadilisha benchi la ufundi kutokana na kutoridhishwa na uwezo wa
timu.
Coastal iliwekeza kwenye usajili wa kishindo, ikiamini
itafanya vizuri katika Ligi Kuu, lakini kwa matokeo haya ya awali tayari hofu
imeanza kuingia na wakati mashabiki wakitilia hofu uwezo wa makocha, wengine
wanatilia hofu uwezo wa wachezaji waliosajiliwa, wakiamini inaweza kuwa ni bora
kwa majina tu.
Kikosi cha Coastal kinaundwa na makipa; Juma
Mpongo, Abraham Chove na Rajab Kaumba, mabeki; Said Sued (Nahodha) Mbwana
Kibacha (Nahodha Msaidizi) Othman Omary, Juma Jabu, Ismail Suma, Jamal
Machelenga, Cyprian Lukindo na Philipp Mugenzi.
Viungo watakuwa ni
Jerry Santo, Razack Khalfan, Mohamed Binslum, Khamis Shango, Mohamed Issa,
Mohamed Soud, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Lameck Dayton, Joseph Mahundi, Aziz
Gilla na Shaffih Kaluani, wakati washambuliaji ni Nsa Job, Atupele Green, Danny
Lianga na Pius Kisambale.
Mbali na Kocha Mkuu,
mshambuliaji wake wa zamani, Mgunda, na
Msaidizi wake, beki wa zamani wa Pan African, Habibu Kondo, benchi la ufundi la
Coastal linakamilishwa na kocha wa viungo, mchezaji wake wa zamani, Ally
Jangalu na kocha wa makipa Bakari Shime.
Wagosi hao wa Kaya watakuwa na mechi mbili mfululizo mwishoni mwa wiki hii mjini Dar es Salaam, Jumamosi wakianza na Yanga na Jumapili na Simba SC Uwanja wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment