Wachezaji wa Azam |
Na
Mahmoud Zubeiry
KATIKA kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii, washindi
wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Azam FC leo wanamenyana na Transit Camp
kwenye Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Azam ambayo ipo chini ya kocha mpya, Mserbia Boris Bunjak,
inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa
kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 8, mwaka huu, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam..
Kuchelewa kwa mechi hiyo ambako kumeenda sambamba na
kuchelewa kuanza kwa ligi hiyo, kumetokana na kuchelewa kufikiwa mwafaka mapema
wa mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu.
Mkataba wa awali wa Vodacom na TFF unafikia tamati
mwishoni mwa mwezi huu na kusainiwa mkataba mwingine, baada ya majadiliano
yanayoendelea.
Lakini kwa kuwa Mkutano Mkuu wa TFF uliopita
uliridhia kuanzia msimu ujao Ligi Kuu iendeshwe na kampuni itakayoundwa na
klabu za Ligi Kuu mjadala kuhusu udhamini mpya wa ligi umekuwa mrefu kutokana
na kuhusisha pande tatu, klabu, wadhamini na shirikisho.
Lakini sasa, kwa vyovyote, hata maridhiano ya
mkataba mpya wa udhamini na Vodacom yachelewe tena, mechi hiyo itachezwa
Septemba 8, ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya
Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa
soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba
kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001,
Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi
ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare
ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa
kuifunga Yanga mabao 2-0.
Wakati huo huo: Jana kikosi cha pili cha Azam, Azam
Academy kililazimisha sare ya bila kufungana (0-0) na Prisons ya Mbeya,
iliyorejea Ligi Kuu, kwenye Uwanja huo huo wa Chamazi.
0 comments:
Post a Comment