John Bocco 'Adebayor' |
Na
Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael
Bocco ‘Adebayor’ amefuzu majaribio katika klabu ya Super Sport United ya Afrika
Kusini na Azam FC inataka dola za Kimarekani 200, 000, zaidi ya Sh Milioni 300
kumuuza.
Habari za ndani kutoka Azam FC, ambazo BIN
ZUBEIRY imezipata zimesema kwamba pamoja na kutaka Milioni 300, Azam
wametoa sharti la kupatiwa aslimia 15 Bocco atakapouzwa na klabu hiyo kwenda
klabu nyingine.
Bocco, ambaye amerejea nchini jana baada ya wiki mbili
za majaribio na Super Sport, inaelezwa yeye mwenyewe ni kama hajaridhishwa sana
na soka ya Afrika Kusini, kwani anaona kama haina ushindani na msisimko kama
soka ya Tanzania kwa sasa.
Pamoja na hayo, uongozi wa Super Sport unatarajiwa
kuja Dar es Salaam wiki ijayo kufanya mazungumzo na uongozi wa Azam, ili
wapunguziwe bei.
Hata hivyo, Azam inaonyesha haiko tayari kumuuza
mchezaji huyo chini ya dola 150,000 kwa sababu inaamini ni mchezaji bora ambaye
anaweza kununuliwa kwa bei nzuri zaidi na timu nyingine baadaye.
Inaoenakana Azam haina papara ya kumuuza Bocco kwa
sababu mbali na thamani yake halisi kama mfungajin bora wa Ligi Kuu, mchezaji
tegemeo wa timu ya taifa na klabu yake, lakini inaaminika kwa sasa mshambuliaji
mwingine aina ya Bocco Azam hawawezi kumpata kwa urahisi kwa namna yoyote.
“Mchezaji ambaye anaweza kufunga mara tatu katika
mechi moja dhidi ya timu ngumu hapa kwetu kama Simba au Yanga si mchezaji
rahisi. Hatukatai kumuuza, na hiyo ndio sera yetu, lakini lazima tumuuze kwa
bei ambayo itakuwa na maslahi kwetu,”alisema kiongozi mmoja wa Azam.
“Umefika wakati Watanzania lazima tuamke, Super
Sport haichezi mara kwa mara michuano ya Afrika na kwa ujumla, hakuna timu ya
Afrika Kusini inayofika mbali kwenye michuano ya Afrika. Na pia tujiulize
katika miaka mitatu iliyopita, Super Sport imeuza wachezaji wangapi Ulaya.
Tazama mtu kama Samatta (Mbwana) amenunuliwa na TP
Mazembe (ya DRC) kwa zaidi ya dola 150,000. Hiyo ni timu ambayo inacheza hadi
Klabu Bingwa ya Dunia, sasa wao Super Sport wana lipi la kutushawishi sisi na
mchezaji mwenyewe zaidi ya fedha? Wao walete fedha tuwauzie mchezaji, ili
tutafute mchezaji mwingine kama Bocco, Bocco ni lulu bwana,”alisema kiongolzi
huyo.
Super Sport ilivutiwa na soka ya Bocco, katika
michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
mwezi uliopita, hivyo kumuita kwa majaribio na kama Azam itamuuza, ataweka
historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kuchezea klabu hiyo, baada ya
Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea Simba SC.
Katika Kombe la Kagame, Bocco alifunga mabao matano
na kushika nafasi ya tatu katika wafungaji bora, nyuma ya Hamisi Kiiza na Said
Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora.
Lakini Bocco pia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, kwa mabao yake 18 akiwapiku hadi
washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo msimu huo, Felix Sunzu, Emmanuel
Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington Enyiana.
Tangu aipandishe Ligi Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009
kwa mabao yake, akiibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa
akiingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza
akizidiwa na Boniphace Ambani aliyekuwa Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi
aliyekuwa Simba na msimu wa tatu na Mrisho Ngassa, kabla ya msimu uliopita
kutimiza ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.
0 comments:
Post a Comment