Wachezaji wa Azam |
Na
Prince Akbar
WACHEZAJI wa Azam na makocha wapya wa klabu hiyo,
pamoja na baadhi ya maofisa wa klabu hiyo, asubuhi ya leo wameangua kilio, tena
kile cha kamasi wakati wakimuaga aliyekuwa Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Muingereza
Stewart Hall ambaye alifukuzwa rasmi jana.
Wachezaji walioongoza kwa kilio Uwanja wa Chamazi
asubuhi ya leo, ni Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’,
Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Hajji Nuhu na Erasto Nyoni, wakati kwa maofisa na makocha ni Vivek Nagul.
Stewart mwenyewe pia alibubujikwa machozi wakati
anaagana na family yake, aliyoishi kwa zaidi ya mwaka kwa furaha, amani, upendo
na mafanikio.
Stewart alifukuzwa jana katika klabu hiyo kwa kosa
la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan
Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame dhidi ya Yanga.
Kikao cha juzi cha pamoja baina ya Bodi ya
Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kiliafiki kuvunjwa
kwa ndoa hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul
ambaye alikuwa anafundisha timu ya vijana, akisaidiwa na Kali Ongala.
Imeelezwa baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati
ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa
kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya
kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea
Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu
kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya
kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne
kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin,
Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji
na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
0 comments:
Post a Comment