Ngassa sasa wa Azam |
Na
Mahmoud Zubeiry
MRISHO Khalfan Ngassa ameuzwa Simba kwa dau la Sh. Milioni
25 mchana wa leo, Azam imethibitisha.
Habari za ndani kutoka Azam, ambazo BIN
ZUBEIRY imezipata kutoka klabu hiyo, zimesema kwamba Simba wamelipa
fedha hizo na wamesainiwa fomu za uhamisho na sasa Mrisho anafuata nyayo za
baba yake Khalfan Ngassa, ambaye aliichezea Simba SC 1991/1992.
Azam ilifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya
mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya
Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC).
Na uamuzi huo, ni wa mzee Said Salim Bakhresa
mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa
bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka iwezekanavyo.
Ngassa alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba
wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga miaka miwili iliyoipita kwa dau la
Sh. Milioni 55, lakini wasiwasi unakuja kwamba, Ngassa ana mapenzi na Yanga na kwa
Simba kumsajili, kuna hatari yaliyotokea akiwa Azam, yatajirudia hata akiwa kwa
Wekundu wa Msimbazi.
Mapema leo mchana, Stewart Hall, kocha Muingereza wa
Azam FC jana alifukuzwa katika klabu
hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga
Mrisho katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY ilizipata kutoka ndani
ya Azam, zilisema kwamba kikao cha jana cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi
ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo
na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa
anafundisha timu ya vijana.
Habari zinasema kwamba, mapema baada ya mechi ya
Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na
kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na
kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea
Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu
kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya
kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Ngassa akisalimia mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao la pili dhidi ya AS Vita |
Sure Boy, ambaye ni mtoto wa kocha wa timu ya vijana
ya Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ jana hajafanya mazoezi na leo pia, naye pia
akituhumiwa kucheza kinazi katika mechi dhidi ya Yanga.
Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne
kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin,
Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji
na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
0 comments:
Post a Comment